Saturday, March 17, 2012

Jinsi gani binadamu wenzetu wanavyoyaathiri maisha yetu

Hakuna mwanadamu aliyezaliwa kahaba, mwizi, jambazi, fisadi ua muuaji. Wote kwa namna zetu tumekuwa tulivyo kwa sababu ya harakati za kimaisha.

Pengine litakuwa swali la msingi kujiuliza, kwa nini kusiwepo na aina moja ya binadamu tofauti na tuonavyo leo, ikiwa wote tumezaliwa ‘wasafi’? Je kati yetu kuna waliopenda wenyewe kuwa wavuta bangi na wakabaji baada ya kuzaliwa kwao?

Tafiti hazionyeshi kwamba, wahalifu walichagua tabia hiyo, wengi kati yao hawakumbuki hata ni lini ilikuwa siku yao ya kwanza kuiba, kuvuta bangi na kulewa. Kama hilo halitoshi miongoni mwa watu waliofungwa na tamaa za ngono ambao walifanyiwa utafiti walionesha kutojua mwanzo wa tabia zao na kufanya liwepo jambo la kujiuliza tena, kwa nini hawajui na iweje wasikumbuke vitu walivyochagua kuvifanya katika maisha yao.

Katika hali ya kawaida ukahaba ni nembo (utambulisho wa mtu/kitu) kama watengeneza bidhaa wanavyofanya wanapozalisha mali zao. Ili mtu ajue kwamba ile ni sabuni fulani lazima mtengenezaji achukue jukumu la kuiwekea jina na kulibandika, iwe ubavuni au mahali popote kumuwezesha mtu kutambua. Hata Mungu katika uumbaji wake alivitambulisha vitu kwa nembo, kama tuviitavyo leo.

Wakati tukisonga mbele na somo letu ni vema tukakumbuka utangulizi wetu kwamba hakuna mwanadamu hata mmoja aliyezaliwa ni mwizi. Ikiwa ndivyo, tuna swali la kujiuliza ni nani ambaye amewawekea nembo majambazi tunaowaona leo mpaka jamii ikafikia hatua ya kuwaita “majambazi sugu.” Hapa kuna haja ya kujifunza zaida.

Siku zote waweka nembo ni watengenezaji wa bidhaa, hivyo wakiwepo majambazi, wezi na makahaba miongoni mwetu hawakufikia hapo kwa hiyari yao bali walitengenezwa na binadamu wenzao, ambapo utafiti wa hivi karibuni umeosha kuwa watu tunaowaamini na kuwapenda sana ndiyo wenye nafasi kubwa ya kutubandika nembo ya mawazo na tabia zao.

Katika hali ya kawaida kila mwanadamua ana mtazamo wake, lakini wengi kati yao hawajiamini katika mienendo na hivyo kuwa tayari kusikiliza na kufuata mara moja mitazamo ya wengine bila kulinganisha na kuhakiki ukweli. Wengi wetu tulikuwa hatunywi pombe, hatuvuti sigara, hatufanyi umalaya, hatusaliti ndoa kwa sababu tulikuwa na mtazamo wa aina hiyo.

Lakini kwa mshangao tukajikuta nasi tunakunywa pombe kama rafiki zetu tuliokuwa tunasoma nao. Tukaanza kuiba mali za kampuni, tukaingia kwenye makundi ya ukahaba, tukaanza usengenyeji na sasa tunaingia taratibu kwenye imani za kishirikina na tayari tumeshakwenda kwa waganga kutafuta dawa za kuwatengeneza waume zetu ili tuwatawale kwa mfano wa ‘shoga’ yetu fulani.

Tunaweza kujiuliza kwa nini tumefikia uamuzi huo? Jibu ni kwamba tumekubali binadamu wenzetu watupige nembo za uhuni, ujambazi, ukaidi, uvivu wa kusoma, utovu wa nidhamu kwa wazazi wetu na waalimu. Tumekubali kuwaunga mkono wenzetu walioshindwa kujenga ambao wanatuambia kuwa kwa maisha ya leo ni vigumu kujenga kwa mishahara midogo tunayolipwa na sisi tumekata tamaa kabisa ya kujiwekea malengo ya kujenga.

Hivi ndivyo binadamu wenzatu wanavyotufanya tuishi kwa mawazo yao, tubadili mitazamo yetu kwa kuiga fikra zao, tujisikie vibaya kwa tafsiri zao na wakati mwingine tunaona aibu kwa sababu ya wenzetu wanavyotusema.

“Aaa, yule hawezi kuzaa maziwa yake madogo” “Nani atamuoa mwanamke mbaya kama yeye” “Hana mvuto kabisa yule kaka, sijui nani atamkubali” “Hawezi kufaulu mitihani kwa sababu hana akili” “Atakufa tu kwa jinsi anavyoumwa umwa.”

Kifupi haya ndiyo maneno ya wanaotuwekea nembo, ambao ni rafiki zetu, ndugu na jamaa tunaowaamini sana. Uchunguzi unaonyesha kuwa asilimia 98 ya binadamu huishi kwa msukumo kutoka kwa watu wengine, lakini jambo baya zaidi ambalo pengini ndilo limenisukuma kuandika mada hii ni kwamba asilimia 89 kati ya hao wanaathiriwa na wenzao kwa kupigwa lebo mbaya huku asilimi 11 tu ndiyo ikitajwa kufanikiwa kwa kufuata mambo mema wafanyayo wengine.

Pengine tuhitimishe kwa kujiuliza kwa nini wengi wetu huathirika kwa sababu ya mitazamo ya wengine na nini cha kufanya? Jibu ni kwamba tumekubali kuacha kujiamini na kuanza kuishi kwa hofu ya kile wanachotafrisi wenzetu kuhusu sisi. Siku zote uwezo ni kitu cha ndani, inakuwaje mtu mwingine atuambie kuwa hatuna uwezo na sisi tumwamini na kunyongea kwa lebo yake?

Huu ni mwaka wa kumi kazini huna hata kiwanja, hujaanza kujenga unaogopa ukishindwa watu watakucheka. Unatumia dawa za kichina kuongeza urembo kwa sababu wanaume wanasema huvutii, umeacha kusoma kwa vile mama kakuambia huwezi kufaulu, umeamua kuwa mtumwa wa mapenzi kwa kumng’ang’ania mwanaume mkorofi kwa kuwa unaogopa akikuacha huwezi kupata mwingine, kamwe usikubali kupigwa lebo na mtu mwingine simamia imani yako na iga mafanikio ya wengine na si kushindwa kwao kiasi cha kujikuta umekuwa changudoa kwa sababu ya kumfuata rafiki yako kwenye magheto.

Kuanzia leo acha kukubaliana na mitazamo ya wengine kuhusu maisha yako, wapuuze wanaokuita majina mabaya, kataa kufuata mkumbo na usikubali kuona aibu kwa mitazamo ya rafiki zako wa karibu. Maisha ni wewe ukiweza au ukishindwa wa kuwajibika ni wewe.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment