Miongoni mwa vitu muhimu katika maisha ya mwanadamu ni kupata furaha. Watu wengi wamekuwa na harakati nyingi za kuhakikisha kuwa wanafurahika katika kuishi kwao. Kuna wanaotafuta furaha kupitia kwa rafiki, wapenzi, ndoa zao na hata jamii zao. Ni wazi kwamba kila afanyalo mwanadamu kupitia maamuzi yake, msingi wake huwa ni kutafua furaha, hii haijalishi kama atafanya jambo mbaya au zuri kwa mtazamo wa watu.
Ifahamike, watu wanavuja jasho katika kufanya kazi kwa sababu wanahitaji mshahara au pato ambalo baadaye hulitumia katika kufurahi. Wasomi, wafanyabiashara nao wanapohangaka katika hili na lile ukichunguza utakuta nyuma yao kuna kiu ya furaha.
Hii ina maana kuwa, furaha ndiyo jambo pekee ambalo watu hulitafuta zaidi. Ni nadra au pengine hakuna mtu ambaye kwa akili timamu ana kiu ya kupata mabaya na kuhangaika kuyatafuta. Mara nyingi yakimtokea basi huwa yamejitokeza tu katika safari yake ya kutafuta furaha. Wezi, majambazi, wazinifu hata watukanaji wote kwa pamoja wanapofanya hivyo huwa nyuma yao kuna hitaji la kupata furaha.
Pamoja na shabaha ya binadamu kuwa katika kutafuta furaha, wengi wao wamekuwa hawaipati kwa sababu hawajui njia za kuipata. Kuna watu wanahangaikia utajiri, wakidhani wakiupata, basi watakuwa na furaha, lakini baada ya kupata utajiri huo hujikuta hawana furaha. Wengine huamua kuoa, kuwa na wapenzi na marafiki lakini nao matokeo huwa tofauti na malengo.
Ingawa kuna matatizo mengi ambayo yanajitokeza katika maisha ya watu kila siku ambayo huondoa furaha, lakini si sababu ya moja kwa moja ya kumfanya mtu ahuzunike, eti tu kwa maana kafikwa na tatizo. Ukichunguza kwa makini utafahamu kuwa furaha si kitu ambacho mtu anaweza kukipata na kikamtosha. Unaweza kupata kila kitu lakini ukawa huna furaha.
Ukisema pesa ndiyo furaha, unaweza kuzipata lakini usifurahike na ukashangaa watu ambao ni masikini wakawa na furaha tele. Hivyo basi msingi wa furaha ni uelewa wa namna ya kuitafuta na kuipata. Swali, furaha inapaika wapi na katika vitu gani? Nibu ni kuishi kwa kuzingatia muongozo ufuatao:
Unaitafutaje furaha?
Watu wengi wanapopata matatizo huwa hawakubali kuyapokea. Kuna mfano wa mtu mmoja ambaye alikuwa bosi katika kampuni, siku moja uongozi wa juu uliamua kumshusha cheo kutoka ukurugenzi hadi mpokea wageni. Bosi huyo alipotelemshwa cheo kwa kiwango hicho hakujiona duni kwa wafanyakazi wenzake, badala yake alichofikiri yeye ni kwamba watu wote wanamuunga mkono na kumsikitikia kwa unyama huo wa kushushwa cheo kupitiliza.
Zile fikra za kuhurumiwa na watu zilimfanya awe na furaha na akawa mtu wa kuwahi kazini kila siku ili watu wakamuone na kumsikitia, jambo ambalo aliamini kuwa uongozi uliomshusha cheo ndiyo unaopata aibu mbele ya jamii na wala sio yeye. Kitendo hicho cha kuwahi kazini na kuonekasna ni mtu mwenye furaha kilimfanya awe mtu wa pekee kwenye jamii, aliweza kutengeneza maswali mengi kwa watu na hatimaye minong’ono ya kuonewa ilianza kusikika.
Kilichotokea hatimaye, kampuni moja kubwa ilipata habari ya kuwepo kwa mtu wa aina hiyo, ikafanya mawasiliano naye na kumwajiri, bila kujali kashfa zilizokuwa zimemwengua katika wadhifa wake wa kwanza. Jamaa huyo alipopata ajira mpya alijirekebisha makosa yake ya kugushi na wizi kwa vile alikuwa amejifunza kilichokuwa kimempata. Bosi huyo aliweza kuendesha kampuni hiyo kwa mafanikio makubwa, jambo lililowafanya wakuu wake wa zamani wajute kumuondolea wadhifa.
Hapa tunajifunza kuwa tunapopata matatizo kinachotufanya tupoteze furaha ni fikra zetu, lakini tukijua kucheza nazo na kuzielekeza katika mlango wa pili, tunaweza kuyatumia matatizo yetu kupata furaha pia. Lazima kila mmoja wetu atambue kuwa matatizo ni shule, tunapoyapata tunajifunza. Lakini hatuwezi kujifunza tukiwa na msongo wa mawazo, lazima tufanye unafiki fulani wa kimawazo kama alioufanya bosi aliyeshushwa cheo, yeye hakuangalia wadhifa wake wa zamani, wala namna gani watu wanamtazama katika kazi yake mpya. Mawazo yanawezaje kutuletea furaha?
Katika hali ya kawaida hakuna mtu hata mmoja anayeweza kumwambia mwenzake lia naye akafanya hivyo. Kila siku tunaona na kusikia mengi kutoka kwa ndugu, rafiki, waalimu wahubiri, wachungaji mapadri wetu na hata kwenye vyombo ya habari, lakini kusikia huko hakuna maana kuwa ni lazima kutuondolee furaha, kwani ndani ya akili zetu kuna kitu muhimu ambacho ni maamuzi yetu.
Utawala wa mawazo yetu ni kazi ya kila siku na uamauzi wa nini ha kufikiri ni suala ambalo lipo kwenye uwezo wa mwanadamu mwenyewe. Ingekuwa ni lazima kila wazo baya tunaloliona na kulisikia lazima lituhuzunishe basi tusingekuwa na furaha hata kidogo katika maisha yetu, kwani hakuna siku ambayo itapita bila kuona, kusikia au kutendewa jambo baya na mtu mwengine.
Ajali zinatokea kila siku, watu wanakufa, wanaugua, wanateseka, wanalia, wanaomboleza na kufanyiana hila, lakini kwa nini hatuyachukulii matukio yote kwa uzito sawa kiasi ha kulia? Ni kwa sababu tuna uhuru wa kuchagua tulie kwa sababu ya nani na kwa nina? Na hii ndiyo silaha pekee ya kuyatumia mawazo kutuletea furaha. Yaani kuchagua lipi la kutuliza na lipi la kutufurahisha na mwisho wa yote tuna uwezo wa kuyatumia mawazo yetu kuchagua mambo ya kufurahisha na kuyapa kipaumbele, bila kujali ni mema au mabaya. (Kumbuka mfano wa bosi aliyeshushwa cheo).
Hivyo ni vema wakati tunapokuwa na mawazo ndani yetu tukazingatia misingi ifuatayo ambayo inaweza kutusaidia kufikia uamuzi sahihi juu ya kila tunaloona na kulisikia, ili mawazo yasitufanye tuhuzunike na badala yake tufurahi. Kwanza ni kujipenda wenyewe. Tukijipenda hatutajihukumu na kujiona duni mbele ya wenzetu na hivyo kutopoteza furaha. Pili ni kujiamini, kuamini huku kutatuwezesha kuwa na msimamo juu ya maamuzi ya kila tunachoshibishwa ndani ya mawazo yetu kupitia mawasilia ya sauti na yasiyo na sauti.
Tatu, kumiliki mawazo yetu yasichukuliwe na ukubwa au udogo wa tatizo. Udhibiti huu lazima uyaone mambo yote yanayoingia kichwani kuwa ni ya kawaida kwa vile yapo duniani na yanawakuta watu kama sehemu ya changamoto za kimaisha. Katika hali ya kawaida ukubwa au udogo wa tatizo unatokana na mawazo ya mtu husika. Nne, kuwa na uvumilivu juu ya kila jambo kwa imani kuwa hakuna marefu yasiyokuwa na ncha. Tano na mwisho ni kuhakiki maamuzi yetu kama yako sahihi kabla na baada ya kutenda jambo.
Kutojiheshimu kunavyohatarisha furaha yetu?
Ni muhimu kila mtu akaishi kama yeye alivyo, lakini linapokuja suala la kuchangamana na ulimwengu, lazima kuwe na kitu cha kujifunza kwa sababu huwezi kuishi nje ya familia na watu wengine.
Kwa msingi huo ili mtu aweze kupata furaha lazima afahamu namna atakavyoweza kujisahihisha tabia yake kwa kujiheshimu yeye na kuwaheshimu wengine anaoishi nao. Kwa maana kuishi kama mtu anatakavyo bila kutazama wengine ni jambo baya. Hivyo dokezo zifuatazo ni muhimu kwa kila mtu kuzifahamu ili kuondoa mkwaruzano kati ya mtu na mtu.
A –Wafanyie wengine mema
Furaha haiwezi kuja kama mtu hajiheshimu mwenyewe na kuwafanyia wengine mema ambayo angependa atendewe. Watu wengi wamekuwa hodari kutembea na wake za watu, kuiba, kudhuru, kutukana, kudharau wengine na hata kunyanyasa, bila kugeuza upande wapili wa shilingi na kufikiri endapo wangefanyiwa wao hali ingekuwaje, si wangepoteza furaha? Sasa kama jibu ni ndiyo kwa nini wao wawe mahodari kuwaumiza wengine? Ni wazi kwamba kila mwanadamu angekuwa makini kufanya yale ambayo angependa kufanyiwa, kiwango ha huzuni kingepungua, na hii ndiyo changamoto kubwa kwa mtu atakaye kupata furaha lazima awafanyie wengine wema kwanza kabla ya yeye kufanyiwa.
B – Kuwa kiongozi
Katika maisha kuna watu ambao hawaelewi kuhusu matumizi ya mawazo na namna ya kutenda kama binadamu, hivyo kwa wale ambao wanaelewa nini maana ya maisha ni vema wakawa viongozi kwa wengine, viongozi katika kusamehe, kukubali kosa, kutenda haki na kusimamia ukweli.
C- Kushukuru
Ni watu wachache sana ambao hushukuru wafanyiwapo mabaya, lakini inashauriliwa kwamba ili kuuita furaha na kupunguza nguvu ya huzuni ni bora mtu akajifunza kushukuru hata kama amefanyiwa jambo baya.
D - Kuwa na juhudi
Mambo yote tunayoyafanya lazima yaambatane na juhudi. Ikiwa tunatafuta majibu ya nini tunataka kifanyeke katika kupata furaha lazima tuwe na bidii, tusifanye vitu kwa uzembe kwani matokeo yake ni kushindwa ambako kutatuingiza katika shida ambazo zitatuhuzunisha. Umeolewa jitahidi kulinda ndoa yako, jitahidi katika kazi na kila jambo ili usikwame.
E- Kuchunga ulimi
Kuna watu wengi ambao wanapoteza furaha kwa kutojua namna ya kutumia ndimi zao. Utakuta mtu yuko katika kati ya watu, anatukana na wakati mwingine kutamka maneno ambayo wenzake hayawapendezi. Kujiheshimu ni pamoja na kuchuja maneno ya kusema mbele za watu kulingana na mahitaji yaliyopo, kuropoka ropoka kuna madhara. Kabla hujasema kitu tafakari kama usemecho kitaleta furaha au huzuni.
Kanuni za kuifikia furaha ya kweli
Wakati wa kutafuta furaha ya kweli lazima kujiuliza baadhi ya kanuni za kimaisha kama unazifuata kwa ufasaha, vinginevyo unaweza kuwa mtafuta furaha lakini usiwe miongoni mwa wanaoipata. Kama nilivyosema awali kuwa, kuna watu hutafuta furaha kupitia kwa wake/waume zao, rafiki, wapenzi na hata kwenye mali, lakini mwisho wa siku wanapokuja kutafakari zaidi hujikuta hawana furaha waliyoitaraji wakati wakihangaikia njia za kuipata.
Kuna watu ambao mawazo yao yanatamani sana kupata mtoto na wengine wameapa kabisa kwamba wakifanikiwa kushika ujauzito watakuwa na furaha, lakini bado kama hawatakuwa makini wao wenyewe watajikuta wanapata furaha ya muda na hatimaye kutoweka na kuanza kujutia harakati zao, huku wakianza safari mpya za kufuata furaha kupitia jambo jingine. Hebu tujiulize maswali haya.
A-Je tunapokuwa tunatafuta furaha tunatumia uwezo wetu wote au kwa kiwango kidogo? Kama tunatumia kiwango kidogo basi tujue kuwa hata kama tutapata kitu tunachodhani kitatufurahisha utajikuta hatufurahi, kwa sababu hatutafanikiwa au tutakuwa na furaha ya muda tu kwa vile nia yetu hatukuijaza kikamilifu ili tuweze kupata furaha timilifu
B- Je tunafanya sawa katika maamuzi au tunabahatisha tu? Endapo tutakuwa tunafanya mambo ya kubahatisha ambayo hatujayahakiki, huzuni yetu itakuwa kwenye makosa na kamwe hatuwezi kufanikiwa kupata yale tunayotaraji yatufurahishe. Kuna watu wanatafuta watoto lakini hawazingatii kalenda za mimba na wengine wanatafuta mali, elimu kubwa, mke mwema, lakini hawako makini katika kufanya maamuzi kwa usahihi. Ni vema tukathibitisha uchaguzi wa mambo ili tufanikiwe kupata yatakayotufurahisha.
C- Je tunatimiza wajibu wetu au tunadanganya? Wapo watu ambao walitamani kuoa ili wapate furaha, lakini walipofanikiwa katika hilo hawakutimiza majukumu yao wakajikuta wanageukwa na wake/waume zao na kujutia uamuzi wao. Msomaji wangu, unapokuwa katika safari ya kutafuta furaha kupitia utajiri, elimu, uongozi ni vema ukatimiza wajibu wako, ili upate matokeo mazuri. Maana kama utakuwa unatamani kufaulu mtihani wako halafu husomi kwa bidii, sina shaka majibu utakayopata yatakuhuzunisha kwa sababu lazima ufeli na furaha uliyotaka haitapatikana.
D- Je tunafuata muongozo, au tunakiuka? Kila jambo tunalotaka kulifanya lina kanuni zake, ukitaka kupika ugali upo muongozo ambao unakutaka uwe na vifaa, uache maji yachemke na hata kutoharakisha upishi wenyewe, lengo ni kupata matoke mazuri. Sasa kama tutakuwa kupata furaha ya kudumu kupitia mambo fulani ni lazima tuyafanye kwa kufuata muongozi na si kwa kukurupuka. Biashara, elimu, kazi, zote hizi zinamiongozo ambayo lazima kuifuata kwa matokeo mazuri.
E- Tunatumia tulivyopata au tunavitelekeza? Wapo watu ambao hutamani kupata kazi, lakini wanapopata hawazitumii, kazi hizo kwa ukamilifu, badala yake wanakuwa watu wa kufanya ujanja ujanja ujanja kwa kutoroka na wakati mwingine kutojihusisha na shughuli nyingine kwa lengo lile lile la kutafuta furaha. Kusema kweli mtu wa namna hii hawezi kuwa na furaha kwa sababu anayolenga yamfurahishe hayatumii kufurahika na badala yake anatafuta jambo jingine. Fikiria kuhusu mume, anaoa lakini anaacha kumtumie mke wake wake anakwenda kwa hawara! Hili si jambo jema na kamwe haliwezi kuleta furaha kupitia mambo tunayoyatafua. Soma vifungu hivi ndani ya kitabu cha Biblia: “Vitu vyote ni halila, bali si vitu vyote ifaavyo. (1 Wakorintho 10:23).” “ Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi (Yakobo 4:17)”
Thursday, March 15, 2012
Njia za kutafuta na kupata furaha
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment