Katika hali ya kawaida kila mwanadamu anahitaji kufarijiwa juu ya  matatizo anayokumbana nayo kwa namna mbalimbali maishani. Mkwamo na  vifungo vya hali ngumu ni suala linalohitaji msaada wa faraja kama tiba  mbadala.
Hata hivyo uchunguzi unaonyesha kuwa karne tuliyo nayo  kwa sasa, hali ya watu kujali na kujitolea kwa ajili ya wengine  inaonekana kunyauka siku hadi siku. Mume, mke, ndugu, matajiri na watu  wenye uwezo wanaonekana kushindwa kutoa faraja kwenye matatizo ya watu.
Maisha  ya sasa kila mtu anaishi sawa na msemo wa ‘abiria achunge mzigo wake.’  Aidha, kasumba ya kutegemea msaada wa kufarijiwa inatajwa kuwa mzigo  unaoelemea wanadamu nyakati hizi hasa pale unapokuwepo ukweli kwamba  wafariji hawapo au wamepungua kabisa ulimwenguni.
Jitihada za  wanasaikolojia ulimwenguni zimekuwa zikijaribu kutafuta jibu na  la  tatizo hili la nini kifanyike ili watu waweze kufarijika bila  kuwategemea watu wengine? Msingi wa utafiti huo ni kupata suluhisho  linalokwenda na wakati kwa watu kuvunjika moyo na kuangamia kwa ukosefu  wa watu wa kuwafariji.
Kama wanadamu tunashida zinazotusonga,  tumedhurumiwa, tumefiwa na tuliowategemea na kuwapenda, tuliowaamini  wametusaliti, tunaumwa magonjwa sugu, ni masikini wa kutupwa, tuna  hitaji la faraja, lakini ndugu zetu tunaowategemea wamegeuza na  kushupaza shingo, yaani  hawataki kutusaidia hata kidogo. Sasa je,  tufanye nini?
Njia pekee inayoweza kutusaidia kukabiliana na  maisha magumu ambayo hayana watu wa kutupenda, kutusaidia, kutuhurumia  na kutujali, ni sisi wenyewe kuchukua jukumu la  kuzifariji nafsi zetu  na njia za kufuata ni hizi:
TUSIKOSOE UTU WETU
Tatizo kubwa  linalowakabili watu wengi ni kuukosoa utu wao. Ndiyo maana wanakimbilia  kuamini kwa wengine kwamba wasipoweza wao ndugu na jamaa zao  watawasaidia.
Udhaifu huu wa kujikosoa ndiyo unazaa tunda la  kuhitaji faraja kutoka kwa watu. Lakini jambo linalosikitisha zaidi  ambalo liliwahi kumchekesha Tara Parker-Papa Mwandishi wa Blogu ya afya  aliyochangia kwenye Tovuti ya New York Times ni pale mtu anaposubiri  sauti toka kwa mwingine imwambie POLE!.
Ni wazi kwamba hatuwezi  kusubiri sauti za pole kwa sababu nasi tunazo, tunachotakiwa kufanya ni  kuziambia nafsi zetu. Zaidi ya hilo, kukiwepo na hitaji lolote la pesa  au nguvu toka kwa mtu  kutuwezesha  kufarijika, si faida kwetu kusubiri  zije wakati wenye nazo hawataki kutupatia.
Sisi wenyewe kama  binadamu tunaweza kusimama peke yetu na kujipenda kwa jinsi tulivyo bila  kuainisha na kujali upungufu wo wote tulio nao kwa vile matatizo ya  mwanadamu hayajapata kumalizwa na uwezo wa mtu uwe wa kuazima au wa  kwake mwenyewe. Lazima tujiwekee mazingira ya kujithamini sisi wenyewe.
Yamkini  nitakuwa sawa nikisema, matajiri tunaosubiri watufariji kwa misaada yao  nao wana shida zinazowatoa jasho. Hao ndugu, rafiki na jamaa zetu  tunaodhani wamekamilika kimaisha wana yao yanayowaondolea faraja. Huo ni  ukweli usiopingika.
TUTAMBUE KINACHOFARIJI
Kwa bahati mbaya  watu wengi hawatambui kitu kichofariji ndiyo maana wanakimbilia  kutegemea msaada. Lakini ukweli ni kwamba mawazo yetu ndiyo faraja pekee  ya maisha.
Tukijikubali, kujipenda na kujiwazia mema  hatutafadhaishwa na hali ya wenzetu kutojali shida zetu, badala yake  tutafurahia matatizo yetu kwa taraji la yote yanapita. Leo naomba  niishie hapa wiki ijayo tutachambua kwa kina tofauti ya maneno BINAFSI  na UBINAFSI ambayo ndiyo yanachangia kwa kiasi kikubwa sana watu  kutegemea faraja kutoka kwa  watu wengine.
Matatizo yako na jinsi ya kujifariji mwenyewe-2
Zaidi  ya saa 126 tangu niandike makala haya kwa mara ya kwanza wiki  iliyopita, nimejiridhisha kuwa imekuwa ni vigumu kwa watu wengi  kutofautisha  UBINAFSI na BINAFSI.
Kutokujua tofauti kubwa  iliyopo kati ya maneno hayo, kunaweza kuwa msingi wa matatizo ya  kimaisha kwa  mwanadamu na ukosefu wa faraja.
Kama lilivyo jina  la kolamu yangu  JITAMBUE, watu wengi hawajitambui na kujithamini,   ndiyo maana wanadhani wamezaliwa ili wateseke hapa duniani.
Ni ukweli  usiopingika, kila mmoja wetu angejua kusimama vema kwenye mhimili wa  maisha yake tungepunguza kwa kiasi kikubwa mifadhaiko ya mioyo yetu na  msongo wa mawazo usiokuwa na sababu.
Ifahamike kwamba mwanadamu  wa kwanza aliumbwa BINAFSI (Mwanzo 2:7, “....mtu akawa nafsi hai”).  Tafsiri ya neno hili inayopatikana kwenye kamusi ya kiswahili sanifu ya  TUKI Toleo la Pili; “kwa nafsi yangu, kwa ajili yangu mwenyewe tu.”  Mwisho wa nukuu.
Po pote pale duniani, mwanadamu binafsi ndiye  mwenye kuishi kwa furaha, ndiye mwenye mafanikio, anayeweza kujifariji  mwenyewe kwa umasikini wake, hali yake duni, ugonjwa wake sugu, taabu na  shida zake, kwa sababu yeye ni mwenyewe tu.
Katika hali ya  kawaida, nyuma ya binafsi kuna ubinafsi ambao unaelezwa kwenye kamusi  kuwa ni “hali ya ya mtu kujifikiria na kujipenda yeye mwenyewe.” Mwisho  wa nukuu ambayo kwa mtazamo inaelea hewani na kuwafanya wengi wadhani  kuwa maana ya maneno haya ni moja.
Ingawa si mhubiri, nikiri kuwa  ni mchunguzaji wa  maandiko matakatifu ambayo yananirudisha kwenye  kitabu cha Mwanzo 3:4-5, ambapo nabaini mwanzo wa ubinafsi ulivyoanza  kwa mwanadamu wa kwanza.
Nukuu ya maandiko hayo inasomeka hivi:  “Nyoka akamwambia mwanamke, hakika hamta kufa, kwa maana Mungu anajua ya  kwamba, siku mtakapokula matunda ya mti huo,  mtafumbuliwa macho, nanyi  mtakuwa kama Mungu kwa kujuwa mema na mabaya.”
Hapa wanadamu hawa wa kwanza wanatamani kuishi kwa ubinafsi, wanataka kufanana na Mungu wao.
Ubinafsi  halisi  ninaouzungumzia ndiyo huu, ambao unamfanya mwanamke ambaye  hajazaa atamani kuzaa kama fulani, amiliki gari, awe na maisha ya juu,  mawazo ambayo humsogeza kwenye hali ya kujidharau na hatimaye  kufadhaika.
Hii ndiyo sumu ya ubinafsi ambayo inaua, inadhoofisha  na kuondoa hali ya uthubutu wa kukabiliana na matatizo yetu kama  wanadamu na kutufanya tulilie kusaidiwa na kufarijiwa na wenzetu.
Msomaji  wangu, kuanzia leo fahamu kwamba ukifadhaishwa na cho chote ujue  unaumizwa na ubinafsi wako unaokusukuma kutaka uwezo na mali za mtu  mwingine uwe nazo wewe.
Amini usiamini, mtu mwenye mawazo ya  ubinafsi ikitokea eneo lote analoishi watu wote wakawa wagonjwa kama  yeye, hawajaolewa, hawana kazi, masikini utashangaa kuona mwanadamu huyo  anaishi kwa furaha, si kwa sababu ya mafanikio yake bali amekosa  aliyemzidi wa kujifananisha naye.
Najua maisha binafsi ni magumu,  lakini yanamafanikio makubwa sana. Kwani maisha kwa ujumla yana  changamoto nyingi sana. Mimi nimejifunza kwa vitendo na kuamini  yanafuraha na matumaini makubwa.
Geuza mtazamo wa matatizo yako na  kujitambua, hakika kwa kufanya hivyo  utaona utofauti wa kimaisha. Onyo,  usiache kuyashughulikia kwa  mtazamo chanya.
Hata hivyo, Mungu  akinisaidia wakati mwingine nitazungumzia faida za ubinafsi kwenye  safari ya mafanikio ya kimaisha, ingawa sitaeleza tamaa ya kutaka vya  wengine viwe vyako, ila nitafafanua umuhimu wa kutaka kufanana na mtu  fulani mwenye maendeleo zaidi yako.
Thursday, March 15, 2012
Matatizo yako na jinsi ya kujifariji mwenyewe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment