Thursday, March 15, 2012

Mambo ya muhimu ya kuzingatia kwenye maisha ya kila siku III

WIKI hii tunamalizia mada yetu ambayo huwa tunaeleza mambo ambayo yatasaidia kutuwezesha kuishi kwa mafanikio na furaha zaidi.
Nakuomba uendelee kutafakari kila dondoo ambazo nitaziandika hapa chini kwa ufupi sana kama ifuatavyo:

Usijihangaishe na jinsi watu wanavyokufikiria : Usitake maoni ya watu wengine yakakuzuia kufanya jambo fulani, utayatia maanani tu pale unapotaka kujitokeza kwa kishindo kama vile kwenye usaili, kukutana na mtu mwingine kwa mara ya kwanza, na kadhalika. Mambo ambayo watu huyafikiria na kuyasema kuhusu wewe si muhimu. Muhimu ni vile ambavyo wewe mwenyewe unajihisi.

Acha nia ya kutaka kudhibiti kila kitu: Maisha ni muujiza usiotabirika. Hali inaweza kuwa nzuri au mbaya leo, lakini hatuwezi kufahamu kwa asilimia 100 hali hiyo itakuwaje baadaye. Hivyo itumie vyema zaidi fursa iliyo mbele yako na mengine mwachie Mungu.
Acha kufanya kitu kilekile kila mara: Ili kukua ni lazima upanue uwezo wako wa kuona mbali na kujiondoa katika mazingira ya raha. Ukiendelea kufanya kitu kilekile, basi utaendelea kuvuna hichohicho ambacho unakivuna kila siku.

Usikubali kufuata njia ya kutatua mambo kirahisi: Maisha si rahisi hususani unapotaka kupata mafanikio makubwa na yenye thamani. Usitake kukimbilia ufumbuzi wa haraka wa matatizo. Fanya kitu ambacho si cha kawaida, yaani kile ambacho hujawahi kukifanya.
Usitake kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja: Fanya kila jambo kwa wakati wake na hakikisha unalifanya vyema.
Acha kufikiri kwamba watu wengine wana bahati kuliko wewe: Fahamu kwamba ukifanya kazi kwa nguvu zaidi, ndivyo utakavyokuwa na bahati zaidi.

Usijibebeshe majukumu mengi mno: Ni vyema mtu kuwa peke yako na ni vyema wakati mwingine kutofanya jambo lolote. Hivyo, utumie muda wako kwa kutafakari mambo mbalimbali na kupumzisha mwili na akili.
Acha kufanya maamuzi ya kukurupuka: Usikubali busara yako ikavurugwa kwa kufanya mambo kwa kukurupuka. Tulia na tafakari mambo yote kabla ya kufanya uamuzi ambao utaleta mabadiliko katika maisha yako.

Usifanya makosa kwa makusudi kwa vile hayatakuletea madhara: Usifanye jambo lolote makusudi kwa vile tu halitakuletea madhara yoyote. Fikiria mambo yote kwa mapana zaidi na ufahamu mwisho wake utakuwaje. Fanya kile ambacho moyoni unaamini ni kitu sahihi.
Usilifikirie kabisa jambo ambalo hutaki likutokee: Elekeza mategemeo yako katika mambo ambayo unataka yakutokee. Fikra njema ndiyo silaha ya mafanikio yote makubwa. Ukiamka kila asubuhi na fikra kwamba kitu fulani kizuri kitakutokea maishani mwako leo na ukakiwekea maanani, utakuja kugundua kila mara kwamba fikra hizo ni sahihi.

Acha kujiona umebanwa na majukumu kila siku: Kuna watu wachache hupenda kujiona wana majukumu kila siku. Hata hivyo, jaribu kufurahia maisha na kupata burudani kila unapoweza.

Acha kuyapitisha maisha yako ukifanya kazi ambayo huipendi: Ukifanya kazi ambayo huipendi ni lazima maisha yatakuwa mafupi sana kwako. Chaguo la kazi sahihi hutegemea jambo moja; Kupata na kuifanya kazi ngumu ambayo unaipenda. Hivyo, ukijikuta unafanya kazi nzito lakini unaipenda, basi endelea nayo. Ukifanya hivyo, utakuwa unaelekea kwenye neema, kwani kazi ngumu inakuwa si ngumu kama unaipenda.

Usifikirie vitu ambavyo huna: Kubaliana na kitu chochote ambacho unacho, kwani watu wengi huwa hawana bahati ya kupata vitu wanavyovipenda.
Mwisho.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment