Saturday, March 17, 2012

Namna ya kuishughulikia na kuishinda hofu II

Katika kulijibu swali hili utaweza kutathmini kwa kujiuliza kuwa “Ni nini katika maisha yangu ambacho nimekipa kipaumbele zaidi kuliko afya yangu na Maisha yangu? Maana ya swali hili ni ukweli kwamba kama una hofu katika jambo fulani maana yake hilo jambo au hicho kitu umekipa umuhimu au uzito usiostahili kuliko maisha yako.

Je ni jambo gani au kitu gani umekipa umuhimu au uzito usiostahili katika maisha yako? Je ni kazi yako?, Je ni elimu yako? Je ni ujenzi wa nyumba? Je ni kibali kwa watu? Je ni watoto wako au mwenza wako? Je ni malipo ya mkopo uliouchukua? Kumbuka haitakusaidia wala kukuongezea chochote kwa kujiua ukikiwaza hicho kitu, mwisho mwenye hasara ni wewe.

Hata mwisho kama hautapoteza maisha yako lakini ukadhoofisha afya yako, faida yake ni nini? Na afya yako ikipotea, nini tena utakifanya kuyanufaisha maisha yako?

Kama hofu yako ni kwenye kupata kibali machoni pa watu wanaokuzunguka, labda ofisini, chuoni, mtaani nk. Kumbuka kuwa watu hao wala hawatajali au kukukumbuka pale utakapokuwa unaugulia wodini au nyumbani kwako kisa ni magonjwa yanayohusiana na hofu.
Labda mfano huu waweza kukusaidia zaidi kuelewa ninachomaanisha.

Kijana mmoja alimuuliza swali mwanafalsafa (philosopher) mmoja akisema, “Nini kinachokushangaza sana kwa huyu kiumbe binadamu?”

Mwanafalsafa alijibu “Ninamshangaa sana kiumbe mwanadamu kwa sababu hupoteza afya yake kwa kiasi kikubwa sana akitafuta pesa, na baadaye hutumia pesa yake yote akiitibu au kujaribu kuirejesha afya yake iliyopotea katika hofu za maisha.

Kwa kuihofia kesho yake, mwanadamu huyu ametumia muda wote wa sasa akijiandaa na hiyo kesho, na matokeo yake, kwa kuichosha sana afya yake ameshindwa kuifurahia leo yake na hata hiyo kesho yenyewe huiona kwa taabu sana” (Mwenye ufahamu na afahamu).

Acha kuyapa mawazo yako au mitazamo yako umuhimu usiostahili.
Hofu, woga na hamaki za mara kwa mara ni alama kwamba unayapa mawazo, fikira na mitazamo yako umuhimu usiostahili. Maana yake ni kwamba kila unaloliwaza au kulifikiri unalichukulia kuwa ni halisi, ingawa mara nyingine ukweli ni kwamba unavyowaza sivyo.

Hakuna ukweli wala uthibitisho kuwa kila unachokiwaza kitatokea.
Hizi twaweza kuziita fikra laini, pale ambapo unadhani kuwa kila unachowaza kitatokea.

Mtu mwenye ukichaa, akiwaza kuwa kuna mtu anataka kumpiga risasi atakimbia huku na huko kujificha. Wakati ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho. Wewe siyo kichaa, kwa nini uweke vyote unavyoviwaza kama vile ni dhahiri? Tena hususan vile vitu vibaya?

Tabia sugu nyingi walizonazo watu husababishwa na fikra, vile wanavyowaza. Usiruhusu mawazo yako yakufanye mtumwa.

Mawazo ya kitaalamu yanaonesha kwamba kama ukiweka mawazo yako sana katika kitu fulani, inaweza kuishawishi tabia au utendaji wako katika hali ambayo yaweza kuanza kufanya hofu zako kuanza kuwa kweli.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment