Saturday, March 17, 2012

Mambo ya kuhuzunisha na njia sahihi za kukabiliana nayo kisaikolojia-5

Jambo la mwisho la kuzingatia tunapoanza hatua mpya za kuelekea katika ushindi ni kutorudia makosa. Kama kufeli kwako mtihani kulitokana na kutosoma kwa bidii, usirudie kosa hilo.

Ongeza bidii katika masomo au kama umeshindwa kujenga nyumba kwa sababu ya kuwa na matumizi makubwa ya pesa, usikubali kuendelea na matumizi hayo, badala yake jibane na utimize malengo yako.

MKE KUANZA/KUACHISHWA KAZI
Inaelezwa katika uchunguzi wa kitaalamu kuwa wanaume wengi huhofia wake zao kuanza kazi. Hii inatokana na wivu wa kimapenzi. Wanaume hudhani kuwa mke anapokwenda kuajiriwa atakuwa na nafasi kubwa ya kushawishiwa kuanzisha uhusiano mpya na wanaume wengine.

Lakini ukweli ni kwamba huzuni hii mara nyingi huwa ni ya bure na matokeo yake huzaa wivu ambao husambaratisha ndoa na uhusiano. Kitu cha msingi kinachotakiwa kufanywa na mwanaume ni kuwa karibu na mkewe, kumjengea hali ya kujiamini na kumtimizia yote anayostahili kama mke, likiwemo tendo la ndoa na ukaribu ambao mara nyingi unatajwa kuwa tiba kubwa ya usaliti.

Aidha kwa wale ambao wake zao wanafukuzwa kazi, jambo la muhimu ni kutiana moyo na kushirikiana kwa ukaribu kutafuta kazi nyingine. Hili linatakiwa kwenda sambamba na kujaliana wakati wote wa tatizo. Hali yoyote ya kumtenga na kumwacha mkiwa ni hatari kwa uhusiano.

Pamoja na hilo endapo kipato cha mwanamke kilikuwa ni sehemu ya matumizi ya nyumbani basi mume na mke wanawajibu wa kukaa pamoja na kupanga upya matumizi yao ili kuendana na kipato kilichopo baada ya mwanamke kufutwa kazi.

KUANZA/KUMALIZA SHULE
Wanafunzi wengi wanapopata nafasi ya kuanza shule kwa hatua yoyote ile, hujawa na hofu ya kuweza kukabili mazingira mapya. Inashauriwa kuwa mwanafunzi anapokwenda kuanza shule lazima awe tayari kubadilika kufuatana na mazingira na asiwe mtu wa kuogopa changamoto atakazokutana nazo shuleni.

Suala hili limeelezewa kwa kina katika kipengele cha mwanafunzi na mazingira ya shule ambacho kipo ndani ya Kitabu cha Saikolojia Namba 2.

Hata hivyo, wanafunzi ambao wanamaliza shule wanashauriwa kutohuzunishwa na hilo, badala yake wawe tayari kujifunza maisha kutoka kwa ndugu wanaoishi nao.

MAISHA KUBADILIKA
Hali ya maisha inapoporomoka huhuzunisha, lakini kinachotakiwa katika kukabili tatizo hili si huzuni bali kuwa tayari kutazama kilichochangia kushuka kwa maisha hayo na kukitafutia ufumbuzi wa haraka.

Hata hivyo, watu wengi wanaelezwa kuwa wamekuwa waathirika wa tatizo la kuporomoka kwa maisha kutokana na ubinafsi kwa kutokuwa tayari kubadilishana mawazo na watu wengine katika kupata ufumbuzi wa tatizo na kuhakiki mipango ya maisha yao. Utakuta mtu akipata pesa basi anaamua mwenyewe kuanza biashara bila hata kupata ushauri kutoka kwa watu, hili ni jambo baya.

Ifahamike kuwa kubadilika kwa hali ya maisha ni dalili ya kuwepo kwa makosa makubwa katika mipango ya kimaisha, hivyo basi kila mtu anayepatwa na tatizo hili anatakiwa kutafuta msaada wa mawazo kutoka kwa wataalamu au rafiki, ili apate mbinu za haraka za kujinasua, kwani kuhuzunika peke yake hakufai.

KURUDI KWENYE MAKAZI YA AWALI
Mtu anapokuwa amehama nyumbani na kwenda kuanzisha maisha yake sehemu nyingine na baadaye kushindwa na kurudi nyumbani kwa wazazi au maskani yake ya mwanzo humfanya ahuzunike. Kinachomhuzunisha si kitendo hicho, bali ni hisia za kudhani kuwa atadharauliwa au kuchekwa na watu.

Hili linaweza kuwa kweli, lakini huzuni pekee haisaidii kuondoa tatizo. Wakati mwingine mbinu za kijeshi zinaelekeza kuwa unaposhindwa kusonga mbele na ulipobakiwa na hatari ya kifo, hatua za kurudi nyuma hustahili kutumika.

Kurudi huku hakupewi maana ya kushindwa, bali kujipanga katika kushambulia kwa nguvu. Kwa maana hiyo mtu anaposhindwa kuishi peke yake na akabaini kuwa kuwepo kwake katika maisha mapya ni kifo, kurudi nyumbani si kosa, kinachotakiwa ni nia ya kujipanga kuelekea katika ushindi mpya.

USUMBUFU WA BOSI KAZINI
Usumbufu wa mabosi kazini umekuwa ukiwafanya watu wengi kufikia hatua ya kuacha kazi, kuhama vituo au kufanya kazi kwa kiwango cha chini. Hali hii huwapata zaidi wanawake ambao wanafanya kazi na mabosi wanaowataka kimapenzi. Usumbufu wa kutongozwa sambamba na kitisho cha kufukuzwa kazi vimekuwa ni huzuni kubwa kwa wanawake wengi makazini.

Wanawake wengi wanakiri kwamba kutongozwa na bosi ni kero ambayo haikwepeki hasa pale hisia za kimapenzi zinapokuwa hazipo kwa mtu husika. Wengi kati ya wanawake hukiri kufanya mapenzi na mabosi wao si kwa sababu wanawapenda bali kwa lengo la kulinda kazi ambayo huwa hatarini pale maelewano na bosi yanapoyumba.

Ukweli ni kwamba uamuzi wa kuwa mtumwa wa mtu kwa sababu ya kazi ni aibu kwa binadamu ambaye ameumbwa na uwezo, utashi na nguvu za kukabili matatizo. Njia pekee ya kukabiliana na tatizo hili, kwanza ni kuwajibika katika majukumu kama mfanyakazi na pili ni kujiamini na kujipenda.

Unapowajibika ipasavyo unakuwa na ulinzi wa kazi yako si tu kwa yule unayemfanyia kazi, bali hata kwako mwenyewe kwa vile utakuwa na hoja za kujitetea kisheria.

Lakini pia kujiamini na kujipenda ndiyo nguzo ya kukulinda wewe na ushawishi usiokuwa na tija kwako. Mfanyakazi lazima awe na msimamo wake kuhusu kazi anayoitumikia ili asiyumbishwe na kitisho cha kufukuzwa kazi, kwani ajira kwa wachapa kazi zipo nyingi katika ulimwengu huu.

Mwisho ni kujipenda. Yaani kuwa mwanadamu mwenye utashi na kutokuwa tayari kuuza utu kwa sababu ya kazi. Endapo bosi atakuja na sera za kutongozana kazini, lazima aambiwe kwa uwazi kuwa hilo haliwezekani na yeye auone msimamo wako.

Akitambua hilo hataweza kuleta usumbufu ambao hatimaye utamkosesha yeye mfanyakazi na kumtia aibu katika jamii. Lakini kufuata hatua za kisheria ni jambo linalofaa pia.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment