Thursday, March 15, 2012

Je,kazi unayofanya itakuendeleza kimaisha?

IMEANDIKWA katika Biblia kuwa, “asiyetaka kufanya kazi asile.” Bila shaka sote tunafahamu kuwa, msingi wa heshima kwa kila mwanadamu ni kazi.

Kwenye mada ya leo hoja si kufanya kazi, bali ni je kazi tunazozifanya zitatuendeleza kimaisha?
Ukipita mitaani kuwauliza watu kama kazi wanazofanya wanategemea zitawafikisha kwenye malengo yao kimaisha, wengi wao watajibu kuwa hawajui, huku wengine wakitilia shaka zaidi kipato kidogo.

Tunapoendelea kujifunza ni vema tukajiuliza, hivi kazi za maendeleo ni zipi, je ni zenye kipato kikubwa pekee?
Inawezekana tukakubaliana na hoja ya kipato, lakini ni wangapi wanaoingiza mamilioni kwa mwezi ambao wanaoonesha kupiga hatua za kimaendeleo? Je wauza mboga na walima nyanya hatujasikia wakisimulia walivyotajirika kwa kazi hizo?

Binafsi naamini, kazi yoyote yenye sifa za kumuendeleza mtu kimaisha lazima iwe na vigezo vitano, ambavyo leo nataka kuvizungumzia kwa lengo la kujielimisha mwenyewe pamoja na wewe msomaji wangu.

KAZI HALALI

Sifa ya kwanza ya kazi ya maendeleo ni uhalali wake. Huwezi kufanyakazi haramu za ujambazi, uuzaji dawa za kulevya, wizi na ukahaba halafu ukatarajia mafanikio makubwa.

Katika ulimwengu huu, matajiri kumi wanaoongoza duniani wanafanya kazi halali. Mfano, Carlos Slim (mafuta na simu), Lakshmi Mittal (kuyeyusha vyuma) na Amaneio Ortega (kampuni ya mavazi), zote hizi ni kazi halali.

Kwenye kipengele hiki tunaweza kujaribu kupindisha ukweli kwa mtazamo kwamba, biashara na kazi haramu ndizo zenye faida kubwa lakini uhakika utabaki kuwa maendeleo bora yenye heshima ya kudumu yanatokana na kazi halali.

KUPENDA KAZI

Ili ujue kwamba kazi yako itakusaidia kimaendeleo, huna budi kujiuliza, unapokuwa kazini unafurahia kufanya kazi yako au unafanya tu kwa sababu huna jinsi nyingine ya kujipatia kipato. Ukiwa unafanya kazi usiyoipenda, fahamu huwezi kuendelea kwa sababu hutakuwa mbunifu, huwezi kujituma kufanya usichokipenda. Hitimisho ni kuwa wapendao kazi zao bila kujali ni ndogo kiasi gani ndiyo watakaofanikiwa.

KAZI YA FAIDA

Kazi isiyokuwa na faida haiwezi kuwa ya kimaendeleo. Katika eneo hili haijalishi ukubwa wa faida bali ni ile zana yenyewe ya kupata zaidi ya kile anachotumia kama mtaji wa kazi.

Ikiwa kazi yako inakupa hasara, usitegemee itakuendeleza, hata kama ukiwa na viwanda, miradi mikubwa kiasi gani tambua tu kwamba kuna siku utafilisika.

KAZI RAFIKI WA JAMII

Wapo watu ambao wanafanya kazi ambazo ni adui wa jamii inayowazunguka. Ukiwa na kazi ya namna hiyo huwezi kufanikiwa kwa sababu watu na mazingira yataihujumu.

Mfano, ukiwa eneo la watu ambao pombe kwao ni haramu usijenge viwanda vya bia na kudhani unafanya kazi ya kimaendeleo, utakuwa unafanya kosa kubwa sana. Kazi rafiki wa jamii ndiyo yenye maendeleo.

KAZI YA MUDA

Mara nyingi kazi za muda huwa si za kutegemea sana na huhitaji umakini zaidi katika kuzitumia katika maendeleo.
Hivyo ukiwa kwenye ajira au kazi ya muda, jaribu kufikiria unawezaje kugeuza kipato unachopata hapo na kukipeleka kwenye mradi wa kudumu ambao utakuwezesha kuendelea kimaisha.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment