Watu wengi wamekuwa wepesi sana kukimbilia kwa rafiki zao ili kuomba  msaada wa mawazo ya nini wafanye kwenye mapenzi. Imani iliyojengeka kwa  watu wengi katika jamii yetu ni kuwa ushauri ni kitu muhimu sana kwa  kila hatua.
Kwa mtazamo wa haraka haraka unaweza kuishia kwenye  ukomo huo wa fikra na kuamini juu ya ushauri wa mtu kukufikisha mahali  sahihi kwenye mapenzi. Unapokerwa na mpenzi unakimbilia kushauriwa na  wakati mwingine hata unapotaka kuoa au kuachana na umpendaye, unamuomba  rafiki yako ushauri.
Je, umeshawhi kufikiria hasara za kuomba ushauri  wa kimapenzi kwa rafiki yako? Hebu ungana nami wiki hii ili nikumegee  kidogo hasara za ushauri.
UTAKUPOTOSHA 
Ni wazi kwamba kipimo  cha uelewa kinatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Ifahamike  kuwa, uhodari wa mambo nao hutofautiana, mtu anaweza kuwa mahiri katika  siasa na akaaminika kwenye jamii, lakini ukimpelekea suala la mapenzi  anakuwa hajui kitu, hivyo ni rahisi kukupotosha.
Uchunguzi  unaonyesha kuwa, wapenzi wengi sana hupotoshwa na rafiki zao wasiokuwa  na uelewa wa kutosha juu ya tatizo au suala husika la kimapenzi. Ni vema  kuwa makini unaposhauriwa.
UTARAHISISHA MAMBO
Mara nyingi  washauri huwa si wao wanaokabiliana na mambo, hivyo ni rahisi kwao  kupima vitu kwa juu juu tu na kushauri kirahisi rahisi. “Vipi kakupiga  namna hii, aaa huyu si mwanaume kwa kweli ni bora ukaachana naye.”  Anasema ni bora kuachana naye kwa sababu haumizwi na kuachana,  unayeachana ni wewe anayekushauri.
“Mkubali tu bwana unalaza  damu, hiyo tabia yake ya uhuni atabadilika, shosti unataka kuacha bahati  ipite?” Kwa mshauri ni rahisi kusema hivyo lakini kumbuka ukubwa wa  tatizo hatimaye utakabiliana nao wewe. Hii ina maana kwamba,  unapofikiria kuhusu ushauri ufikirie pia kuhusu kushauriwa jambo  kirahisi, ukiuvaa mkenge mwenye kuumia utakuwa ni wewe.
UTAKUGEUZA
Ulimwenguni  kuna aina zaidi ya 1000 za mapenzi na kila mmoja anatajwa kupenda kwa  staili zake. Mapenzi ni kama chembe hai nyekundu zilizopo kwenye damu ya  mwanadamu ambazo zinaelezwa na wataalamu kuwa hazifanani hata kidogo.  Uzoefu unaonyesha kuwa, washauri wengi hushauri kwa uzoefu wao, lakini  je ni sahihi uzoefu huo uwe msaada kwa mtu mwingine?
Jibu ni  hapana, kinachotokea mara nyingi kwenye ushauri ni mtu kumfanya mwenzake  awe kama yeye alivyo, yaani apuuze aamue na apende kama staili yake,  jambo ambalo haliwezekani kabisa kwenye mapenzi. Vipi Juma ageuke ghafla  awe kama Hassan kwenye suala la mapenzi? Ushauri ni muhimu lakini upime  kama unalingana na matakwa yako.
UTAKUONDOLEA UJASIRI
“Kwa  maelezo hayo mumeo ni malaya sana, naona itakuwa vigumu kumbadilisha,  ni bora ukaanza maisha yako kwa sababu kuna siku hali itakuwa mbaya.”
Huu  ni ushauri ambao unaweza kumuondolea mtu ujasiri wa kukabiliana na  tabia ya mumewe hadi kufikia hatua ya kumsaidia akaachana na tabia zake  mbaya.
Ushauri huondoa ujasiri wa kukabili tatizo hasa pale  anayekushauri atakapolipeleka suala lako kwenye njia ngumu isiyokuwa na  ufumbuzi. Ikumbukwe kuwa anayeamini kushindwa ni mshauri lakini wewe  kama mwanamke unaweza kusimama kutetea penzi lako na kuliweka sawa mpaka  jamii ikasema: “Jamani huyu dada kamrekebisha kweli mumewe, hakuwa hivi  alikuwa mlevi lakini sasa kaacha pombe.
UTAKUNYIMA FURSA
Kwenye  mapenzi kuna fursa nyingi za mafanikio ambazo unaweza usizipate ukiwa  mtu wa kusikiliza sana ushauri wa watu. Kuna wakati ambao unatakiwa  usimame wewe kuamua kumpenda mtu ambaye jamii inaona kama utapotea.
Thursday, March 15, 2012
Hasara 5 za ushauri wa rafiki kimapenzi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment