Thursday, March 15, 2012

Elimu ya Darasani Si Kila Kitu

“MIMI ni masikini, sijasoma, maisha yanazidi kuwa magumu kila kukicha. Nawalaumu wazazi wangu kutonipeleka shule.” Hii ni kauli ya mama mmoja ambaye alikuja ofisini kwangu kuomba ushauri.

Japo alikuja analia, mwenye huzuni na simanzi kwa jinsi maisha yalivyokuwa yanamuendea, namshukuru Mungu aliondoka huku uso ukiwa na tabasamu.

Watu wengi bado wamegubikwa na fikra kuwa bila elimu ya darasani huwezi kufanya chochote maishani na ili uwe na maisha bora ni lazima uende shule.
Ndiyo maana utakuta wazazi wengi wanawaambia watoto wao kuwa nendeni mkasome ili muwe na maisha bora. Kauli hii huota mizizi akilini mwa watoto lakini wanapoanza kuukabili ulimwengu halisi, ndipo mambo hubadilika kabisa.
Nataka kuweka kumbukumbu sawa kuwa, kusoma si kitu na kutokusoma bado si kitu, bali ili ufanikiwe maishani inategemea na jinsi unavyotenda mambo.

Kuna msemo mmoja wa kizungu ambao napenda sana kuutumia unaosema ;
‘Life can compel you to move either foward or backward depending on what you do.’
(Maisha yanaweza kukupeleka mbele au nyuma kutegemea na jinsi unavyofanya). Hapa hakuna kusoma wala kutosoma.
Binafsi naamini sana katika elimu ya darasani, tena nahamasisha watu kwenda shule ili wapate mwanga wa maisha.
Ndugu zangu, mafanikio maishani ni uchaguzi wa mtu mwenyewe, kufanya kazi kwa nguvu na kutumia vyema kila fursa inayopatikana. Ukiangalia maghorofa yaliyopo Kariakoo na kwingine, utashangaa utakapooneshwa wanaoyamiliki. Wengi wao hawajasoma hata kidogo lakini wameweza kufikia kiwango hicho.

Nilishasema huko nyuma kuwa siri kubwa ya kufanikiwa maishani ni kujibidisha katika utendaji wa kazi huku ukiwa na nidhamu na matumizi ya fedha, watu muda na kuendelea kuwa na miradi mbalimbali.
Elimu ya mitaani ambayo mimi huiita Street University ni muhimu kuliko ile ya darasani. Hata kama umesoma hadi vyuo vyote duniani lakini ni lazima uje mtaani ujifunze maisha yanavyotakiwa kuendeshwa. Mara nyingi tunayofundishwa darasani ni tofauti kabisa na tunayokutana nayo katika maisha halisi.

Nataka kukuhakikishia kuwa hata kama hujasoma sana, mafanikio katika maisha ni uamuzi.
Kuna makundi matatu ya elimu ambayo yanajitegemea.
Kundi la kwanza ni Elimu ya Kitaaluma (Academic Education), Elimu ya Chambuzi (Proffesional Education) na Elimu ya Fedha (Financial Education).

Zote hizi ni muhimu sana lakini elimu ya fedha naipa kipaumbele cha kwanza kutokana na ukweli kuwa ni lazima ujue jinsi gani unatakiwa kuzitumia fedha zako hata kama ni ndogo au nyingi kiasi gani.
Elimu ya fedha inapatikana shuleni na mtaani lakini tofauti ni kuwa, shuleni utaipata elimu hii kwa nadharia lakini mtaani utaipata kwa vitendo. Ukienda kinyume na utaratibu huo, kufanikiwa katika maisha yako itakuwa ndoto.

Napenda kuhitimisha kwa kusema kuwa safari ya mafanikio maishani inahitaji uvumilivu na kujitoa kwa dhati na ni lazima uumie, uvuje jasho, uhangaike ndipo mambo yaweze kwenda sawa.

Tuache kupandikiza mbegu mbaya kwa watoto wetu kuwa waende shule ili waajiriwe ili wawe na maisha bora, badala yake tuwaambie ukweli kuwa unaweza kusoma na bado usiwe na maisha bora isipokuwa ili uwe na maisha bora ni lazima ufanye kazi kwa nguvu na kuzifanyia kazi kila fursa unazopata. Tuwaambie kuwa tunaenda shule ili kupanua uelewa na si kufanikiwa maishani.
Uwezo wa kufanikiwa uko mikononi mwako, ni wewe tu kuamua.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment