Hakuna hata mmoja anayependa kupokea lawama mara kwa mara, na mara nyingi inategemea ni jinsi gani unavyomjibu yule anayekulaumu, labda utamwambia maneno ya dharau kejeli, matusi au kujibu kihasira. Kibaya zaidi ni kwamba majibu haya yote hayampoozi mlaumu, kinyume chake yanampa moto wa kuendelea kulaumu, na hivyo hali kuwa mbaya zaidi.
Katika hali zote lawama zinapotolewa kuna kiwango fulani cha upande mmoja kuhisi kutotendewa sawa, ingawa mara nyingine lawama hizi huelekezwa kwa asiye mhusika.
Wengi hupenda kuzirusha lawama kwa wale walio dhaifu kwao, mfano. Baba kumlaumu mama, mama kulaumu watoto au wafanyakazi nk.
Mara nyingi ni vigumu kunyamaza pale unaporushiwa lawama, hususan pale unapojua kabisa kuwa lawama hizo hazikustahili wewe, katika hali kama hii yakubidi ujitahidi kukaa kimya, kwa sababu muhimu zifuatazo:
1. Kama wote mtafuka moto na kuwa jeuri au kujibizana hakuna kitakachofanyika, hali itakuwa ngumu zaidi na mlaumu au mlalamishi atapata kitu kingine cha kulaumu juu yako, yamkini akasema wewe huambiliki.
2. Kwa vyovyote lawama zitakavyokuwa, fahamu tu kuwa mteja (ikiwa ni kwenye biashara) wakati wote ana haki, fahamu hakuna biashara bila huyo mteja. Hata kama amekosa, mlaumu wakati wote hujiona ana haki ya kutoa malalamiko yake na kusikilizwa. Kwa kunyamaza na kumsikiliza, unatunza kazi yako na kuiendeleza.
3. Kama kelele hazitapungua, lawama zaweza kuvuka mpaka na kuwa lawama au shutuma binafsi nahii yaweza kuleta ugomvi binafsi.
4. Kwa sababu ni rahisi sana kupandishwa hasira zaidi ya kupooza hasira, ikiwa utamruhusu mlaumu akupandishe hasira, utalazimika kuzielekezea hata kwa watu wengine wasio husika, ambao unahitaji kuwapa huduma pia. Hii siyo haki na inawapa mlango mwingine wa kuanza kukulaumu.
5. Ukiruhusu mtu akupandishe hasira, kiwango chako cha msongo wa mawazo kitapanda, na hivyo waweza kujikuta unapata matatizo kiafya. Mfano. Kuumwa kichwa mara kwa mara, mgongo kuuma, mshtuko wa tumbo, na mapigo ya moyo kuzidi kasi. BP, wale wenye vidonda vya tumbo huzidi kuuma nk.
6. Kuruhusu kupandiswa hasira mara kwa mara kazini, huwafanya wengi kwenda kuzishushia nyumbani, nahii huleta mfarakano na watu wa kwenye familia. Hasira na migongano hii ikizidi nyumbani, utalala na kuamka nayo na hivyo kwenda nayo kazini asubuhi, hii hukufanya kuanza siku na hasira na hivyo kukwaruzana na yeyote yule.
7. Unajua kabisa kuwa, siyo jukumu lako kukasirikia kazini dhidi ya mteja au wale unaowahudumia, hali hii ikitokea, utajihisi vibaya moyoni, na waweza kuwapoteza hata wale ulionao karibu na walio marafiki.
NINI TUFANYE KWA MTU MWENYE TABIA YA LAWAMA
Jitahidi kujiweka huru, mpole na usiyepaniki kwa vyovyote iwezekanavyo (be relaxed as possible) vuta pumzi ndefu, acha mabega na shingo yako iwe huru mbali na hasira na jaribu kuhisi utulivu.
Tulia hadi joto na moto wa mlaumu ushuke, ukijaribu kuweka neno hapo atatulia na kukuamkia tena. Mwili wako uonyeshe mawasiliano, weka pozi la utulivu siyo la shari, muangalie machoni, usimkwepe, kama ni kwenye meza, egemea kidogo upande wake kama vile uko tayari kumsikiliza kwa upole.
Msikilize anachosema sawia, ikiwezekana chukua karatasi na kalamu akuone ukiandika pointi za kile anacholaumu. Hii itakusaidia kumwonyesha kuwa unamaanisha na hivyo kushughulikia kile anacholaumu. Pia itakukumbusha wewe nini haswa kilikuwa kinalaumiwa mara baada ya yeye kunyamaza.
Baada ya kusikiliza anachokisema, mwonyeshe mlaumu kuwa unahisi sawa na vile anavyojisikia, na hata ingekuwa niwewe ungeumia au ungelaumu pia. Mfano; Mwambie; “Naelewa kabisa jinsi nilivyokuudhi hasa kwa jinsi ilivyotokea” hii inamwonyesha anayelaumu kuwa unamuhurumia na kwamba huoni kuwa analaumu tu bila sababu.
Pata muda wa kuliangalia tatizo kiundani, siyo mara zote mlaumu ana haki, ingawa hauhitaji kumwambia hivyo usoni kwake. Kama ni jambo litakalohitaji muda basi mwombe muda wa kulishughulikia na muahidi kumpa taarifa baadaye na kweli ufanye hivyo ulivyoahidi.
Pale unapogundua kuwa unamakosa katika lile lililokuwa lina laumiwa, basi kuwa mrahisi kuomba radhi na uwe mkweli usitake kufunika mambo na kujitetea.
Kamwe usijitetee, hatakama siyo wewe mhusika mfano; “Siyo kosa langu” mimi sikuwepo jana” kamwone bosi basi “Usilaumu kabla ya kuuliza kwanza” nk. Mlaumu hana muda wa kujua nani ni mhusika ili amlaumu yeye. Ukitupia lawama kwa wengine kama ni kwenye ofisi au kampuni basi unafanya wateja au mteja kupoteza imani na ofisi au wafanyakazi wengine.
Kinachotakiwa, fanya kile uwezacho kupunguza tatizo, na mlaumu akuone ukiwabize kulifanya hilo. Mara utakapo mweleza kuwa unafanya kitu basi akuone ukikifanya muda huo.
Usishangae, hata mtu unayemjua kuwa ni mpole, anaweza kuwa mkali mara tu anapogeuka kuanza kuwa mtoalawama, na hasa kama siyo mara ya kwanza kwa tatizo la jinsi hiyo kutokea. Ni ngumu kuanza tu kushughulikia kila anachokilaumu kabla kwanza haujashughulikia hisia zake. Zungumza naye kwanza. Mruhusu amalize kuongea ili apoe. Tingisha kichwa taratibu kuonyesha uko na yeye, akimaliza ongea taratibu.
Lawama kwa njia ya simu:
Katika hali hii, yakupasa ujitahidi kuwa mpole, hata kama hiyo simu inaingilia mambo na ratibu zako za kazi, najua hii ni ngumu hasa ukizingatia kuwa mlaumu hakuachii hata nafasi ya kumsikiliza, bali anafuka tu kama moto.
Weka kalamu na karatasi karibu na wewe mara zote (kama ni ofisini) akiacha nafasi kidogo, muulize jina lake na ikibidi anapiga simu kutoka wapi, au ofisi gani, kama huna uhakika mwambie akutajie tarakimu za jina lake au la ofisi.
Kama kuna kitu utalazimika kuangalia katika mafaili, vitabu au computer, basi muulize kama angependelea kusubiria katika simu (hold on) au angependa kukata simu na umpigie baada ya muda kidogo.
Kamwe usiweke mkono katika kisemeo (ikiwa ni simu ya mezani) mlaumu atajua kwamba umeamua kumfanyia ukatili na hutaki kumsikiliza. Hii ni kwa sababu simu za sasa zimetengenezwa katika hali ambayo sauti inapita sawa katika sehemu ya kuzungumza na sehemu ya kusikilizia.
Ikiwa unataka kumkatisha mlaumu, wakati wote. Jaribu kumwita kwa jina lake, hii itamfanya atulie kukusikiliza zaidi ya kusema “samahani” “unajua”, ni kweli…”
Kama ni kitu ambacho hautaweza kukishughulikia muda huo, muahidi karibu kuhakikisha madai yake yanashughulikiwa.
Labda kosa laweza kuwa lako, ikiwa hivi, basi kubali na kumtaka radhi, jaribu kumwelezea jinsi utakavyojitahidi kuweka mambo sawa, kamwe usijitetee wala kutupia lawama kwa wengine. Hali hii itakufanya uonekane dhaifu na mkwepa majukumu. Unapokubali na kushuka mara nyingi mlaumu naye huwa muelewa.
Ikiwa unaona lawama zinakuwa kubwa na kushindwa kuzitafutia ufumbuzi haraka basi tafuta eneo au upenyo wa maafikiano, hii itafanya kasi ya ujeuri wa mlaumu kupungua kwa sababu ni ngumu yeye kuendelea kupigizana kelele na mtu anayeafiki kila usemalo.
Lawama hizi za njia ya simu huwa zaidi katika ulimwengu wa biashara, lawama hizi huleta matatizo mengi zaidi.
Watu wengine ambao hawawezi kulaumu uso kwa uso, huwa rahisi kwa kutupa lawama kupitia simu. Katika biashara, au maofisini, hali huwa ngumu zaidi maana, unakuta mlaumu kishapiga simu kwa secretari (katibu muhtasi) nayeye akamruhusu mtu huyo aongee nawewe, basi anakuja na hasira mara dufu. Kama secretari siyo mchapakazi na labda amechelewa kumuunganisha mlaumu huyu na wewe basi mlaumu anaweza kutamani kukupasukia mara anapokupata wewe kwenye simu. Watu wengi huchemka zaidi kwenye simu zaidi ya wanavyokuwa ana kwa ana, hali hii hufanya maelewano kuwa magumu zaidi.
Kwa sababu hauwezi kuona sura ya huyo anayelaumu, wala mwili wake ni vigumu mmoja wenu kupoa maana haujui jinsi anavyojielezea au jinsi gani anamaanisha kutafuta suluhu.
Saturday, March 17, 2012
Jinsi ya kuishi na watu wenye tabia ya kulaumu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment