Thursday, March 15, 2012

Wazazi na Mafanikio ya Kimasomo

Uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na baadhi ya mashirika yanayojihusisha na malezi ya watoto ulimwenguni akiwemo Daktari Janet Gonzalez Mena wa Marekani umebaini kuwa wazazi ndiyo mwanzo hasa wa mafanikio ya watoto wao na kwamba wengi kati ya vijana wanaoshindwa katika maisha kushindwa kwao kunaanzia ndani ya familia zao.

Malezi ya wazazi kwa tafsiri sahihi ndiyo yanayomkuza mtoto na kumtambulisha katika jamii kwamba yeye ni nani? Tunawapata watu wa kabila la Wanyamwezi, Wayao, Wamakua, Wamakonde kwa sababu wamezaliwa na kulelewa na wazazi wa makabila hayo.

Pamoja na yote, kuzaa peke yake yakusimamii tabia ya mtoto, bali kulea. Waswahili husema: “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Kwa bahati mbaya wazazi wengi wamekuwa hawaelewi kuwa wao ndiyo wenye jukumu la kumtayarisha mtoto awe mwema na mwenye uwezo wa kufikiri.

Hali hii inatokana na kutokuwepo kwa elimu inayotoa somo la jinsi ya kuwalea watoto bila kuwaharibia ufahamu na kuwadumaza katika uelewa wa mambo.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, wazazi ambao ndiyo wenye uchungu na watoto wametajwa kuwa chanzo cha watoto kushindwa kukabiliana na changamoto za kimaisha pamoja na masomo.

Ukichunguza kwa makini watoto wengi wanaokuwa mbumbumbu darasani (nazungumzia wale wasiokuwa na kasoro za kibaiolojia) ni wale ambao wazazi wao hawakuzingatia mambo yafuatayo katika kuwalea tangu walipokuwa wadogo hadi kukua kwao.

HUDUMA BORA

Wazazi wengi hasa wa dunia ya tatu wanakabiliwa na tatizo la uzazi holela, usiozingatia uwezo wa kulea na kuwapatoa huduma muhimu kwa watoto. Mfano lishe bora, mavazi na malazi. Wanasayansi wanasema chakula bora ndicho kinachoweza kuimarisha ukuaji wa viungo vya mtoto na kuufanya ubongo uwe katika hali nzuri ya kumudu kutafsiri mambo.

Hivyo ni jukumu la mzazi anayetaka mtoto wake awe na uelewa mzuri darasani ahakikishe kuwa anampatia mwanae chakula bora kitakachomjenga afya na kumuwezesha kuwa na mwili wenye nguvu ya kukabili magonjwa ya kitoto. Lakini sambamba na hilo mzazi anatakiwa kusimamia afya ya mwanae kwa kumpeleka hospitalini mara kwa mara kutibiwa na kushauriwa.

UTAMBUZI WA KIPAJI

Jambo la pili ambalo ni muhimu kwa mzazi ni kutambua mapema kipaji ha mtoto na kumuongoza sawa na kipaji chake. Ingawa shule nyingi nchini (Tanzania) hazitoi elimu ya ngazi ya chini lakini baba na mama bado wanawajibika kujua ni elimu ya kiwango gani kutoka shule gani itamfaa mtoto wao.

Inashauri kwa mzazi kumtambua mwanae ana uelewa gani, ili ajue namna ya kumsaidia ili afikie kiwango bora cha uelewa. Kwa mfano mtoto akiwa na uelewa wa chini anatakiwa kupelekwe kwa waalimu wazuri wenye uwezo wa kumsaidia anaposhindwa, haifai mtoto wa aina hii kupelekwa shule za ilimradi na kudhani huko atasoma na kuelewa.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment