Thursday, March 15, 2012

Dalili 5 za Mtu asiyejiamini I

KUJIAMINI ni hali ya kuwa na uhakika juu ya kile unachokifanya, tenda, nena na hata muonekano kwa ujumla.

Kujiamini kunasaidia sana katika kutafuta njia ya mafanikio maishani. Ni suala la muhimu sana kujiamini.

Mwandishi mmoja wa vitabu vya saikolojia, Ben Carson aliwahi kuandika;
‘Confidence can pull you to success’ (Kujiamini kunaweza kukusogeza palipo na mafanikio).
Kwa nini watu hawajiamini? Kutojiamini kunatokana na nini? Haya ni baadhin ya maswali ambayo ni lazima tujiulize.
Utamjuaje mtu asiyejiamini? Hapa chini nitaainisha dalili tano za mtu asiyejiamini kabisa. Lakini pia kabla sijaendelea mbele zaidi, naomba niweke kumbukumbu sawa kuwa, mtu asiyejiamini ni nadra sana kufanikiwa maishani.

KULALAMIKA

Dalili ya awali kabisa ya mtu asiyejiamini ni pamoja na kulalamika kila mara. Yaani jambo dogo tu lakini malalamiko yanakuwa mengi kupita jambo lenyewe.

Mwanasaikolojia mmoja nchini Marekani, Willie Jollie katika kitabu chake cha It Only Takes A minute to Change your Life, aliandika kuwa;
‘Too much complaining proves how weak and unconfident you are’ (Kulalamika kupita maelezo kunathibitisha ni kwa namna gani ulivyo dhaifu na hujiamini).

Mtu wa kulalamika, anakuwa hawezi kujisimamia juu ya jambo f’lani pasipo uwepo wa wengine na pia kulalamika sana kuonesha ni jinsi gani hujiamini katika kufanikisha mambo maishani.
Lakini pia, kulalamika kunaambatana na woga katika maisha kwani mara nyingi mtu muoga haishi kulalamika hasa anapoachiwa jambo f’lani alitende peke yake. Hivyo dalili ya awali kabisa ya mtu asiyejiamini ni pamoja na kuendekeza tabia ya kulalamika kila wakati.

Mtu anayejiamani hapendi kulalamika, badala yake hutenda mambo kwa vitendo na si malalamiko.
Lakini pia, tafiti za kisaikolojia zinaonesha kuwa, watu wanaopenda kulalamika ni wale wenye maneno mengi ambao kazi yao kubwa ni kuongea na si kutenda. Hili ni jambo baya sana maishani. Achana na maneno mengi, jiepushe na tabia za kalalamika ovyo, fanya kazi kwa vitendo huku ukitumia muda mwingi kuwa kimya.

KUTEGEMEA SANA WENGINE

Kuna baadhi ya watu hawawezi kufanya jambo lolote maishani pasipo kutegemea mawazo ya wengine. Hata kama jambo hilo liko ndani ya uwezo wake lakini hawezi kulitenda hadi atakapoambiwa na watu, sasa tenda.
Watu hawa huwa na uwezo mkubwa sana ndani yao lakini hushindwa kujisimamia wenyewe. Hata kama ana fedha kiasi gani, lakini hawezi kutenda jambo bila kusukumwa.

Mfano utakuta mtu anataka kuchukua hatua fulani nzuri sana lakini anashindwa hadi baadhi ya watu wamuamulie ndipo atende.
Mfano mtu amegombana na mkewe anakuwa hawezi kuamua nini cha kufanya juu ya suala hilo na hapo ndipo atakimbilia kwa rafiki zake kuwaomba wamsaidie nini cha kufanya jambo ambalo huashiria ni kiasi gani hajiamini.

Usiishi kwa mawazo ya wengine. Hata wewe una akili kama wao na pengine kuwashinda lakini unakuwa huna uhakika na unachokiwaza na kuona kama bila wao huwezi kujisimamia maishani. Hii ni hatari sana. Jitegemee, jiamini, tenda mambo kwa kutegemea muongozo wa upeo, busara, maarifa, akili na mawazo yako mwenyewe. Ni suala la utulivu tu.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment