Saturday, March 17, 2012

Kwanini mipango yako haikamiliki

Bila shaka wakati unasoma makala haya, una mipango ya kujenga nyumba, kuoa, kujitegemea, kufanya biashara, kusoma, kuanzisha kampuni na kutafuta kazi na inawezekana huu ni mwaka wa tatu, wanne au wa kumi pengine kujafanikisha mipango yako.
Mpaka sasa hujui ni kwa nini miaka 13 imepita tangu uajiriwe, lakini huna hata cha kuwaonyesha jamaa kama mafanikio ya kazi yako. Kichwani una mipango mingi, lakini imeshindikana kutekelezeka.

Kisaikolojia katika kila kushindwa kuna sababu nyingi sana, ambazo mtu akizitumia anaweza kupata nafuu ya maumivu yatokanayo na kushindwa kwake. Duniani kuna watu wengi ambao wameridhika kabisa na hali za kutofanikiwa, kisa wanasababu ya mshahara mdogo, hawana kazi au hawajasoma.

Msomaji wangu, hata wakati unasoma makala haya una sababu zako za msingi kabisa ambazo nikikuuliza kwa nini ulifeli mitihani unaweza kuniambia. Hakuna ubishi mwenyewe umeziamini na bahati mbaya zaidi ukimsimulia mtu mwingine naye atakuambia: “Aisee pole sana kulikua hakuna namna zaidi ya matokeo hayo.

Taifa, ukoo, watu hawafanikiwi miaka nenda rudi, si kwa sababu hawajapanga kufanikiwa, la! Bali wameacha kubeba mzigo wa KUSHINDWA kwao ili waumie na kuongeza nguvu ya kutafuta na kujikuta wanakumbatia SABABU zinazowafanya wajione walikuwa na haki ya kukosa jambo fulani katika jamii.

Hivyo jibu la haraka na la msingi linalochangia watu kushindwa kukamilisha mipango yao ni KUSHIKA SABABU na KUIACHA HALI YA KUSHINDWA ikiuawa. Kitaalamu ili mwili uongeze nguvu ya kufanya jambo kwa kiwango kikubwa ni lazima upewe nia ya ushindi. Lakini mtu akikata tamaa na kusema “Aah! Siwezi kwa sababu 1,2,3 mwili nao huipokea taarifa hiyo na kulegea.

Wakati tunaendelea kujifunza kuhusu hili, ni vema kila mmoja akawa anajiuliza mwenyewe kwa nini hajafanikiwa. Hapo tunaweza kupata sababu nyingi ambazo tunaweza kuzigawa katika makundi mengi, lakini hitimisho la yote litapunguza orodha ndefu na kubaki na makundi mawili tu ya sababu hizo nayo ni MTAZAMO na WOGA.

Ifahamike kuwa wapo wanaoshindwa kufanikiwa kwa sababu, mitazamo yao ina kasoro ya kupunguza ukubwa wa vitu. “Mimi mshahara wangu mdogo.” “Sina uwezo wa kufaulu hesabu.” Ukoo wetu ni maskini hatuna uwezo,” na mifano kama hiyo ambayo inaweza kumfanya mtu akajiona duni kwa sababu tu amepungukiwa kitu au hali fulani ambayo angekuwa nayo kwa ukubwa anaofikiri angeweza kufanikiwa.
Lakini anashindwa kujua kwamba, kuna waliofanikiwa kutoka katika udogo huo huo anaoupa yeye kama sababu ya kutofanikiwa kwake.

Hii ina maana kwamba alivyotazama ni tofauti na alivyofikiri mwenzake mpaka akafanikiwa licha ya kuwa na mshahara mdogo pengine kuzidi hata anaopokea yeye kwa mwezi. Huu ni MTAZAMO!
Kwa upande wa sababu ya aina ya WOGA, kifo ni adui wa maendeleao ya wengi. Watafuta maisha wengi wanatazama usalama wao zaidi ya mafanikio yao, hata kama kuna jambo wanaweza kulifanya likawasaidia lakini wanaogopa kufa. “Machimboni siwezi kwenda, juzi watu wamekufa mgodini.” “Ile ni kazi ya hatari sana tunaweza kufa.”

WOGA ungepewa kipaumbele na wanasayansi, ulimwenguni tusingeona ndege zikiruka, tusingepata chanjo na tiba ya magonjwa, kusingekuwa na silaha za maangamizi na magari yasingetembea barabarani kwa sababu ya waendeshaji kuogopa kupata ajali.
Kukumbatia woga na kuacha kujaribu kufanya mambo ni sababu ya kutofanikiwa kwetu kama vijana tunaotegemewa na taifa kuliendeleza.

Naamini mitaani kuna vijana wanaogopa, kuondoka kwenye familia zao na kujitegemea, wakihofia kushindwa kuendesha maisha yao na hivyo kuona ni bora waitwe ‘kula kulala’ kwa miaka 40, kuliko kutafuta chumba na kuanza maisha ya kujitegemea.

Nakumbuka hata mimi nilipata shida sana kuishinda hofu ya kujitegemea, lakini nilipoyapa mafanikio sehemu ya kwanza na kuiweka kando hofu, leo nimefikia hatua nzuri ya kimaendeleo ambayo sikuwa nayo kabla na jamii sasa inaniheshimu.

Hapa tunajifunza kwamba, licha ya sababu kuingilia mipango yetu ya kimaisha hatutakiwi kuipa nafasi ya kututawala akili zetu, badala yake tushikilie mafanikio kuwa NIA yetu ya KWANZA.Tukifanya hivyo tutajikuta tunashinda sababu moja baada ya nyingine na kupata tunachotamani maishani mwetu.

Maisha yetu yameyumba baada ya kudhurumiwa, hilo ni sawa, lakini nia yetu ibaki kuwa ni mafanikio, tuanze moja na sababu itufundishe kutorudia makosa. Tumetetereka kimaisha tulipoachwa na waume wetu, nakubali, lakini tusikubali sababu hiyo itufanye tuwe duni mpaka jamii itucheke: “Ana nini siku hizi, tangu kaachwa kawa kama chokora.”

Tumefeli masomo kwa sababu ya mikwamo ya kimaisha, shule tulizosoma ni dhaifu, hatukuwezeshwa ipasavyo, zote hizo ni sababu za msingi, lakini tunachotakiwa kufanya ni kuziweka kando na kubaki na nia ya kufaulu mitihani.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment