SOTE tunahitaji nafasi za kujijenga upya au nafasi ya mara ya pili. Huu siyo ulimwengu uliotimia.
Watu wote hatujatimia. Binafsi nimeshaanguka mara nyingi mno maishani, wala sioni aibu kuweka wazi. Kwa sababu kuanguka ni sehemu ya maisha. Hii ina maanisha kuwa nimeshajaribu mara nyingi.
Ni mara chache sana kwa binadamu kutimiza mambo sawia kwa mara ya kwanza. Ni lazima ushindwe mara kadhaa. Hii ni kanuni ya maisha.
Tofauti kubwa iliyopo kati ya nafasi na kikwazo ni mtazamo. Vitu vingi vinafanyika au kushindikana kutokana na mtazamo wa mtu husika. Kupata nafasi ya pili maishani ni kujipatia fursa ya kukua dhidi makosa ya nyuma.
Ngoja nikumegee njia ambazo zitakurejeshea matumaini mapya maishani baada ya kuanguka na kushindwa mara kadhaa.
1. Sahau yaliyopita
Kilichofanyika, kimefanyika. Maisha yanapoonekana kuwa magumu, watu wengi sana huwa ndiyo tiketi ya kukata tamaa. Hushindwa kabisa kukubaliana na ukweli halisi na badala yake sasa hubaki wakiumia kwa makosa waliyoyafanya huko nyuma. Hiyo siyo njia sahihi ya kuishi.
Acha yaliyopita yapite. (Let the bygones be bygones).
Kila kipindi kigumu maishani mwetu huzaa fursa ya ukuaji na ubunifu kwa kila mtu. Lakini ili kujipatia ukuaji na ubunifu huo ni lazima kwanza tujifunze kuachana na yaliyopita. Ni lazima tufahamu kwamba vikwazo na ugumu wa maisha hupita kama kitu kingine maishani. Na vinapopita, vinabaki na somo kubwa.
2. Jifunze kitu
Kila kitu ni somo la maisha. Kila unayekutana naye, kila unachokumbana nacho.
Usiwe mwepesi wa kukata tamaa, hususan pale mambo yanapokuwa magumu. Kama hupati kazi uliyoitaka au uhusiano wako unalemaa, kitu muhimu pekee ni kuwa na uvumilivu.
3. Ondoa mtazamo hasi
Kuwaza katika mtazamo hasi huzaa matokeo hasi. Kuwaza katika mtazamo chanya huzaa matokeo chanya.
Kuwaza katika mtazamo chanya ni mwanga bora katika harakati za mafanikio makubwa. Akili ni lazima iamini kuwa inaweza kufanya kitu chochote ambacho kinawezekana kibinadamu.
4. Kabiliana na hali halisi
Ni lazima ukabiliane na majukumu yako mwenyewe na si mtu mwingine. Usikubali watu wakaamua juu ya majukumu yako kwani katika kufanya hivyo, utakuwa mtumwa wa mawazo ya wengine jambo ambalo si zuri maishani.
Ni wewe pekee utakaye dhibiti mpangilio na mwenendo wa maisha yako. Kila mtu anapitia kipindi kigumu maishani. Hilo liko wazi. Ni lazima ukabiliane na hali ngumu uliyonayo. Usikate tamaa.
5. Jikite katika mambo unayoweza kuyabadilisha
Baadhi ya nguvu zinakuwa nje ya uwezo wa kibinadamu. Jambo la msingi ni kufanya kila kinachowezekana kufanyika huku ukitumia uwezo wako wote.
6. Tambua unachokitaka
Huwezi kufanikisha kitu ambacho hukijui. Ni lazima utambue ni nini hasa unachokitaka.
Weka mikakati thabiti juu ya kile unachotaka kitokee na baada ya kukuweka sawa anza kukifanyia kazi kwa nguvu, akili na maarifa yako yote. Usifanye kitu kwa kuiga mkumbo au kwa kigezo fulani ambacho si sahihi.
7. Achana na mambo yote yasiyo ya muhimu.
Achana na mambo yasiyokuwa ya muhimu maishani. Hiki ni kipindi ambacho unatakiwa kushughulikia mambo ya msingi tu na si kingine. Tumia vizuri kila ulichonacho. Jiepushe na anasa ambazo hazikusaidii kwa lolote.
8. Dhamiria kwa dhati
Ukiweka sawa mipango yako yote, hakikisha unadhamiria kwa dhati kabisa. “Nataka kununua kompyuta moya mwezi ujao” hilo ni lengo na mpango ambao ukidhamiria unaweza kuutimiza.
Pia, Kuwa makini na matendo yako. Achana na mipango isiyokuwa na vitendo. Kila ukipanga mpango maalum. Basi anza moja kwa moja kuufanyia kazi.
9. Kuwa mtendaji zaidi kuliko muongeaji
Nilishawahi kusema huko nyuma kuwa dunia ya sasa haihitaji maneno na badala yake inahitaji vitendo tu.
Tenda zaidi ongea kidogo. Ukiwa mtu wa kufikiria tu bila kutenda, basi utaishia kufikiri tu jambo ambalo si jema katika mchakato mzima wa kutafuta mafanikio maishani.
Falsafa ileile ndiyo hutumika linapokuja suala la kuacha tabia mbaya. Kama una tabia mbaya ambayo unataka kuiacha lakini ukawa unaishia kuwaza tu bila kuchukua hatua madhubuti, basi mafanikio juu ya suala hilo ni hafifu.
10. Jiwekee ratiba maalu ya kila siku
Ni rahisi sana, lakini kujitengenezea ratiba ya kila siku kunaweza kubadili maisha yako.
Ratiba yakinifu, anza kuifanyia kazi na mwisho wa siku kila kitu kitakuwa makini na murua.
Kwa kufanya hivyo, kutasaidia kuianza siku yako kwa muamuko bora, na kuihitimisha siku kwa mpangilio maaulum na ikiwa unajiandaa kwa ajiki ya ratiba mpya ya kesho.
Lakini pia kutakusaidia kutazamia mambo ya muhimu.
11. Jidhibiti
Kadri unavyofanya kazi kwa nguvu, ndivyo unavyozidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kufanukiwa.
Achana na tabia ya kungoja mambo yajiseti menyewe.
Kama ukiendelea kufanya kile unachokifanya, utaendelea kupata unachokipata.
Kama unataka nafasi ya pili tena kwa dhati kabisa, yaani unataka kurudi kwenye kiwango kizuri cha maisha ulichokuwa nacho kabla, ni lazima uwe tayari kujitoa kwa dhati kwa kila kitu ulichonacho kwa ajili ya hilo. Maanisha kwa moyo wote.Hakuna kulemba!
Mwanzoni yaweza kuwa ngumu mno, lakini baada ya siku 21 za mwanzo kila kitu kitaanza kuwa safi. Huo ndio ukweli halisi.
Kumbuka, maisha siyo rahisi, hususan unapopanga kujipatia kitu kizuri. Kutimiza ndoto yako ni kazi kubwa na ngumu. Kuwa tayari kwa mabadiliko, dhamiria na uwe na uwezo wa kujidhibiti. Kila kitu kinawezekana.
12. Kamwe usiwafurahishe watu
Watu wengi sana hununua vitu wasivyovihitaji kwa fedha ambayo hawana kwa ajili ya kuwafurahisha watu ambao hawawajui!
Hapa namaanisha nini? Kuna baadhi ya watu hufanya mambo Fulani hata kama hawakupenda ili mradi tu waonekane bora kwa baadhi ya watu ndani ya jamii.
Usiwe miongoni mwa watu hawa. Ni upotevu wa muda.
Endelea kufanya unacho amini kuwa ni sahihi. Jirekebishe unapokosea, na mwisho wa yote ni lazima ufanikiwe tena. Utafika unapopataka endapo tu utadhamiria kwa dhati.
No comments:
Post a Comment