Thursday, March 15, 2012

JE, uhuru unaweza kukufanya uwe mwenye furaha?

JE, uhuru unaweza kukufanya uwe mwenye furaha? Uhuru unaweza kutupa furaha ya kweli maishani? Jibu la maswali haya ni ndiyo na hapana.

Ni vyema kufahamu kwamba furaha inayoambatana na uhuru inategemea na aina ya uhuru ambao unao. Unaweza kuwa huru katika sura mbili tofauti. Ukiwa huru kwa kuachana na dhambi na uovu, unaweza kuwa na furaha ya kweli. Lakini ukiwa na uhuru ambao hautokani na misingi ya uadilifu na wema, basi utakuwa katika mateso.

Jambo hili lina sehemu mbili ambazo zinaweza kumfanya mtu akawa mtumwa.Ukiwa mtumwa wa dhambi na uovu, utajikuta katika mateso, vilevile ukiwa mtumwa wa kutimiza matendo ya wema na ukarimu, utajikuta katika furaha ya kweli.

HAKUNA UHURU KAMILI


Jambo muhimu la kufahamu ni kwamba, katika hali halisi, hakuna uhuru kamili au utumwa kamili kwa binadamu. Siku zote tunapojiona tuko huru tufahamu wazi kwamba wakati huohuo tunakuwa watumwa.

Tofauti inategemea ni nani tunayemtumikia na nani ambaye hatumtumikii. Ukweli ni kwamba huwezi kuwa huru kwa kila kitu, kwani iwapo utakuwa huru kabisa, basi utajikuta umekuwa mtumwa wa kutokuwa na kitu chochote.

Hali ya kutokuwa na kitu chochote itakutupa katika mateso makubwa. Iwapo utahitaji uhuru kamili, basi utakuwa unataka kitu ambacho hakipo yaani hali ambayo haiwezi kuwepo au kupatikana.

HALI ITAKAYOKUFANYA UWE NA FURAHA


Uhuru utakaokufanya uwe na furaha ni uhuru wa kuachana na dhambi na maovu. Huu ni uhuru unaokutenganisha na chuki, fahari, wivu na maovu mengine.

Huu ni uhuru ambao utakupa amani na dhamira njema ya moyo. Kwa upande wa pili, utumwa unaweza pia kukufanya ukawa na furaha. Huu ni utumwa ambao utakufungamanisha na wema, upendo, uvumilivu na maadili mengine katika jamii.


Iwapo dhamira yako itaweka mbele kuheshimu vitendo vyema katika jamii, basi utakuwa umejiweka katika nafasi njema na yenye kukuletea furaha.

UHURU UTAKAOKULETEA HUZUNI


Uhuru ambao unaweza kukufanya uwe na masikitiko ni uhuru wa kutokuwepo kwa upendo, amani, ukarimu na mambo mengine ya kiadilifu. Hebu fikiria, iwapo utajitenga na vitu hivyo muhimu, unaweza kweli kuwa na furaha?

“Mimi sioni sababu ya kujitesa, bora niwe huru kwa kuishi peke yangu, kwani napata nini kwa kujipendekeza kwao zaidi ya kupoteza muda wangu na mali zangu.” Kauli hii ni ya kutafuta uhuru utakaokuletea huzuni baadaye.

NI NANI KIONGOZI WAKO?


Furaha yako ni kazi inayofanywa na pande mbili, yaani wewe na kiongozi au bwana wako. Ufahamu kwamba siku zote una mkuu wako anayekuongoza. Iwapo utakuwa umejitenga na maovu na ukawa mtu wa kutenda wema, basi wema au uadilifu ndiye bwana wako.

Iwapo utakuwa umeachana na matendo mema na ukawa mtumwa wa maovu, fahamu kabisa kwamba uovu ndiye kiongozi wako. Na iwapo utakuwa umetengana na wema na maovu, je bwana wako ni nani? Bila shaka anaweza kuwa ni wewe mwenyewe.

Ukiamini hivyo utakuwa unakumbatia kiini macho. Hii ni kwa sababu tukiwa tunaendelea kuishi, hatuwezi kuachana kabisa na mema na maovu. Mambo hayo mawili siku zote yatakuwa yanatuandama katika safari ya maisha yetu kwa kuyapenda au kuyachukia, kila mara yakitupa changamoto ya kuchagua upande tunaotaka kuutumikia.

TUNATAKIWA KUCHAGUA


Tunatakiwa tuchague aina ya uhuru tunaoutaka. Tunatakiwa tumchague bwana au kiongozi ambaye anaweza kutupa furaha ya kweli. Ni lazima tuchague upande wa kuutumikia.

Je, unataka kutumikia uovu au unataka kutumikia uadilifu? Au, je, unataka kujitumikia wewe na masilahi yako tu?

UPANDE MUHIMU WA KUUTUMIKIA


Inawezekana wapo watu kwenye jamii tunazoishi ambao wanatafuta uhuru kwa kujitoa kwenye matendo mema, yaani wanaona ni utumwa kuwasaidia wenzao na hivyo kuamua kutafuta uhuru kwa kujitenga au wanatafuta unafuu wa kupumzika katika majukumu ya kuwafanya binadamu wenzao wafurahie maisha.

Jambo hili si jema, kwani upande sahihi uletao furaha ya kweli ni kuwa huru mbali na matendo maovu. Asiwepo mtu miongoni mwetu ambaye atataka uhuru kwa kujitenga na mema eti kwa sababu wema unamtumikisha kwa kumchukulia muda na fedha zake.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment