Thursday, March 15, 2012

Anza Mwaka na Mawazo Mapya III

Mateso na shida ulizopitia zisikurudishe nyuma, usikate tamaa kabisa. Mwandishi mmoja wa vitabu vya saikolojia, Willie Jolley aliwahi kuandika katika kitabu chake cha It Only Takes A minute to Change your Life kuwa; ‘Winners never quit and Quitters never win!’ (Washindi kamwe hawakati tamaa na wakata tamaa kamwe hawashindi!). Maneno yao ya kukuvunja moyo yageuze kuwa kuni za kuchochea moto wako wa mafanikio, ili siku moja uje uwathibitishie kuwa wewe ni mshindi.

Kaa mbali na marafiki wanaokatisha tamaa katika maisha. Fanya kazi kwa nguvu, kuwa mbunifu, usiwe mtu wa kulalamika hovyo, chunga matumizi ya muda na fedha, heshimu kila mtu aliyeko mbele yako, epuka kujikweza.
Kila siku endelea kujifunza vitu vipya.

Achana na starehe ambazo hazina maana kabisa, jutia umasikini ulionao kwa sasa, jiwekee mikakati muhimu ambayo itakuvusha. Kuanguka maishani ni jambo la kawaida sana hasa katika safari hii ya kutafuta mafanikio.

Ngoja nikupe mfano mmoja, Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln alishindwa mara nyingi mno kabla ya kuwa rais! Aliwahi kugombea ubunge akashindwa, aliwahi kuanzisha biashara mbalimbali lakini alishindwa. Lakini baadaye akashinda urais, hii ni baada ya kusota kwa muda mrefu sana.

Pamoja na kushinda urais huo, bado alikutana na changamoto ya kudharaulika lakini mwandishi mmoja aliandika makala kwenye gazeti ambayo ilisomeka; ‘This is the most powerful president in the United States of America’ (Huyu ndiye rais mwenye nguvu kuliko wote katika nchi ya Marekani) ni maneno hayo ndiyo yalibadili kabisa muonekano na fikra za rais huyo ambaye baada ya kuamini maandishi hayo akapewa tuzo ya kuwa rais bora. Na leo hii utawala wake unakumbukwa kuwa miongoni mwa tawala bora Marekani na duniani kwa ujumla.

Hivyo basi ni lazima kuwepo maadui wakati wa kusaka mafanikio ambao watakusaidia kuchochea nguvu yako ya kutafuta maendeleo.
Kuwa tayari kujitoa hata katika hatari ambazo ni mbaya zaidi. Mafanikio yanapatikana palipo na hatari (Success dwell on the edge).

Mbinu nyingine ya kupata mafanikio ni pamoja na kutumia muda mwingi ukiwa kimya ukitafakari mambo, kwani akili iliyotulia ndiyo hupata nafasi nzuri ya kubuni mambo ya muhimu. Kuwa mkimya muda mwingi, achana na maneno mengi kwani hayakusaidii kwa lolote zaidi ya kukuchosha kwani unatumia nguvu nyingi mno katika kuongea. Rafiki yangu mmoja aliniambia ‘Silence means a lot’ akimaanisha kuwa ukimya humaanisha mengi. Wewe kuwa kimya, fanya mambo kwa vitendo.

Jambo lingine la muhimu kuzingatia ni kuachana kabisa na tabia ya kufanya jambo kwa ajili ya kutafuta sifa. Achana na sifa ambazo hazikusaidii kwa lolote. Fanya mambo kulingana na jinsi moyo wako unavyokuelekeza kwa manufaa yako na si kwa ajili ya kusifiwa. Wengi wafanyao hivyo huwa hawafanikiwi kamwe. Dunia ya sasa si ya kutaka sifa na maneno mengi. Hii ni dunia ya vitendo na ustaarabu. Epuka kubishana na mtu yeyote kwa jambo lolote.

Achana na ugomvi wa aina yoyote, fanya kazi kwa nguvu na ubunifu wa hali ya juu. Jambo lingine muhimu ni kujifunza kusaidia watu. Pendelea sana kusaidia watu kwa namna yoyote ambayo unaweza, na ukimsaidia mtu hakikisha hakuna mtu anayejua.

Usitoe msaada kwa kujitangaza kwa watu. Kwa kufanya hivyo msaada wako hautakuwa na maana kwani hauna baraka za Mungu. Nikiwa naelekea mwisho wa makala haya, naomba nikukumbushe jambo muhimu sana kuwa maisha ni jinsi unavyoishi.

Mwamuzi wa hatima ya maisha yako ya kesho ni wewe mwenyewe na si mtu mwingine. Ukiamua kufanikiwa na ukajiwekea dhamana, basi ni lazima ufanikiwe. Pia kumbuka kuwa mafanikio ya kesho yanajengwa leo kwani mafanikio ya leo yalijengwa jana. Kila kitu kinawezekana hapa chini ya jua endapo tu utaamua kwa dhati. Naomba nikutakie mafanikio mema kwa mwaka huu wa 2012 ambapo naamini kama utayazingatia haya basi mafanikio kwako ni lazima. Mwisho

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment