Saturday, March 17, 2012

Tofauti kati ya kutimiza lengo na kufanikiwa!

Utafiti wa kisaikolojia unaonesha kuwa, watu wengi sana wameweza kutimiza malengo waliyojiwekea maishani,lakini bado hawajafanikiwa hata kidogo japo wana kila kitu walichokihitaji katika maisha yao hapa duniani!Wapo waliokuwa na malengo ya kuwa madaktari,wanasheria,waalimu,waandishi wa habari na kila aina ya maisha mazuri ikiwemo kumiliki magari ya kifahari, majumba na wake wazuri lakini bado wanalia kwani hawajafanikiwa.

Hapa chini nitaainisha kwa ufupi maana za haya maneno mawili na jinsi ya kuyatofautisha.

KUTIMIZA LENGO:

Hapa ndipo kwenye mkanganyiko mkubwa sana, kwani watu wengi huishia hapa na wakifikiri kuwa tayari wameshafanikiwa maishani.

Kutimiza lengo ni kitendo cha kufikia yale uliyokuwa unayatamani kwa muda mrefu, yaani kupata kile ulichokihitaji maishani. Mfano labda ulikuwa na ndoto ya kuwa mhasibu, ukasoma kwa nguvu na bidii zote na hatimaye ukafikia kuwa mhasibu. Basi hapo unakuwa umetimiza lengo na kufanikiwa.

Mwandishi mmoja wa mambo ya saikolojia, Halord Sherman aliwahi kuandika katika kitabu chake cha The New TNT Miraculous Power within You kuwa, Getting what you ever wanted in Life, doesn’t indicate success’ akimaanisha kuwa kupata kila kitu ulichokihitaji maishani, haiashirii mafanikio’ na kwamba unaweza kutimiza kile unachokitaka lakini bado ukawa hujafanikiwa maana hauna furaha nacho! Kufanikiwa ni kufurahia ulichokifikia.

KUFANIKIWA:

Hiki ni kitendo cha kufurahia kile ulichokipata. Ni kweli kabisa ulitaka kuwa mwandishi wa habari sawa, lakini je, unafurahia uandishi wako wa habari? Ni kweli kabisa ulikuwa na ndoto na malengo ya kuwa mbunge, daktari, mkulima nk. Swali linabaki palepale kuwa una furaha na unachokifanya?

Nadhani sasa msomaji utakuwa umepata mwanga katika kutofautisha maneno haya mawili kati ya kutimiza lengo na kufanikiwa.

Hivyo basi kwa pamoja tumeweza kuona kuwa, kutimiza lengo ni kufikia au kupata kile ulichokuwa unakihitaji na kufanikiwa ni kuwa na furaha na ulichokipata.
Kwa hiyo mtu anaweza kufikia lengo lake lakini bado akawa hajafanikiwa kwa sababu hafurahii alichokipata.

Chukulia mfano kuwa, ulikuwa na hamu kubwa sana ya kununua gari na hilo likawa ndilo lengo lako. Baada ya mwaka mmoja ukanunua gari kweli. Lakini kila siku gari hilo linaharibika, halitunzi mafuta kila siku uko gereji. Je, utakuwa umefanikiwa kweli? Hapana, utakuwa umetimiza lengo la kununua gari lakini bado hujafanikiwa.

Mfano mwingine ni huu, wakati ukiwa kijana, ulikuwa na malengo ya kupata mume au mke bora, na ulipokua kweli ukapata mke/mume mzuri na familia bora. Kweli, baada ya miaka kadhaa ukapata mume/mke mzuri kama ulivyokuwa umelenga.

Lakini baada ya kuingia kwenye ndoa kila siku inakuwa ni ugomvi, malumbano na migogoro isiyoisha.Je, unakuwa umefanikiwa? Au umetimiza lengo la kuwa na mke/mume bora?

Jibu ni wazi kuwa unakuwa umetimiza lengo lakini unakuwa hujafanikiwa.
Jambo la msingi ambalo nataka kulisisitiza hapa ni kuwa, ni lazima umakini utumike katika kujiwekea malengo maishani. Jiwekee malengo ambayo ukiyatimiza basi ufurahie kuyafanya.



KATIKA maisha, ni bora ukajiwekea utaratibu wa kumtegemea Mungu maana yeye ndiyo kila kitu katika maisha yetu. Achana na ujanja wote wa kibinadamu.
Kuna msemo mmoja ambao aliwahi kuuongea King Martin Luther katika moja ya hotuba zake ambao unasema:

‘Don’t battle a war that you know you cant win!’ yaani akimaanisha usipigane vita ambayo unajua kabisa huwezi kushinda’.
Kwa nini nimetoa mfano huu, watu wengi sana wamekuwa wakifanya mambo ambayo hayawasaidii kupata maendeleo maishani mwao, na wanafanya hivyo kwa sababau tu fulani anafanya. Hayo siyo maisha.

Shida ambazo unazipitia kwa sasa, usizichukie na badala yake sasa zigeuze shida hizo kuwa kuni za kuchochea nguvu zako za kuelekea maishani. Usipende sana kujihukumu kwa makosa ambayo umeyafanya huko nyuma kwani hayawezi kufutika kwa kujilaumu na badala yake sasa anza upya kwa kufanya kazi kwa bidii huku ukibadilika siku hadi siku. Dada yangu mmoja ambaye ni mfanyakazi mwenzangu naomba nimtaje kwa jina moja la Naila aliwahi kuniambia kuwa:

“No one can go back and change a bad beginning. But any one can start now and create a successful ending. Every successful person has painful story! Every painful story has a successful ending.

Accept the pain and get ready for success. Have a good start!
Ni maneno yanayotia nuru mpya maishani. Dada huyu alimaanisha:
“Hakuna mtu anayeweza kubadilisha mwanzo mbaya. Lakini mtu anaweza kuanza na kutengeneza mwisho wenye mafanikio.

Kila mtu mwenye mafanikio ana historia yenye maumivu! Kila historia yenye maumivu ina mwisho wenye mafanikio. Kubali maumivu na uwe tayari kwa mafanikio. Nakutakia mwanzo mpya!”
Hata wewe msomaji wangu, endelea kupambana na maisha. Usikubali mtu yeyote akuvunje moyo.

Unapoanza safari ya kutafuta mafanikio, vitainuka vikwazo vingi mno. Watu watakuambia maneno ya kukatisha tamaa, watasema huwezi kwa sababu hukusoma, familia yako masikini na mengine mengi ya kuvunja moyo na kuondoa matumaini.
Jambo moja la kuzingatia ni kuwa, hakuna binadamu anayeweza kukuamulia maisha yako yawe vipi. Thamani yako ni kubwa sana na malengo uliyojiwekea ni lazima uyatimize na hatimaye kufanikiwa.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment