KUPANDA na kushuka ni hali ya kawaida katika maisha ya mwanadamu. Siku  zote dira ya kuishi inapatikana katika kanuni hii inayoacha giza la  maisha ya kesho. 
Pamoja na kuwepo kwa mambo hayo mawili katika  maisha yetu, imebainika kuwa kukosa limekuwa ni jambo baya linalokatisha  tamaa watu wengi. Ingawa kukosa ndiyo njia sahihi ya mwandamu  kujifunza, lakini si wote wanaopenda kujielemisha kupitia kwayo. 
Kukosa,  limekuwa ni suala la aibu na lenye kukatisha tamaa ya kuendelea kuishi.  Si wasomi wengi wanaofurahia kushindwa mitihani yao na wachache kati ya  watafuta kazi wanaoridhika na majibu ya HAPA HAKUNA KAZI, pindi  wanaposaka ajira.
Bila shaka hii ni changamoto kubwa katika  maisha ya wengi, machozi ya wanadamu yanadondoka chini pale suala la  kushindwa kufanikiwa katika jambo fulani linapotokea. Wasiopata usingizi  na wanyonge wa kauli wanatoka katika makundi ya waliojaribu mara nyingi  kupata wachumba, kutafuta kazi, kufanya biashara, kutafuta utajiri,  kulima na kujikuta wakipata jibu la kukosa.
Mpaka sasa tafiti  zinaonyesha kuwa, dunia imepoteza watu wengi kwa sababu ya ukataji  tamaa, hii ina maana kwamba, wengi hatufahamu mantiki ya kukosa katika  harakati za maisha yetu. Lakini ukweli unabaki kuwa mafanikio hayana  maana kama kutofanikiwa hakutakuwepo.
Mara nyingi mafanikio  makubwa ya kimaisha hutokana na kushindwa. Watoto wanapoanza kutambaa au  kutembea huanguka na kuumia, lakini kwao si apizo la kutorudia tena  kupiga hatua, bali ni zingatio la umakini zaidi juu ya nguvu na mbinu za  kutembea bila kudondoka wakati ujao. Hivi ndivyo inavyompasa mwanadamu  anayetafuta na kukosa, yaani ajaribu mara nyingi na asikate tamaa.
 Lakini  kwa kuwa ukataji tamaa mara nyingine si kitu cha kupenda na hasa  linapokuja suala la kuzama kwa matumaini yaliyokusudiwa na mhusika,  ndiyo maana nimeona ni muhimu kuandika mbinu kadhaa za kumsaidia mtu  aliyejaribu na kujikuta katika hali ya kukata tamaa.
KWANZA:  Jifunze kuwa mtu mwenye kutegemea mafanikio bila kujali kama una kitu au  huna. Ukilala na kuamka itazame kesho kuwa ndiyo siku ya kufanikiwa  kwako. Usikubali kuwa  na mtazamo wa kutofanikiwa, kwani mawazo ya aina  hiyo yatakuondolea ujasiri wa kujaribu na kujikuta unazidi kudidimia  katika matatizo. Kumbuka waliofanikiwa si miungu ni watu kama wewe!
PILI:  Ukikabiliwa na mawazo ya kukosa jipe muda wa kupumzika, kwa kusikiliza  muziki na nyimbo uzipendazo. Fanya mazoezi ya viungo na utembelee sehemu  zinazokuvutia, ukifanya hivyo utaiongezea akili yako nguvu ya kufikiri  vema na kupunguza uwezekano wa mawazo ya kukata tamaa kukua na  kukunyonya nguvu za kujaribu tena.
TATU: Zungumza na rafiki zako  mara kwa mara juu ya yale ambayo unaona hayaendi sawa. Usiwe mtu mwenye  kukaa peke yako chumbani, kwani utaipa uhuru mkubwa akiri kupembua na  kuzalisha mawazo hasi mengi ambayo yatazidi kulikuza tatizo lako.  Waswahili husema; akili isiyo na mawazo toka nje ni nyumba ya shetani.
NNE: Kaa chini na ufikiri zaidi kwa nini hukufanikiwa ulipojaribu.
lengo  la kufanya hivyo lisiwe katika kujihukumu, bali kukusanya nguvu zaidi  za kujaribu kwa mara nyingine. Ikiwa ulifeli mtihani, jiulize ni kwa  kiwango gani ulisoma, ili kama kuna mahali hukujituma, wakati mwingine  uongeze bidii.
TANO: Jiamini mwenyewe na usifikie hatua ya  kujihukumu na kujiona hufai miongoni mwa jamii. Usijilinganishe sana na  waliokuzidi kimaisha na kutamani kuwa kama wao kwa tukio la mvumo kama  kulala masikini kuamka tajiri. Usipojiamini na kujipenda mwenyewe huwezi  kufanikiwa kabisa. Fahamu wewe ni bora kuliko yule unayemuona mbele  yako.
SITA: Kumbuka kuwa tunajifunza kutokana na makosa, kwa  maana hiyo ukiona umeshindwa kufikia malengo, tambua kuwa umejifunza  siyo kwamba umekwama. Katika kushindwa zidi kupata ujuzi na  kujisahihisha. Ukizingatia hayo utajikuta kesho ya furaha inakuja mbele  yako.
Saturday, March 17, 2012
Je,Umekata Tamaa Maishani? Endelea Kusoma
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment