Saturday, March 17, 2012

Jinsi ya kuwa na mawasiliano bora

Mawasiliano bora ni muhimu kwa mafanikio yetu katika nyanja mbalimbali. Kama hatuna mawasiliano bora au hatuwezi kuwasiliana inavyotakiwa, itakuwa vigumu kwa watu wengine kutusaidia katika kile tunachokihitaji.

Kushindwa kuwasiliana vyema kunadumaza na mara nyingine kuua kabisa uhusiano baina yetu na wengine. Kwa maana hii basi hatuna budi kuzingatia sana maelezo na ushauri uliomo kwenye mada hii na kuufanyoa kazi.

Vitu vya kuzingatia
Yatazame au yachukulie mazungumzo yako na wengine kama majadiliano ya kawaida tu na siyo mashindano.

Hii itakusaidia kuwa na uhusiano na mawasiliano bora na wengine hususan pale utakapoyachukulia mazungumzo ya mara kwa mara kama majadiliano na siyo mashindano. Majadiliano ni mazungumzo yenye kusudi la kufikia suluhisho au muafaka fulani. Ni mazungumzo ambayo yanapotumika nia yake siyo kumuumiza wala kumuumbua mtu bali kutoa nafasi kwa pande zote kufikia matokeo bora.

Mazungumzo yenye ushindani ni yale yenye nia ya kuumiza, kuumbua, kuaibisha na kudharaulisha, ambayo nia yake ni kumuonesha mshindi na aliyeshindwa mwishoni mwa mazungumzo hayo.

Wale wenye tabia ya kuzungumza kiushindani huyachukulia mazungumzo kama nafasi ya kuonesha ubabe au kunyanyasa wengine. Hata kama yule mnayezungumza naye ana nia ya mashindano, wewe fanya majadiliano ya kawaida ili taratibu uweze kumbadilisha mtazamo wake.

Kuwa msikilizaji makini
Kati ya alama za kuonyesha kuwa wewe ni mwenye mawasiliano bora ni pamoja na uwezo wa kuwa msikilizaji mzuri. Wapo watu ambao hupenda kuongea tu na siyo kusikiliza. Sambamba na hilo, unatakiwa kuomba na wewe pia usikilizwe vizuri.

Muombe yule anayekusikiliza akuache umalize kuongea ndiyo na yeye aanze kuongea. Kamwe hamtafikia muafaka wowote ikiwa wote wawili mnaongea kwa wakati mmoja.
Yafuatayo yatakuwezesha kuwa msikilizaji mzuri.

Sikiliza na kuelewa kabla ya kujibu
Fahamu fika kile kinachozungumzwa, elewa nia na dhumuni la majadiliano.

Uliza swali pale unapodhani hujaelewa ili uweze kuelewa vyema nia ya mzungumzaji.
Jaribu kuweka kwa kifupi au kwa muhtasari kile kilichozungumzwa, mweleze anayezungumza unavyojihisi juu ya alichokuwa akikieleza na hakikisha ulimuelewa vyema.

Eleza unavyofikiri wewe. Mweleze aliyekuwa anazungumza kama umekubaliana naye au la, toa sababu za kukubaliana au kutokukubaliana.

Kuwa mzungumzaji mwenye ujasiri
Ujasiri katika mazungumzo huchochea uhalisi na kuaminika katika kile unachokisema.

Tabia za mzungumzaji bora
Zifuatazo ni tabia za mzungumzaji bora;
Tumia sentensi zinazokuelekea wewe zaidi ya sentensi zinazowaelekea wengine.

Jilenge wewe zaidi ya kuwalenga wenzako unapozungumza. Unapotumia sentensi za ‘ninyi’ au ‘wewe’ mara nyingi unaweza kuonekana usiye na ujasiri, tofauti na pale unapotumia sentensi zenye ‘mimi’. Unaweza kuonekana pia kama usiyejiamini.

Sentensi zenye ujasiri na zenye kukulenga wewe binafsi ni kama vile:
“Nimefurahi kukuona”
“Ningependa kuzungumza na wewe”

“Sijafurahishwa na maneno yako” na mengineyo. Katika mazungumzo yako tumia zaidi sentensi na siyo maswali. Hii itakuwezesha pia kuonesha kuwa una ujasiri katika kile unachokisema na unajiamini.

Mfumo wa mazungumzo ya kutumia maswali haujengi mawasiliano bora. Kwa mfano: “Hivi ninyi mnamwonaje yule rafiki yetu?”
Badala yake ungetakiwa kusema “Mimi sifurahishwi na matendo ya huyu rafiki yetu.”

Au mara nyingine baba wa nyumba anapouliza “Hivi mnadhani nani baba humu ndani?” Hii huonesha kutojiamini kwake.
“Hivi unafikiri mimi mjinga?”
“Hivi jamani sisi hatupewi huduma?”

Namna nyingine bora zaidi ya kuuliza swali ni:
“Je, waweza kunisaidia tafadhali?”
“Je, utakubali kuoana na mimi?”
Namna bora ya kuzungumza katika sentensi ni:
“Nitafurahi sana ikiwa utakubali kuoana na mimi” au “Nitafurahi sana kupata msaada
kutoka kwako.”

Matumizi ya sentensi za kukiri
Tumia zaidi sentensi zenye “kukiri” na siyo sentensi zenye lawama. Sentensi zenye kukiri ni zile ambazo anayezungumza anasema kile ambacho angetaka aone kikifanyika au kile ambacho angependa aone kikitendeka.

Kinyume chake ni sentensi zenye lawama; Hizi ni zile ambazo mzungumzaji anazungumza kile asichotaka au kile asichokipenda kitokee au kifanyike.
Mfano wa sentensi zenye lawama:

“Sipendi kabisa vile unavyonichukulia.”
“Sipendi kabisa unavyoniingilia katika maongezi.”
Mfano wa sentesi zenye kukiri; “Ningefurahi kama ungesubiri nimalize kwanza kuongea halafu na wewe utaongea.”

Sentensi zenye lawama huonesha ukosefu wa ujasiri kwa mzungumzaji, mbaya zaidi sentensi hizi hazisaidii chochote katika kubadili tabia ya yule anayeambiwa maana hazioneshi bayana ni nini kinachotakiwa kufanyika kama mbadala.

Sentensi zenye lawama pia huonesha wazi tabia yako sugu ya kulaumu. Pia huonesha vitu usivyovipenda tu na kuvisahau vile vizuri unavyovipenda.

Ni vigumu sana kumsaidia mtu ambaye analaumu usiku na mchana kuwa hapendi hiki, hapendi kile, hataki hiki na wala hataki kile na bado hawezi kusema anapenda au kutaka nini badala yake. Kwa hali hii watu hawa wanabaki kuwa walaumu mara dufu.

Lugha ya mwili wako iwe nzuri (Positive body language)
Lugha ya mwili ni vile tunavyoweza kutumia miili yetu kuonesha nia zetu. Mwili ni kiungo muhimu sana cha mawasiliano.

Tafiti zinasema kwamba, hata wakati mtu anazungumza kupitia mdomo, asilimia 60 (sitini) ya ujumbe wake hupitia au kueleweka siyo kwa kupitia maneno ya kinywani mwake bali ni kwa kupitia lugha ya mwili wake. Jambo hili ndilo hutiliwa mkazo na ule usemi usemao “Matendo huzungumza zaidi kuliko maneno.”

Lugha ya mwili huhusisha vitu kama vile muonekano wa sura (facial impression), mikunjo ya uso, macho yalivyowekwa, kinywa kilivyotumiwa, pua inavyofanywa wakati wa kuongea, mikono na pozi ya mwili ilivyo kwa ujumla wakati wa kuzungumza.

Ni vyema kujikumbusha kila wakati kuhusu umuhimu wa lugha ya mwili ili itusaidie kujijua sisi wenyewe na ule ujumbe tunaoutuma.

Hapa nataka kujaribu kueleza baadhi ya maeneo ya lugha ya mwili ambayo yatakusaidia kuweza kubadilika au kujirekebisha katika mchakato mzima wa mawasiliano kupitia mwili wako.


Kutembea kwa hatua za kudunda au kunesa
Kutembea huku huwasilisha hisia za ujasiri. Tabia hii huweza kuwa ya asili au ya kujifanyisha hususan pale unapodhani kuwa unachofanya ni cha muhimu zaidi na unapoamini kuwa wewe ni bora. Kutembea kwako kwaweza kuonesha kila kinachoendelea akilini mwako.

Kupanda au kushuka kwa sauti unapoongea
Pale unapojua hauna ugomvi au uadui na yeyote basi sauti yako itakuwa nzuri na ya kusikika kwa yeyote. Vituo vyako na misemo yako itakuwa ya kawaida na yenye uwiano. Pale unapohisi hofu au kuwepo kwa wabaya wako, mara nyingi sauti yako huwa chini na isiyo na ujasiri.
Unashauriwa kwa hali yoyote ujitahidi kuzungumza kwa sauti ya kati, isiyo chini sana wala juu sana.

Mavazi sahihi
Unapohisi una nafasi fulani katika jamii au sehemu fulani, utajikuta unajali sana suala la kuvaa kwako. Mavazi huweza kuzungumza nia ya moyo na huweza kuonesha picha mbaya au nzuri kwa wanaokutazama. Mavazi ya aina fulani huweza kukupa tafsiri mbaya kwa watu tofauti na vile ulivyo kihalisia. Kwa upande mwingine mavazi mengine yamefanya wengine kuonekana kama vile ni wa maana sana na wakutegemewa wakati uhalisi hauko hivyo.

Pozi zuri la mwili
Kuketi au kutembea katika mwili ulionyooka huonesha ujasiri. Hii ina maana kifua kinakuwa mbele na tumbo ndani kidogo. Hata askari waliojasiri hulazimika kuwa katika pozi hili. Pozi zuri ni ishara ya ukakamavu na afya njema.

Mwonekano wa macho
Mwonekano wetu machoni huweza kuonesha hofu, aibu au ujasiri hususan tunapokutwa katika maeneo au matukio ambayo hatukutarajia. Mwonekano wa macho huthibitisha ukweli au uongo wa kile tunachozungumza.Mwonekano wa macho yetu huweza pia kuthibitisha kumaanisha au kutokumaanisha, uhakika au kutokuwa na uhakika katika kile tunachokizungumza. Wako wengine wasioweza kamwe kuwatazama machoni wale wanaowahofia au kuwaogopa.

Ukaribu au mgusano
Tabia ya kujitenga na wengine huweza kumaanisha kujikweza au kukosa ujasiri. Jaribu kuwa karibu na wengine zaidi kadri utamaduni wa jamii uliyopo unavyokuruhusu.Kama kukumbatia kunaruhusiwa katika jamii yako, fanya hivyo. Kama kushika mkono ndiyo kunakoruhusiwa basi hakikisha unafanya hivyo, mara kwa mara. Mgusano wa mwili unamaana kubwa sana katika kuongeza ukaribu baina ya watu.

Ishara za mwili
Tumia ishara unapoongea (gestures). Mfano tumia mikono, tumia kichwa na macho kusisitiza unachoongea. Kuongea tu kwa madomo pasipo kiungo chochote cha mwili, hufanya mazungumzo yako kuwa butu sana. Ishara za mwili tunazitumia kusisitiza au kuthibitisha tunachokiongea.

Ishara hizi za mwili zitumike taratibu, zisizidishwe sana maana zaweza kuwabughudhi wengine.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment