Kwenye mapenzi kuna nyakati za kutofautiana, kukasirishana. Katika  hali ya kawada kipindi hiki huwa ni za hatari kwa sababu husababisha  nyufa kubwa za uhusiano na kulifanya penzi kukosa ladha.
Sote  tunajua, watu hupigana, huachana, hujeruhiana, hutukanana,  hudhalilishana wakiwa na hasira. Hata hivyo si wote wanaojua wafanye  nini wanapojikuta wameingia kwenye hatua hiyo mbaya. 
Msomaji wangu,  hebu jaribu kukumbuka ugomvi mmoja uliotokea kati yako na mpenzi wako na  ikiwezekana jikumbushe mlivyoanza! Utabaini kuwa mlianza kama utani na  mkajikuta mmefura kwa hasira, mkatwangana makonde, mkatamkiana maneno  makali ya kuudhi na pengine mkaamua kuachana.
Yote hii ni kwa sababu  mlikosa elimu ya mazungumzo. Ingekuwa mmoja wenu hasa yule aliyekuwa wa  pili kukasirika anafahamu hatua za kuzungumza na mtu aliyekasirika  angechukua jukumu la kutuliza machafuko na kuleta amani kwenye mapenzi.   Tazama  hatua tano za kuzungumza na mpenzi aliyekasirika.
MPUNGUZE MHEMKO
Hasira  hujaza kifua, huathiri mzunguko wa damu na ufahamu. Mtu aliyekasirika   huwa vigumu kwake  kusikiliza au kutazama mambo kwa jicho la tatu.  Mwenye hasira huwa hafikirii matokea yajayo badala yake hutazama zaidi  tukio na jinsi ya kupata ushindi iwe kwa maneno au kwa mapambano.
Katika  hali ya namna hiyo, mtu mwingine akija na busara za kutaka kumgeuza  haraka haraka hawezi kumuelewa. Muhimu hapo ni kuacha kumwadama,  kujibizana naye, kumshawishi asikilize badala yake mpe nafasi ya kusema  atakavyo, abwate ajuavyo huku wewe ukimuitikia na kumkubalia lawama  zake. “Basi mpenzi mwenye makosa ni mimi.” Kauli za aina hii  zitampunguza hasira kwani atajiona msindi.
MSOME SAIKOLOJIA YAKE
Kwa  kuwa unamfahamu mpenzi wako kwa kina itakuwa rahisi kwako kumtambua  kuwa amepunguza hasira na kurudi katika hali yake ya kawaida. Ukisha  fahamu hilo chukua jukumu la kumsoma kisaikojia ili kujua kama yuko  kwenye hali nzuri ya kusikiliza yale uliyotaka kumwambia wakati  alipokuwa na hasira.
Zoezi hili linaweza kuchukua saa kadhaa na  wakati mwingine hata siku mbili. Lengo ni nini? Ni kupata matokeo sahihi  ya kuondoa chuki za mwenza wako na kumfundisha madhara ya kukasirika  kwenye uhusiano wenu wa kimapenzi. “J, nakupenda sana, lakini juzi  uliniumiza, uliniambia mimi malaya kwa kosa ambalo sikufanya?” Bila  shaka muda huo atakusikiliza zaidi kuliko ungebishana naye  alipokuwa na  hasira.
MRUHUSU AKUJIBU
Pamoja na kumsoma kisaikojia na kumwambia  kinagaubaga makosa yake, usimzuie kujitetea, mpe nafasi ya kuzungumzia  kilichomkasirisha. “Unaona bado unanitukana, sasa naamini siku ile  ulikuwa umedhamilia.” Usisiseme hivyo, mwache ajibu hoja hata kama  atakuwa anakukandamiza na kuzidi kujijengea ushindi. Mvumilie aoshe  ubongo wake.
EPUKA MARUMBANO
Kama nilivyosema kwenye hapo juu,  wapenzi wengine huwa wagumu kuelewa, ni watu wa kuficha udhaifu wao na  kutopenda kuonekana wamekosea. Watu wa namna hii unapowarejeshea  mazungumzo  wanaweza kujikuta wanahamaki tena.
“Kwa hiyo ulikuwa  unasemaje…nilifanya ndiyo,… wewe unaamuaje?” Mkifika kwenye alama hiyo  usikubali kurumabana naye mwache aseme halafu wewe ingia kwenye hatua ya  tano.
MUOMBE MSAMAHA
Hata kama atakuwa yeye ndiye mwenye makosa  na amekataa kukiri, usijali, chukua jukumu la kumuomba msamaha na  kueleza tena nia yako ya kumazungumzo ilikuwa ni kuelewana si kugombana.  Kumbuka hata kama amekiri kosa, bado unatakiwa kumuomba radhi kwa  kurejea yaliyopita. “Mpenzi inawezekana nikawa nimekuudhi kwa  niliyosema, nakuomba sana tusameheane.”
Thursday, March 15, 2012
Hatua 5 za kuzungumza na mpenzi wako aliyekasirika
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment