Thursday, March 15, 2012

Anza Mwaka na Mawazo Mapya I

HAKIKA Mungu ni mwema kwa kila kitu anachonitendea maishani mwangu. Ni wengi walitamani sana kuuona mwaka huu mpya lakini kwa neema na fadhila zake wametangulia mbele ya haki. Jina lake lihimidiwe.


Baada ya kusema hayo, ngoja tuingie moja kwa moja kwenye mada yetu ya leo inayotufungulia mwaka ambayo naamini itabadilisha kabisa maisha yako. Na ndiyo sera ya kona hii ya Jitambue.


Safari ya maisha ni ndefu, ina kila aina ya adha, mabonde, miteremko, miinuko na milima mingi. Hakika ni safari inayohitaji ujasiri mkubwa kuikabili. Ni wale waliodhamiria kwa dhati tu ndiyo huikamilisha safari hii! Wengi wetu huishia njiani kwa kukata tamaa.


Kama ilivyo kwa safari yoyote ambayo ni ndefu, hivyo ndivyo ilivyo hata safari ya maisha nayo inachosha sana. Iwe kwa gari, ndege, meli n.k ni lazima uchoke.


Yawezekana kabisa unayesoma makala haya tayari safari ya maisha yenye mafanikio imeshakuchosha kutokana na urefu au ugumu wake. Umekata tamaa kabisa na kuacha mambo yaende kama yalivyo. Huna njia nyingine ambayo unaweza kuitumia yaani huna usafiri mwingine, umeanguka na unadhani huwezi kunyanyuka tena. Maisha yako yamejaa machozi, simanzi, maumivu, majuto, tabu, mihangaiko, hofu, mashaka, upweke, simanzi, huzuni, manung’uniko nk.


Umejaribu kufanya mambo mbalimbali kwa miaka mingi lakini hakuna chochote ulichoambulia zaidi ya kubaki palepale. Kuchekwa, kukatishwa tamaa, kuzomewa, kubezwa, kusimangwa, kuseng’enywa na kudharaulika imekuwa sehemu ya maisha yako kila kukicha.


Ndugu nyangu, hata kama giza nene la ufukara na umasikini limetanda maishani mwako, huoni mbele, nyuma, kulia, kushoto na kwingineko na umezama kwenye lindi la umasikini, leo nataka kuzungumza na nafsi yako, nataka kupandikiza mbegu tofauti kabisa akilini na moyoni mwako. MBEGU YA USHINDI! Mbegu ambayo italeta mwanga na matumaini mapya kabisa maishani. Kabla ya kuendelea na makala yangu yangu hebu ngoja nikukumbushe kitu kimoja muhimu kuwa WEWE NI MBARIKIWA, WEWE NI TAJIRI MKUBWA NA LAZIMA UFANIKIWE. Muda wa Baraka zako ulikuwa haujafika, wakati umewadia.

AMKA NA USIMAME
Msomaji, katika maisha haya ya mafanikio, kuna siri kubwa mno ambayo imejificha nyuma ya pazia, ni hazina ambayo wengi wetu tumefichwa, leo naweka wazi kila kitu.

MPAKA KIELEWEKE
Kila binadamu aliyezaliwa hapa chini ya jua, ameumbwa na Mungu kwa makusudi maalum, ana umuhimu mkubwa mno. Mungu hakukuumba kwa bahati mbaya maana hata hayo majani, miti na viumbe vingine vimeumbwa kwa sababu maalum sembuse wewe binadamu unayefanana naye kwa kila kitu. Tuliza akili nikupe dawa na njia bora za maisha.


Siri kubwa ambayo nataka kuiweka wazi hapa ni kuwa siku zote maishani hakuna kitu kizuri ambacho huja kwa urahisi. Hakuna mafanikio pasipo maumivu. Ni lazima utoke jasho. Watu wengi husahau kuwa siku zote kabla Mungu hajakupa matunda ya duniani ni lazima akuonjeshe joto la jiwe kwanza, ni lazima ujutie, ukifanikiwa kwa urahisi bila kuhangaika mara nyingi mafanikio hayo huwa hayadumu. Kwa ndugu zangu Wakristo ngoja niwakumbushe mifano miwili kutoka kwenye Biblia.


Baba yetu Ibrahimu ndiye anafahamika kwa jina la Baba wa Imani. Lakini jina hili hakulipata kirahisi, kuna kitu cha hatari sana alikifanya, alijitolea. Mungu alitaka kumjaribu kabla ya kumpa Baraka za kuwa na uzao imara. Alimwambia amtoe mwanaye (Isaka) kama sadaka ya kuteketeza.


Kwa wazazi mtakuwa mnaelewa namaanisha nini. Yaani mwanao wa damu halafu umtoe kwa kumchinja kwa mkono wako mwenyewe. Inatisha na yataka moyo. Lakini Ibrahim alikuwa tayari.


Alimchukuwa Isaka hadi porini lakini Mungu akamzuia kufanya hivyo ndipo akapewa jina la Baba wa Imani.
Aidha, katika nchi ya Usi kulikuwa na babu yetu Ayubu ambaye ukisoma mateso yake ni lazima utokwe na machozi, huyu aliteseka hadi akailaani siku aliyozaliwa.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment