Ni ngumu na kamwe siyo rahisi kumbadilisha mtu mwenye tabia ngumu awe rafiki. Badiliko hili lawezekana ikiwa mhusika (mwenye tabia ngumu) atadhamiria na kuwatayari kushughulika ili kubadilika.
Kwa hiyo kama ni ngumu au haiwezekani kumbadilisha basi jaribu kubadili mtazamo wako na jinsi unavyoishi naye au nao, kwasababu mara nyingi wewe ndiye unaye kwazika au kuumizwa wakati yeye (yule anayekuudhi) anafanikiwa na anaendelea na furaha yake tu.
Mawasiliano baina yetu na watu wengine yanajumuisha jinsi tunavyowafanyia wengine na jinsi wao wanavyotufanyia sisi (reaction and counter reaction). Kwa kubadili jinsi sisi tunavyowatendea wengine inaweza kubadili jinsi wao wanavyotutendea sisi. Hata kama ni kwa muda au kitambo kidogo tu. Hata kama hali hii haibadili hali kwa kudumu ila inaweza kurahisisha mazingira ya kuishi na mtu au watu wenye tabia ngumu.
Kila wakati lazima uwe na akili sana katika kuishi na watu wenye tabia ngumu, kama hutoweza kujizuia, na ukaanza kuwabwatukia basi itakuwa unaleta tatizo hasa pale ambapo mwenye tabia hii ngumu ni bosi wako. Je, utaropoka au kutukana kama ulivyozoea?
Hata kama mtu au watu wenyetabia hii wako ndani ya familia na yamkini ni wadogo kwako kiumri, bado kuropoka na kuwapayukia siyo suluhisho, hali hii yaweza kukugharimu.
Najua kila mmoja wetu anajinsi anavyofanya kwa mtu au watu wenye tabia ngumu. Wote hatuna namna moja, mmoja anaweza kuwa ni mkimya na mwenye ujasiri hata anapoudhiwa, mwingine hupayuka na kumjibu yule anaye muudhi, mwingine anaamua kulia tu anapoudhiwa, wako wanaozira na kuamua kutozungumza tena na aliyewaudhi, wapo ambao husambaza habari mbaya kuhusu huyo mwenye maudhi, wako ambao huamua kumwambia uso kwa uso jinsi walivyo kwazika, sijui staili yako ni ipi.
Ni rahisi sana kuumizwa au kuudhiwa na maneno au matendo ya mwingine, na mara mtu huyo anapojua kuwa unaumia yeye hupata nguvu, hii huwa ndiyo silaha yake muhimu pale mnapopambana.
Unachotakiwa kufanya ni kuwaachia wakati wote wao wawe washindi, kamwe usitafute kushindana nao, utaumia mwenyewe. Njia pekee ni kujitahidi kuwa mjanja na mwenye akili kuliko yeye na pia kuwa na ushawishi katika yale wanayotaka kuyatenda hata pasipo wao kugundua.
Je, unawajibu vipi watu hawa (How do you react?)
Ni jambo jema kuanza kujitazama jinsi unavyowatendea wengine na jinsi tunavyoshughulika na wale wanaotukwaza. Kumbuka kuwa jinsi unavyoikabili hali hiyo katika mazingira fulani inawezekana isiwe hivyo katika mazingira mengine.
Watu wenye tabia ngumu na zinazotatiza mara nyingi huweka mitego ya maneno au matendo na kwa kiasi kikubwa unaweza kunaswa na kuwaruhusu wakuchezee jinsi watakavyo, na kati ya vitu wanavyo vipenda na kuvitamani ni kukuona unalia na kuumia na kuchanganyikiwa. Kwahiyo fikiri kwanza kabla hujafanya chochote mbele yao.
Watu watabia hii mara zote huwachukulia na kuwatendea watu wote sawa kwa hiyo usifikiri kila alichosema au alichofanya kwako ni cha kibinafsi sana na alikikusudia kwako. Angeweza kufanya au kusema hivyo hivyo hata kwa mwingine aliye karibu naye wakati ule. Kwa kufahamu hili itakusaidia kupunguza maumivu yanayoletwa na hisia zako kwake.
Hembu jiulize ni jinsi gani umewahi kukabiliana na mtu au watu wa jinsi hii, na je ilikuwa ni kwa jinsi ya kuumiza au kuelemisha? Fahamu kwamba kujibu kwa kupayuka, kutukana au kubishana haisaidii, bali kunakushusha chini ya miguu ya yule aliye kusababishia maumivu hayo, na sasa atakuwa anafurahia na kukuona wewe mjinga.
Ni chaguo lako, la ni jinsi gani utakabiliana na mtu au watu wa aina hii, ingawa unaweza kuchagua njia bora itakayoweza kukusaidia kukuimarisha na kupunguza udhaifu wako, zaidi ya kuamua kuchagua njia ambayo itakuacha umeumia, umechoka, umekatishwa tamaa na umejeruhika moyo.
Hii haimaanishi uwe mtu wa kusema ndiyo tu kwa kila kitu na kila mtu, na haimaanishi kuwa hutakiwi kukasirika HAPANA, hasira ni asili na haina tatizo lolote hapa, ila tu matokeo ya hasira hiyo ndiyo yanayoweza kuleta shida. Je ni jinsi gani unakabiliana na hasira yako na unaionyeshaje? Kwa fujo, kupayuka kubishana, kulia, kuvunja vitu, kunyamaza n.k.
Ili Kujua jinsi watu wenye tabia ngumu wanavyokuathiri. Jiulize maswali yafuatayo:
Je, ni unataka kutawaliwa na wengine?
Najua jibu ni kwamba hakuna nayetaka kutawaliwa na mwingine, na ndiyo maana unaweza kujikuta unabishana au kushindana na huyo anaye kukwaza.
Tatizo ni kwamba mwisho wewe ndiyo unaumia na yeye anabaki kufurahia kwa kukushinda mfano; tazama fujo za madereva barabarani hususan wale wa daladala.
Nikweli unahasira naye, lakini je hiyo ni njia muafaka ya kumkabili? kumbuka mwishoni atakayeumia ni wewe.
Fikiri kama unatatizo la shinikizo la damu kama utakubali kuyumbishwa kihisia na tabia mbovu za mwingine wewe ndiyo utabaki unaumia na siyo tu kama hutoweza kufanya vile moyo wako utakavyo bali pia utaachwa ukijihisi kuchoka, kuumizwa kwa hisia zako mwenyewe na kukatishwa tamaa na tabia yako wewe mwenyewe.
Nini Mwitikio wako pale unapoudhiwa? (Haswa na yule mwenye hasira na wewe)
Je, unalipa hasira kwa hasira?
Je, unajitetea na kuukimbia ukweli (being defensive)
Au unajificha kutoroka au kumkwepa?
Njia zote hizi hapa juu siyo nzuri.
Hata kama una haki ya kukasirika, lakini bado atakayeumia unabaki kuwa ni wewe. Na siyo tu utaumizwa na kukasirishwa kwa tabia yake mwenye kukuudhi bali utaumizwa moyoni mwako kwa vile wewe ulivyotenda, dhamiri itakushtaki zaidi (guilty conscious).
Je, unajizumgumziaje wewe mwenyewe, vibaya au vyema?
Mfano: Ukweli mimi najichukia haswa ninapofikia kipindi cha mitihani au usaili.
Hivi mimi nikoje?
Hivi kwa nini nimeumbwa hivi?
Kamwe mimi siwezi kufanya lolote jema!
Wakati wote mimi ni mtu wa bahati mbaya tu!
Wala huhitaji kujichukia unapofikia wakati wa mitihani au usaili, unachohitaji kufanya ni kujiandaa mwenyewe vizuri na kuwahi mapema katika eneo la tukio.
Hisia potofu na zisizojenga ambazo tunajiwazia wenyewe mara nyingi hutupotezea muda na mara tunapoziruhusu hutuharibia siku yetu nzima.
Unafanya nini unapopingwa? (what do you do when you are criticized)
Wako watu wanaopendelea kupinga wengine katika kila kitu, hata katika vile visivyostahili kupingwa,hakuna chochote chema kinachoweza kusemwa na yeyote, bali yeye peke yake. Hata kama kilichosemwa kina ukweli kwa asilimia kubwa basi mtu huyu atajitahidi walau kurekebisha hata lugha tu, ili mradi kisipite hivihivi bila yeye kukipinga japo kidogo (hawa ndiyo wale wenye tabia ngumu).
Hali hii huwapa kufurahi na kujijengea nguvu kwa jinsi wanavyopinga wengine.
Ni kweli upinzani mwingine ni wa ukweli na unajenga lakini hapa nakazia wale wanaopinga ili tu kujifurahisha nafsi zao na kuwafanya wale wanaowapinga waumie mioyo.
Je, unapopigwa, unajibuje? Je, unajitetea au unajishusha na kukubali kila kinachopingwa kwa kuamini kwamba anayekupinga yuko sawa na kwa hiyo unayameza maoni yako yote, bila kuchambua kwa kina mapingamizi hayo.
Kuna jinsi ambavyo unaweza kumkabili au kumjibu anayekupinga na ikawa kama umeweka petroli kwenye moto, upinzani utawaka na hata kuleta ugomvi, lakini pia iko njia ambayo unaweza kumjibu mtu huyu na ukanyamazisha fukuto lote.
Je, una mtazamo hasi (mtazamo usiofaa) na wa kudumu katika kitu fulani?
Mfano; Labda unasema “Mambo yangu hayaendelei tangu nihamie katika nyumba hii, au mambo yangu yanakwama tangu nimuoe au niolewe na huyu, ni matatizo tu tangu tuoane, watoto hawa hasara tupu.” n.k.
Mtazamo huu hasi, waweza kukugharimu siyo tu kukunyima raha bali pia waweza kuharibu hisia zako na za wengine pia.
Ukijikuta katika hali hii ni vyema kujifahamu na kujitahidi kuelewa nini tatizo husika na jitahidi kubadilisha mtazamo wako.
Tafuta vile vitu ambavyo unaweza kuvitazama katika mtazamo chanya hata kama ni vidogo. Tafuta kuviongelea vile unavyovipenda zaidi ya vile usivyovipenda.
Je, unazimeza hisia zako zote, nzuri na mbaya?
Je, unaona ni ngumu sana kusema “nakupenda” “umependeza” “umeniudhi” n.k. labda unaweza kusema neno moja tu na siyo lingine. Wengi wetu tumekuzwa katika mazingira ambayo tunahofu kusema chochote ili tu tusije tukamkwaza mtu, hata kama tunaumizwa au tunajisikia vyema kusema kitu fulani, lakini tunajizuia.
Badala yake tunakwenda kusemea pembeni. Yamkini kunyamaza kunaweza kuwa na faida katika baadhi ya mazingira lakini siyo hata katika kukubali vitu visivyofaa. Hakuna ubaya wowote katika kuelezea jinsi unavyojisikia moyoni mwako ili mradi tu unaeleza kila unachokihisi kwa hali njema na siyo kwa hasira au shari. Katika hali hii kamwe hutowapoteza marafiki zako, na kama kuna yeyote aliye rafiki atasumbuliwa na hili basi usihofu, kubali tu kumpoteza kwa kuwa hakuwa wa muhimu au wa msaada sana kwako.
Hali ya kujifanya hujaumia au hujakwazika na wakati umekwazika na unalia ndani kwa ndani inaumiza na kufanya ujisikie vibaya sana. Inakufanya uzidishe mazingira ya msongo wa mawazo (stress) hasa pale unapojiwazia wewe mwenyewe zaidi ya kushughulika na wale waliokuudhi. Mtazamo wako jinsi unavyojiona wewe mwenyewe huathirika sana, na pia waweza kujisababishia tatizo hasa pale wale wenye tabia ngumu watakapo kugundua kuwa huwezi kusema chochote hata ukiumizwa na hii itawafanya wakugeuze mpira wa kuchezea.
Je, wewe ni kati ya wale wanaojiamini kusema chochote wanachokifikiri bila kujali matokeo yake?
Hebu fikiria jinsi unavyojisikia pale ambapo mtu au watu wengine wangefanya hivyo hivyo kwako. Je, unataka kuwasababishia wengine maumivu ya moyoni? Kusema chochote kinachoshuka toka kichwani mwako kupitia kinywani mwako bila kufikiri juu ya matokeo au athari zake kwa wale wanaokusiliza au waliokuzunguka kunaweza kukupotezea marafiki na kuishusha hadhi yako kwa urahisi sana.
Mara nyingi mtu wa jinsi hii huweza kujikuta akiwa pweke na anayepingana na ulimwengu (kila mtu anamchukia). Hii ni kati ya hisia za kuhuzunisha na kuumiza sana muda wote, lakini pia huumiza zaidi pale unapogundua kuwa ni maumivu uliyojitakia mwenyewe. Peke yako unajikuta umetengwa na mtego wa kihisia na kukuzamisha usipoweza kujikwamua tena.
Saturday, March 17, 2012
Jinsi ya Kuishi na Watu Wenye Tabia Ngumu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment