Sunday, March 18, 2012

Heri upweke kuliko mpenzi asiyejua maana II

KILA mtu angeyaheshimu mapenzi, angejua jinsi ya kulinda hisia za mwenzi wake. Angeelewa maana ya kupenda, asigekuwa na shaka pale anapopendwa. Angeishi ndani ya mwenzake, hivyo kuumizana kusingekuwepo, migogoro mikubwa na kuachana isingetokea.

Migogoro mingi inatokea kwa sababu wengi wameyageuza mapenzi kama mchezo (game), hawajui kuwa saikolojia inaonya vitendo vya kuucheza shere moyo wa mtu. Kumfanyia hivyo mtu mwenye hisia za ndani na za kweli katika kupenda unaweza kuua bila kukusudia.

Katika sehemu ya kwanza ya makala haya nilieleza kuwa kama hujawa tayari kupenda, kunyenyekea na kuheshimu ni vizuri ukakaa pembeni kwa sababu unaruhusiwa kucheza game na mtu lakini ni kosa kubwa kucheza game na moyo wa mtu.

Hata hivyo, nilitaka kila mtu awe makini anapokuwa anaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu. Anapaswa kujihakikishia upendo kutoka moyoni badala ya kujaribu. Wengi walioingia kwa mtindo wa kupima kina cha maji, walilia kwa kusaga meno.

Lipo tabaka ambalo linakuwa limejitosheleza kuwa mapenzi hamna lakini wanang’ang’ania, matokeo yake wanauguza jeraha la moyo kwa muda mrefu. Wengine wakajipa ugonjwa wa moyo. Ni vizuri kuwa makini mno ikiwa unahitaji kupata thamani halisi ya penzi.

Pigania kuhifadhi moyo wako. Uweke katika himaya salama. Usijidanganye kwa penzi lisilo na uelekeo. Lenye sura ya upande mmoja. Wewe unapenda, yeye anakuchora, presha inakupanda na kushuka mwenzako hana habari hata kidogo, tena ikiwezekana atakucheka kama katuni.

Kuna watu hawaoni hili umuhimu, mpenzi maana yake ni msiri wa maisha yako. Unapokuwa umelala fofofo hujitambui, ubavuni kwako yupo yeye. Anaweza kukufanya lolote wakati wewe unaogelea ndotoni. Mpende akupendaye, vinginevyo utakumbana na maumivu yafuatayo;

HATAKUSIKILIZA IPASAVYO

Mapenzi ni hisia. Ni rahisi kwako kujua kwamba uliyenaye anakupenda kwa dhati mnapokuwa mnazungumza. Je, anakusikiliza kiasi gani?

Mtu ambaye hana mapenzi na wewe, hata umwambie kwa lugha gani hawezi kukuelewa. Tena inawezekana ulizungumza naye jana kwa herufi kubwa, lakini leo jua limechomoza anarudia yale yale.

Inawezekana ulimuonya kuhusu tabia ambazo zinakufanya heshima yake ipotee. Hakatazwi kuwa na marafiki wa jinsia nyingine, lakini mazoea yake siyo mazuri kiasi kwamba wanaweza kutembea barabarani wameshikana viuno. Ikiwa unamueleza habadiliki, huyo hakupendi.
Hakusikilizi kwa sababu hana hisia na wewe.

ATAPENDA KUKUFANANISHA

Haamini kama wewe ni mwanamke au mwanaume mwenye mvuto kamili. Akiona wengine barabarani ni rahisi kushawishika. Atajiuliza hivi huyu na wangu vipi? Huyu anaonekana ni mzuri zaidi. Anajiuliza maswali hayo kwa sababu hajakukubali. Shtuka mapema.

Mwanasaikolojia Brandon King katika makala yake: “Be aware with ones heart!” anasema kuwa ni rahisi mtu kujidanganya kwamba aliyenaye siyo chaguo sahihi kwa sababu yupo naye lakini hiyo hutokea kwa mtu ambaye mapenzi yake si asimilia 100.

Anasema: “Vitu vya thamani yeye huvichukulia ni rahisi. Hajui kama mpenzi wake ni wa gharama kubwa. Mtu wa barabarani labda kwa sababu tu amevaa kapendeza, yeye ataanza kumfananisha na mwenzi wake nyumbani na ikiwezekana kumuona bora.

“Wengine hawana uvumilivu, kwa hiyo wanaweza kujikuta wakimwaga sifa kwa watu wa pembeni. Wakiendelea huharibu kabisa kwa sababu hujikuta wakiwaeleza hata wapenzi wao, kitu ambacho taaluma ya saikolojia katika eneo la mapenzi inakataza.”

Brandon anaonya: “Ni kosa kubwa kumsifia mtu wa jinsia inayofanana na mwenzi wako mbele yake. Mfano unamwambia mwenzi wako wa kiume kwamba ‘yule kaka mzuri jamani’! Hata kama huna hisia za ndani ya moyo wako lakini haiwezi kumpa picha nzuri, atajiona hayupo salama kwamba unavutiwa na mwingine.

“Fikiria na wewe upande wako. Mwenzi wako anamuona mwanamke na yeye anamwagia sifa, ‘dah yule manzi mrembo, wewe ungekuwa mrembo kama yeye ningejidai sana’! Bila shaka utaumia sana, kwa hiyo na yeye ndivyo anavyoweza kupata maumivu.”

Anashauri: “Kila mmoja aridhike kwa jinsi mwenzi wake alivyo. Haikusaidii kitu kumuona bora wa jirani kwani kuna wenzako wanajiuliza huyo wako watampataje? Mheshimu na mtukuze mbele za watu. Ukijenga imani kwamba mpenzi wako ni bora kuliko wote duniani, itakuwa na moyo wako utakubali.”

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment