MPENZI msomaji wa safu hii, awali ya yote sinabudi kumshukuru Mwenyezi  Mungu ambaye amekuwa akinipigania katika maisha yangu na kuniongozea  dakika za kuvuta pumzi yake kila uchwao.
Hakika hiyo ni zawadi pekee  kwangu licha ya kwamba sijawa mkamilifu machoni pake, hivyo namuomba  azidi kunitia nguvu ili siku moja nimgeukie na kuyatenda yale  yanayompendeza.
Baada ya kusema hayo machache, ngoja nirejee kwenye makala niliyokuandalia yenye kichwa husika hapo juu.
Ni  watu wachache ambao wanaweza kujisifu kwa uhodari wa kutafuta. Naamini  ni nadra kumkuta mtu akifurahia kubeba mzigo mzito, kulima, kufanya  kazi, kujituma katika shughuli hii na ile kwa sababu kutafuta  tunakuchukulia kama kero.
Ni rahisi kutamani kufanya kazi kidogo  lakini si kupewa fedha au mgawo wa mafanikio kwa kiwango kidogo. Tamaa  ya wanadamu wengi ni kupata na si kutafuta.
Kwa msingi huo, sioni  haja ya kusubiri jibu la kipi bora kati ya kupata na kutafuta kwa  sababu najua; vijana wengi wanatamani sana kupata kazi nzuri kuwa na  fedha nyingi za kufanyia anasa, mavazi ya gharama na  nyumba za kisasa,  hivyo chaguo lao ni kupata.
Kitaalam, miongoni mwa makosa makubwa  yanayofanywa na watu ni kupenda kupata na kuchukia kutafuta. Msomaji  wangu, utajiri si wingi wa fedha au mafanikio bali kufanya kazi na  shughuli nyingi zaidi ya mafanikio uliyopata.
Siku zote  wanaofanikiwa duniani ni wale wanaopenda kutafuta, hawachoki kuwekeza,  hawaachi kujitumikisha, hawatafsiri faida kama pato la kutumia kwa anasa  bali nyenzo ya kuwawezesha kutafuta zaidi.
Mchanganuo wa mambo haya  mawili uko hivi: KUPATA; mfumo wake ni matumizi. Mtu aliyepata mshahara  akafurahi, akaridhika, hana njia nyingine zaidi ya kuutumia mshahara huo  kununulia nguo, kulipia umeme, pango la chumba na karo za shule.
Ukweli  ni kwamba, hata kama fedha na mafanikio aliyopata mtu yatakuwa makubwa  kiasi gani kwa mfumo huu wa kutoa, matokeo tarajiwa ya siku za usoni ni  kumalizika kwa pato na hivyo kumpeleka mtu kwenye hatua nyingine ya  kutafuta.
KUTAFUTA; Ni mrija uvutao mafanikio. Anayetafuta hupata  zaidi na zaidi na uzuri wake ni kwamba, mfumo huu umeunganishwa moja kwa  moja na KUPATA. Kwa msingi huo anayetafuta anakuwa sawa na mtu  anayeishi ndani ya mifumo miwili kwa mpigo na kwake mtu huyo hakuna  kufilisika.
Nashauri, watu wote tufurahi zaidi wakati wa  kutafuta, tujivunie uwezo wa kutenda, tupende kazi zinazotuingizia  mishahara na kamwe tusipende mishahara inayotupeleka kwenye matumizi  yatakayoturudisha kwenye mfumo wa kutafuta tusioupenda.
Muhimu  kuunganisha nguvu katika harakati za kutafuta maisha na kuachana na  mfumo wa kushirikiana zaidi kwenye matumizi ya vile tunavyopata kwa  sababu mwisho wake ni mbaya.
Nimalizie makala haya kwa kuwashukuru wasomaji wangu wote kwa kuniunga mkono.
Siku  zote nafurahi kusikia jinsi ambavyo makala zangu zimekuwa zikibadilisha  maisha ya watu. Naomba tuzidi kukutana kwenye ukurasa huu na kwenye  mtandao wa kijamii wa facebaook.
Thursday, March 15, 2012
Kipi bora kati ya kupata na kutafuta?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment