Wiki iliyopita tulieleza mambo kadhaa ambayo yatasaidia kutuwezesha kuishi kwa mafanikio na furaha zaidi.
Nilikuomba msomaji utafakari kwa kina dondoo zile lakini kwa kuwa hazikwisha, zinaendelea leo katika safu hii na nitazifasiri kwa ufupi sana kama ifuatavyo:
Acha kuyakuza mambo madogo: Moja ya njia za kufahamu mambo muhimu ni kujiuliza swali hili; “Je, jambo hili litakuwa muhimu katika kipindi cha mwaka mmoja? Litakuwa muhimu katika miaka mitatu au mitano ijayo? Kama jibu ni hapana, basi huna haja ya kuhangaika nalo.
Usifanye jambo kwa kutegemea matarajio ya wengine badala yake fanya jambo lako kikamilifu na ikiwezekana livuke matarajio yako. Baada ya hapo mambo yote yatajinyoosha yenyewe.
Usikimbilie ufumbuzi mwepesi wa matatizo yako: Hivi sasa watu wanakimbilia kupata ufumbuzi wa haraka wa matatizo yao. Kwa mfano, watu wanakimbilia kumeza vidonge vya kupunguza uzito badala ya kufanya mazoezi na kula chakula bora. Ukweli ni kwamba hakuna maajabu ambayo yanashinda nguvu za mtu kufanya bidii, kujiwekea malengo na kufanya kazi kwa nguvu.
Usitoe ahadi utakazoshindwa kuzitimiza: Usitoe ahadi zitakazokushinda. Timiza unalolifanya kwa kuzidi hata lengo ulilojiwekea.
Usikubali fikra na hisia zako zikakubana moyoni: Watu hawawezi kumsoma mtu na kutambua mawazo yake. Hawatafahamu unavyojihisi mpaka uwaeleze. Hivyo, waeleze watu wengine shida zako.
Acha kusema jambo kwa kufichaficha: Jambo unalotaka kulisema liseme waziwazi na hakikisha unajieleza kinagaubaga.
Usitake kuzuia mabadiliko: Kwa vyovyote, hali ikiwa nzuri au mbaya sasa, ni dhahiri baadaye itabadilika. Hili ni jambo la wazi. Hivyo kubaliana na mabadiliko na fahamu kwamba mabadiliko huja kutokana na sababu zake. Mwanzoni hayawezi kuwa mepesi au ya wazi, lakini baadaye yatakuwa ya maana.
Usifikiri una haki katika jambo fulani: Hakuna mtu mwenye haki maalum katika dunia hii. Sote tuko sawa. Tunavuta hewa ileile. Tunapata kile tunachotoa kwa wengine. Tunapata kile tunachokitokea jasho.
Usisubiri kufanya jambo hadi dakika ya mwisho: Watu ambao wanashindwa kupanga, hupanga kushindwa.
Usitake kujionyesha sana: Usitake kujiingiza katika mambo ya watu wengine na usitake kujionyesha kwa wengine bila sababu ya maana.
Acha uvivu: Ushughulishe mwili wako! Fanya matembezi marefu ya kujinyoosha mwili au tenga dakika 30 kwa ajili ya kufanya mazoezi mbalimbali nyumbani kwako au sehemu wanazofanyia watu mazoezi (Gym).
Usile vyakula ambavyo havina faida mwilini mwako: Fahamu kwamba kile unachokula ndivyo kinaufanya mwili wako uwe ulivyo sasa.
Acha tabia ya kula kama vile ni moja ya burudani: Usile chakula wakati hujisikii kufanya hivyo.Kula wakati ukiwa na njaa tu.
Achana na tabia za kipumbavu ambazo unajua kabisa ni za kipumbavu: Usisome huku unaendesha gari. Usitumie kilevi halafu ukaendesha gari. Usivute sigara wakati unaendesha gari na kadhalika.
Achana na watu ambao wanakurudisha nyuma kimaendeleo: Kusema “hapana” kwa watu sahihi kunakupa muda na nguvu za kusema “ndiyo” katika mambo ya maana. Utumie muda wako kuwa na watu wema na makini na ambao mnafanana mawazo yenu.
Usijitenge: Jichanganye na watu wengine. Kutana na watu wapya, uliza maswali na jitambulishe.
Itaendelea wiki Ijayo.
No comments:
Post a Comment