Hakuna kitu kibaya maishani kama kuonekana upo katika daraja la chini kuliko kawaida kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia kuna madhara makubwa.
Kitaalamu hakuna jambo ambalo hutokea maishani bila sababu maalumu hivyo hata kudharauliwa kwako ndani ya jamii unayoishi kunatokana na jinsi unavyotenda mambo yako.
Ninaposema hivyo ninamaanisha kuwa matendo yako, muonekano wako, kuzungumza kwako kunaweza kukufanya ukaonekana kituko na kushushwa daraja katika jamii.
Mwalimu wangu wa somo la maisha na saikolojia, Bw. Eric Shigongo aliwahi kuniambia ‘Nothing happens in the sky, but the elements should be there’ akimaanisha kuwa hakuna kitokeacho angani pasipo kuwa na dalili au sababu zake.
Naomba nianze kutoa njia za kukusaidia kurejesha heshima yako kwa kuperuzi na wewe baadhi ya dokezo muhimu zinazoweza kukusaidia kujenga heshima yako.
MUONEKANO
Kwanza kabisa ni jinsi unavyoonekana. Muonekano ninaouzungumzia hapa ni usafi wa mavazi na mwili kwa ujumla. Hata siku moja hakuna mchafu anayeheshimika katika jamii anayoishi hata kama ana kipaji kikubwa kiasi gani.
Kwa hiyo uchafu wa mavazi na mwili huchangia mtu kudharauliwa katika jamii anayoishi. Linaweza kuwa jambo dogo sana lakini ni moja kati ya sababu kubwa inayochangia kuporomoka kwa thamani yako kwa watu.
Maana itafikia sehemu watu wanakwepa kuongozana na wewe kwa hofu ya kuaibika mtaani. “Tusiongozane naye atatutia aibu bure, mchafu sana bwana.”
Mazungumzo
Hapa naomba nieleweke kuwa unachokizungumza kinaweza kukujengea heshima au kukubomolea. Kauli zisizo na busara zitakufanya udharaulike kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na mantiki huchangia kuporomosha heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi.
UTENDAJI KAZI WAKO
Ndugu zangu, siku zote heshima ya mtu ni kazi. Watu wengi hawapendi kufanya kazi kwa bidii huku wengine wakijiendekeza kwa tabia ya kuombaomba, jambo hilo halifai kwa vile huchagia kubomoa heshima yako mbele ya jamii.
KUTOTIMIZA AHADI
Kama una tabia za kuahidi mambo halafu unashindwa kuyatekeleza, basi unajiweka katika nafsi mbaya ya kutunza heshima yako katika jamii unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi kuliko kuahidi na kutotimiza.
SIFA ZISIZO NA MAANA
Nakumbuka msemo mmoja kutoka kwa Mwandishi mwandamizi aliyekuwa mtaalamu wa falsafa za maisha, Marehemu Adolf Balingilaki ambao unasema:
‘Ukitafuta heshima kwa gharama ya juu, basi utalipwa dharau kwa bei nafuu’
Msemo huu unamaanisha nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo yako kwa ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya kujifagilia na kujiinua basi watu huishia kukudharau na kukuona mshamba wa maisha.
Kwani hata katika maandiko matakatifu yanasema ajikwezaye hushushwa. Hivyo kujigamba na kujikweza kwako huchangia kwa kiwango kikubwa sana kuporomosha na kuondoa kabisa heshima yako hivyo kubaki mtu wa kudharauliwa tu.
KUTOKUWA MWAMINIFU
Suala la uaminifu ni pana, kuna uaminifu wa fedha, siri, dhamana na mambo kama hayo, hivyo ni vema kila unachoaminiwa lazima ukitunze ukiwa mtu wa kuvunja uaminifu fahamu kuwa utashusha heshima yako.
Thursday, March 15, 2012
Jinsi ya kurejesha heshima yako katika jamii
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment