UNAPO tafuta mafanikio ni lazima kwanza upitie shida na vikwazo vya kila namna.
Hakuna mafanikio ya bure, ni lazima uyatolee sadaka. Sadaka ya jasho. Ni lazima ufanye kazi kwa nguvu na maarifa ya hali ya juu.
Mateso ya maisha ni makali sana, tena wakati mwingine Mungu huzidisha ukali kwa lengo la kutaka kuona kama ukipewa hiyo neema utailinda.
 Siri nyingine ambayo nataka kuiweka wazi leo ni kuwa, vikwazo vipo katika safari ya kusaka mafanikio.
Ni  lazima ulie kwanza ili baadaye ufaidi mema ya nchi! Usivichukie vikwazo  vya maisha kwani vinakomaza, vigeuze kama kuni za kuchochea hamu yako  ya kufanikiwa.
Maisha ya dhiki unayoishi si yale ambayo yalimaanishwa kwako, badala yake maisha ya kweli yanakuja.
Lakini  yatakuja endapo utafanya kazi kwa nguvu, bidii na kumfanya Mungu ndiye  nguzo muhimu maishani mwako. Nilishawahi kusema huko nyuma kuwa, kuna  wakati maisha huonekana magumu sana.
ZINGATIA HAYA:
Sasa mateso yote yamefika kikomo,  naomba uyazingatie kwa makini nitakayo yaainisha hapa. Yatabadili maisha  yako. Mafanikio yako unayo mkononi mwako ni uamuzi tu. Ndani yako kuna  uwezo mkubwa mno ambao hakika hujaamua kuutumia ipasavyo.
Hujataka kuitumia vizuri zawadi amabayo Mungu alikupa. Zawadi ya akili.
Hukuumbwa kabisa uje uhangaike kama ulivyo sasa. Ukiamua kubadilika ni mara moja tu. Acha kulia, futa machozi.
Muda wa kufaidi matunda ya dunia umewadia kama utazingatia vizuri ninayoandika hapa.
Umeteseka kwa muda mrefu mno, miaka yote imekuwa michungu kwako, machozi yamekuwa faraja yako namba moja!.
Mwaka huu wa 2012 ni mwaka wa mapinduzi kwako. Ndiyo! Ni mwaka ambao hakika utakupa thamani ya utu wako. Amini hilo.
Kwanza  kabisa, tumia muda mwingi kuwa peke yako katika sehemu ambayo imetulia,  hakikisha hakuna kelele aina yoyote katika eneo hilo.
 Chukua kioo kisha kiweke mbele yako. Jiangalie kwa muda wa dakika zisizopungua kumi kisha sema maneno haya.
“  Mungu baba, ahsante kwa kuniumba hivi nilivyo, nakushukuru kwa kila  hatua uliyonipitisha maishani mwangu tangu nazaliwa hadi sasa.  Nakushukuru kwa kunipa zawadi hii ya pekee, zawadi ya akili ambayo  sijaitumia hata theluthi yake. Sasa nimeamua kuwa uliyenimaanisha.
 Kuanzia leo nayabadili maisha yangu kwani nimechoka kukaa hivi”.
Baada ya kusema hayo, sasa amini kuwa umekuwa huru.
Haijalishi  kwa una miaka mingapi, lakini chukulia kuwa mateso yote ya huko nyuma  ni kama historia ambayo kamwe haiwezi kujirudia na uisahau kabisa.
Anza  kubadili fikira zako kwa kuamini kuwa hukuumbwa kushindwa kabisa. Kaa  chini ufikirie ni kitu gani ambacho ukikifanya kinaweza kubadili maisha  yako kabisa.
Jichunguze kwa makini, hakikisha unapata wazo la  biashara. Katika maisha kuna vitu vitatu muhimu sana ambavyo ni wazo,  watu na fedha.
Kamwe vitu hivyo haviji kwa pamoja. Pata kwanza wazo ndipo mengine yafuate.
Naomba  nikukumbushe kuwa, ukianza safari yako ya kutafuta maisha, yatainuka  mabango mengi kutoka kwa watu ambao mimi huwaita Negativism (wavunja  moyo) ambao kazi yao kubwa ni kuvunja wenzao moyo. Watasema huwezi kwa  sababu tu hukusoma, kwenu masikini, baba yako hakuweza.
Nataka  nikuambie kuwa, hata kama watasema nini juu yako, maneno yao yasikuvunje  moyo hata kidogo kwani wao si waamuzi wa maisha yako. Mwalimu wa somo  la ujasiriamali, Eric Shigongo aliwahi kusema kuwa;  ‘Someone’s opinions  over you does not have to be your reality’(mawazo ya mtu juu yako  yasiwe ukweli wako).
Maadui huongezeka mara dufu unapotafuta mafanikio, kwani wengi huwa hatupendi kuona mtu anapiga hatua ya maendeleo maishani.
Kwa  hiyo basi acha  wakudharau lakini ukifumba macho na kuzidi kusonga  mbele, ipo siku wanaokudharau watakusalimia kwa heshima huku wengine  wakihitaji msaada wako.
Itaendelea wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment