Naendelea kuchambua mada yetu tuliyoianza wiki iliyopita na sasa nahitimisha na dalili nyingine zilizosalia. Twende pamoja...
KUSITA KATIKA MAAMUZI
Kipengele hiki hakiko mbali sana na kilichotangulia lakini kuna baadhi ya vitu katika kuelekezana. Kwamba unakuta mtu ana vitu vingi sana kichwani mwake lakini hawezi kuchukua hatua kuvikamilisha na kuviweka katika hali ya utendaji.
Hapa nazungumzia suala la kusita katika kuchukua hatua juu ya unachokiwaza na kukifikiria maishani. Mfano labda mtu yuko kijijini, ana kipaji cha kuandika habari au ana ndoto za kuwa mfanyabiashara, ameamua kwenda mjini kutafuta hizo njia za kumuwezesha kutimiza ndoto yake. Tatizo linakuja katika kuchukua hatua za utekelezaji juu ya jambo hilo. Anakuwa hajiamini kama anaweza kukaa mbali na nyumbani kwao. Anakuwa mtu wa kusita katika kufanya maamuzi sahihi.
Wakati mwingine una rafiki ambaye hakika hana faida yoyote kwako, yeye ni mtu wa kukunyonya tu lakini hana mchango wowote kwako. Sasa unashindwa kufanya maamuzi sahihi ya kuachana naye kwa kuhofia kuwa bila yeye utapwaya. Eti umemzoea sana. Huku ni kusita katika maamuzi ambapo nasema ni dalili ya kutojiamini. Usisite, chukua uamuzi muafaka tena kwa wakati. Jiamini katika kuamua mambo.
KUJIKOSOA
Hii ni dalili kubwa sana ya kutojiamini maishani. Unakuwa ni mtu wa kujifananisha na wengine kisha kujishusha katika thamani. Hapa nazungumzia watu walio na mawazo mazuri sana lakini kabla hujayawasilisha kwa watu, unaanza kujikosoa. Hivi kweli hili ni jambo jema kulisema? Au nitaelewekaje? Watakubali kweli mawazo yangu? Yaani ni mtu wa kujikosoa kila wakati, kuona kama huna kitu cha kusema au kuwasilisha kwa wengine.
Achana na tabia ya kujilinganisha na wengine. Iwe kwa mavazi, fedha, uzuri wa sura nk. Jione kuwa wewe ni bora kuliko wengine kama yeye ni mzuri wa sura, basi ni yeye. Kama ana nguo nyingi kuliko wewe sawa. Lakini jambo la msingi hapa ni kujiamini na kuondoa zana ya kujikosoa. Mchango wako ni mkubwa sana katika jamii . Ni suala la wewe kujiamini. Jiamini kuanzia leo.
WIVU
Hapa nazungumzia wivu ambao hauna maana hata kidogo. Utakuta mtu anampinga mtu pasipokuwa na sababu maalum. Unakuwa mtu wa kuwapinga wengine kila wakitaka kufanya jambo muhimu la kimaendeleo kwa kuhofia tu kuwa watakuzidi kwa sababu hujiamini katika utendaji wako wa mambo.
Unakuwa unawaza, f’lani akifanya hivi atanizidi katika suala hili, au akifanya hiki mimi nitaonekana sifai mbele za watu na jamii kwa ujumla. Ni mtu wa kuwaza uwezo wa watu pasipo kujifikiria mwenyewe. Achana na wivu wa kutojiamini. Jiamini sasa. Kwa kufanya hivyo kila kitu kitanyooka na maisha utayaona yapo tofauti.
MUHIMU
Maisha yanaendelea kama kawaida, jitahidi kuondoa zana zote potofu katika maisha, ondoa fikra za kushindwa hata kidogo kani wewe hukuumbwa kuja kuteseka hapa chini ya jua.
Thursday, March 15, 2012
Dalili 5 za Mtu asiyejiamini II
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment