Unaweza  kuona ni kama swali la kipuuzi lakini lazima lipate jibu. Katika  uchunguzi wangu kuna kitu ambacho nimekigundua, katika mapenzi ya sasa  hivi eti wanajiita kwenda na wakati (dot com). Kumekuwa na tabia ya  kukosekana kwa uaminifu, watu wamekuwa wakizungukana, hata marafiki.
Hii  imekuwa ikiwakuta wasichana wengi hasa wanafunzi ambao wamekuwa  wakiingia katika mapenzi bila kujua nini hasa maana ya mapenzi. Wengi  wao huona kuwa na mpenzi ni fasheni, kumbe mapenzi ni maisha kamili,  ambayo kama utafanya vibaya huenda ukavuruka mpangilio wako wote wa  maisha yako.
Nia yangu kubwa si kuwagusa wanafunzi ambao wamekuwa  ndiyo wanaongoza kwa kuuliza maswali juu ya penzi lao kukosa muelekeo.  Naomba twende pamoja ili tujue njia ya mapenzi ni ipi ambayo siku zote  itakufanya uwe na penzi salama. 
Siku zote unapoanza mapenzi hakikisha yule unayetaka kumkabidhi  dhamana ya moyo na mwili wako yupo vipi. Usikurupuke kwa vile umeambiwa  unapendwa, kuutoa mwili wako kwa mtu si jambo la mzaha hata kidogo.
Chukua  muda wako kupata undani wa mtu anayetaka kuuhifadhi moyo wako, kwani  kosa lako linaweza kukutia kwenye mateso makubwa. Japo kumjua mpenzi wa  kweli yahitaji kutumia muda mrefu, lakini ni vizuri kuvuta subra kabla  hujatoa uamuzi.
Pia unapokuwa umeanzisha uhusiano jiepushe  kuchanganya wapenzi, anaweza kutokea mtu ambaye hakika moyo wake ulikuwa  radhi kufanya lolote hata kuachika kwa ajili yako. Lakini bahati mbaya  umo ndani ya ndoa au ndani ya penzi miliki.
Mapenzi yana njia  moja, penzi la kweli ni lile ulilomo na wala si la pembeni. Sawa na  mashindano ya riadha ya mita 100, ukikimbia katika mstari wa mwenzako  utakuwa umefanya makosa.
Mwenzako akigundua hilo, huo ndiyo utakuwa mwanzo kutafuta njia ya kukuacha.
Makala  haya yanawagusa watu wote walio kwenye ulimwengu wa mapenzi ili kujenga  uhusiano ulio imara. Jiepushe kujirahisi hovyo, si kwamba unapendwa  bali unajishushia heshima yako.
No comments:
Post a Comment