NI imani yangu kuwa, si wote wanafahamu kwa undani aina nne za watu  katika ulimwengu wa mafanikio, jambo ambalo naamini linachangia kwa  kiasi kikubwa kuwafanya hawa wafanikiwe kimaisha na wengine wasifanikiwe  kabisa.
Kwa kufahamu hilo, nimeona ni vyema nikaandika makala haya  kuhusu aina za watu katika ulimwengu wa mafanikio ili kuamsha akili za  watu katika kukabiliana na changamoto nyingi za kimaisha.
Kwenye  ulimwengu wa mafanikio binadamu wamegawanyika katika makundi manne  ambayo ni WATENDA USAHIHI, WANAOLIDHIKA, WANAOTAKA KUPENDWA NA WASHINDI.  Naomba tufuatane katika kuangali kwa undani aina hizi za watu ili  kuanzia leo kila mtu afahamu yupo kundi gani.
WATENDA USAHIHI: Ni  watu ambao katika maisha yao huwa hawataki kukosea au kuonekana  wayafanyayo si sahihi. Watu wa aina hii huwa ni wagumu sana kufanya  jambo ambalo akili zao hazihakiki kuwa litamalizika kwa mafanikio.
Kikwazo  kikubwa kwa watu wa aina hii mara nyingi ni kusitasita katika kuamua.  Ni watu wa kuogopa macho ya watu hasa suala la kushindwa kutimiza  malengo linapowajia akilini. Kinachowaogopesha zaidi watu wa kundi hili  ni kuabika mbele za watu jambo fulani likiwaharibikia.
WANAORIDHIKA:  Kundi jingine la watu katika ulimwengu wa mafanikio ni wale  wanaoridhishwa na hali zao na kwamba hawahitaji mabadiliko ya aina  yoyote kwenye maisha yao. “Ndugu yangu, hali hii tumeizoea, mwaka wa  nne.” Wamezoea maisha magumu.
Hata hivyo, wapo wanaozoea kazi na  majukumu yao ya kila siku kiasi kwamba hawataki kubadilika, hawapendi  kuongezeka zaidi ya hapo walipo. Utakuta uwezo wa mfanyakazi alioanza  nao miaka 7 iliyopita ni huohuo mpaka leo. Wafanyakazi wengine wanaweza  kuajiriwa nyuma yake wakajitahidi kusoma, kujifunza kazi na kupanda vyeo  na kumwacha mridhikaji yuko palepale. Kundi la wanaoridhika.
WANAOTAKA  KUPENDWA: Kuna watu katika maisha yao wanataka kumfurahisha kila mtu  kwa lengo la kuvuta upendo wa wanadamu wenzao. Utakuta maisha yao yote  ni kuwatumikia wengine kutoa fedha za maendeleo kwa kumsaidia huyu na  yule kwa malipo ya kupendwa na jamii.
Ni wazi kuwa watu wanaoishi  katika kundi hili hawawezi kufanikiwa kwa sababu kipato chao kingi  hukitumia katika kuwafanya watu wengine wafurahi na si kusukuma mbele  maisha yao ya kila siku.
WASHINDI: Kundi la mwisho la watu ni  wale ambao katika maisha yao ya kila siku hupenda kufika kwenye kilele  cha mambo yote wanayofanya. Hutamani kufanikiwa zaidi na zaidi,  hawakubali jambo liwashinde, kila walichokusudia kukifanya huhakikisha  kwamba wanakabiliana na changamoto zote na mwisho wa safari kupata  ushindi.
Baada ya kuangalia hayo, ni vema kujiuliza; Je ni sahihi  kutokuwa makini katika mambo yako ama kuridhika na mafanikio  uliyoyapata? Inawezekana kweli mtu akaacha kusaidia wenzake kwa hofu ya  kuwa katika kundi la tatu? Jibu ni hili:
Ni vema mambo matatu  ya  mwanzo yakaongozwa na la nne yaani USHINDI. Kwa maana hiyo kila mmoja  wetu lazima awe mtu ambaye anatamani sana kufanikiwa katika maisha yake  ya kila siku.  Watu wote wakiwa na nia hii wataweza kuyapita makundi  mengine matatu kwa uangalizi mkubwa.
Hawatakubali wawe makini  wasifikie malengo, hawataacha kujaribu bahati kwenye mambo ambayo akili  zinaona ni magumu, hawataridhishwa na mafanikio au hali walizonazo na  hawatakubali kutumika kama kuwafurahisha watu bali kila kitu watafanya  kwa kiasi kwa lengo la kufika katika mafanikio sahihi.
Haya dunia yako, chaguo ni lako. Asante kwa kuwa nami.
Thursday, March 15, 2012
Aina 4 ya watu katika ulimwengu wa mafanikio
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment