SIKU nyingi nimezungumzia juu ya umuhimu wa kuwa na nidhamu katika muda na kutambua vyema matumizi yake katika njia sahihi.
Bado imenibidi kukumbushia tena kwani naona bado kuna tatizo juu ya hilo, na kama kawaida ya kona hii ya Jitambue, kuweka tiba mahali ambapo pana maradhi ya kisaikolojia. Lengo ni kuona jamii inakaa katika mantiki inayohitajika.
Muda ni kiungo muhimu sana katika maisha ya binadamu hasa linapokuja suala la kujikwamua kiuchumi, kijamii na kidiplomasia. Hakika ukitambua vyema jinsi ya kuheshimu na kuwa na matumizi sahihi na muda wako, suala la mtu kufanikiwa maishani ni la lazima hata kama mtu mwenyewe hataki.
Watu wengi wamekuwa na upungufu wa nidhamu na muda wao na hivyo kushindwa kuwa na matumizi yakinifu na sahihi, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo maishani.
Mafanikio yote chini ya jua, msingi wake mkuu ni nidhamu ya muda na matumizi yake katika njia stahiki. Hebu jaribu kuangalia watu wengi waliofanikiwa maishani jinsi wanavyozingatia muda katika utendaji wa kazi zao.
Kwa nini nasisitiza kuheshimu muda na kuutumia vizuri? Ni kwa sababu muda ukishaondoka haurudi na hauna neno ‘excuse’ (samahani) kama wengi tufanyavyo. Watu wote tumepewa masaa sawa kwa siku ambayo ni 24.
Mfalme na mjakazi wake wote wamepewa masaa 24 kwa siku, hii ni pamoja na machinga na waziri mkuu. Mmiliki tajiri wa Kampuni la Microsoft, Bill Gates, mwandishi wa safu hii, na mpiga debe stendi ya mabasi, wote tumepewa muda sawa ambao ni masaa yaleyale 24!
Kwa nini Gates awe na mafanikio maishani mwake na mimi naendelea kusota mitaani? Jibu ni kwamba utofauti mkubwa uliopo baina yangu na Bill Gates ni nidhamu na matumizi ya muda.
Epuka sana kutumia ovyo muda wako kwani majuto ya muda uliopotea huwa ni makali kuliko kitu chochote. Jifunze kuheshimu muda, achana kabisa na hulka ya upotevu wa muda pasipo na sababu maalum.
Tumia muda wako kufanya mambo muhimu maishani ukiachana na mambo yote ambayo si ya lazima kwako.
Jinsi ya kuheshimu na kutunza muda
Ratiba sahihi: Kabla ya kulala usiku, hakikisha unaweka sawa ratiba yako ya siku inayofuata kwa maandishi. Yaani andika na uorodheshe kwa mpangilio maalum shughuli zote ukianza na ya kwanza hadi ya mwisho.
Irudie ratiba hiyo zaidi ya mara tatu kabla ya kupanda kitandani.
Lakini pia ni lazima uwe na ratiba maalum ya kuamka asubuhi. Kila uamkapo asubuhi jikumbushe tena ratiba ya kazi zako kwa siku hiyo huku ukinuia kuwa hutarudi nyumbani pasipo kukamilisha shughuli hizo.
Katika siku za mwanzo wa zoezi hilo, hata ukienda kazini kwako ni lazima uende na karatasi hiyo kwa ajili ya kujikumbusha mara kwa mara. Kwa kufanya hivyo utajikuta muda wako mwingi unautumia kwa kufanya shughuli zako muhimu.
Maneno mengi: Kwa nini unakuwa mzungumzaji kuliko mtendaji? Fanya kazi kwa matendo na si kwa maneno kwani dunia ya sasa haihitaji maneno bali vitendo na kujishughulisha na mambo yako muhimu.
Kama kila jioni ukitoka kazini kwako breki ya kwanza ni baa na kuanza kuagiza “moja moto, moja baridi” unadhani ni matumizi sahihi ya muda?
Kama unatumia muda mwingi kuongea na kupiga blaa blaa na porojo zisizo na maana unadhani ni matumizi sahihi ya muda?
Usipoteze muda wako kwa jambo ambalo halina faida yoyote katika maisha yako.
Jifunze kuheshimu muda kwani leo hii wewe ni kijana lakini miaka kadhaa ijayo utakuwa baba au mama mwenye majukumu katika familia. Kama uliutumia vibaya muda wako wakati wa ujana unategemea kuishi maisha ya aina gani?
Msingi bora na imara wa maisha ya kesho unajengwa leo na katika kujenga msingi imara wa maisha katika siku za ujana ni kuheshimu muda huku matumizi yake yakiwa na mpangilio maalum.
Hakuna mtu ambaye anaweza kununua muda hata kwa kiasi gani cha fedha kwani yakitimia masaa 24 tu, kwa siku basi biashara huishia hapo.
Kama nilivyoeleza awali kuwa matajiri wengi hutumia muda wao mwingi kuwa bize na shughuli zao za msingi huku sisi walalahoi tunatumia muda mwingi kupiga porojo na hadithi za akina Juma na Uledi.
Mfano mzuri ni Bill Gates ambaye napenda kumtumia katika mifano yangu kwani ni mmoja kati ya watu ninaovutiwa nao sana katika matumizi yao ya muda. Jamaa huyu pamoja na utajiri mkubwa alionao, bado huingia ofisini saa moja na nusu asubuhi na kutoka saa tatu hadi saa nne usiku!
Kwa nini anafanya hivyo? Kwa sababu anajua muda ukishaondoka hawezi kuurudisha, hivyo ni vyema kuutumia kwa wingi kwa ustahiki kadiri uwezavyo.
Kila siku ukiamka, ona kama hiyo ndiyo siku yako ya mwisho kuishi hapa duniani!
Halafu jitahidi kufanya mambo yote muhimu kwako kabla ya kuondoka katika uso wa dunia.
Kwa kufanya hivyo hutakuwa na muda wa kuchezea.
Tathmini matumizi ya muda wako kwa siku:
Baada ya siku kumalizika, ufikapo nyumbani kabla ya kulala anza kutafakari kwa jinsi gani umeutumia muda wako kwa siku hiyo.
Je, umetimiza sawasawa ratiba yako uliyojipangia kwa siku hiyo?
Na kama hujatimiza ni wapi ulikwama?
Ikiwa hujatimiza ratiba hiyo basi jutia hadi kiwango chako cha mwisho huku ukijiapiza kutorudia kupoteza muda wako.
Amka, amka, amka na kufanya kazi, fanya kazi kwa nguvu, zingatia matumizi sahihi ya muda wako.
Achana na maneno mengi, jiepushe na starehe, anasa na mambo yote ya aina hiyo ambayo hayana faida yoyote maishani mwako.
Kumbuka muda ni mali, na ulivyo leo kunatokana na jinsi ulivyofanya mambo yako jana na utakavyokuwa kesho, ni jinsi unavyofanya mambo yako leo!
Maisha ni jinsi unavyoishi.
Wewe ndiye mwamuzi wa hatma ya maisha yako na Mungu ni mwezeshaji tu.
Hakuna mafanikio ya bahati mbaya. Kuwa masikini kunatokana na kuwaza kimasikini na kuwa tajiri ni matokeo ya kuwaza kitajiri!
Tatizo linalotusumbua wengi wetu ni kushindwa kuheshimu na kutunza muda, utakuta mtu kaagizwa kufanya jambo flani na kupewa kabisa muda muafaka wa kumalizika kwa kazi hiyo lakini kwa kutokuwa na nidhamu ya muda utasikia akisema; ‘Aaa nitafanya baadaye bwana.., muda si bado upo!’ ndugu zangu, hayo siyo maisha.
Ukimuona mtu anaendesha Range Sport leo, ujue alitokwa jasho kwa kuzingatia umuhimu wa muda huku akitumia vizuri kila fursa iliyopatikana kwa wakati huohuo.
Mpenzi msomaji wangu, nikiwa naelekea mwishoni kabisa mwa makala haya, naomba niwakumbushe jambo moja muhimu.
Katika maisha ni lazima upitie nyakati ngumu ndipo uweze kusimama imara.
Kuna kipindi maisha yataonekana kuwa magumu mno lakini si tiketi ya kukata tamaa kabisa.
Endelea kupigana kwa kadiri uwezavyo.
Kwa Wakristo wenzangu naomba niwakumbushe kwamba kwenye Biblia, katika methali za Mfalme Suleiman iameandikwa;
‘Mungu hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa’ sasa katika hali kama hiyo, basi msomaji wewe chakarika kwa kufanya kazi kwa nguvu huku Mungu akiwa nguzo muhimu maishani mwako. Hakuna kinachoshindikana chini ya jua kama tu utadhamiria kwa asilima miamoja.
Ni lazima uwe na mahali unapotaka kufika maishani, katika maisha usiishi ilimradi unaishi lakini jaribu kujiwekea malengo muhimu huku malengo hayo yakiwa na mwisho wa kutimia na baada ya kujiwekea mikakati hiyo basi anza kuchukua hatua kwa kufanya kwa vitendo.
Nilisha sema huko nyuma kuwa achana kabisa na maneno na badala yake tumia muda mwingi kwa kutenda.
Muda ni mali, utumie vizuri. Mafanikio ni lazima.
Thursday, March 15, 2012
Muda na Matumizi Yake
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment