Saturday, March 17, 2012

Mambo ya kufanya unapoboreka

Maisha tunayoishi yamejaa kasi zinazosababisha watu wengi kuboreka. Tangu asubuhi tunapoamka, tunakutana na mambo mengi yanayozichosha akili zetu na kutuletea msongo. Zifuatazo ni dondoo nyepesi zinazoweza kukutoa kwenye hali ya kuboreka na kukurudisha kwenye furaha na uchangamfu.

1. Fanya mambo unayoyapenda
Kila mtu ana jambo ambalo akilifanya hujisikia furaha. Kama ni kuangalia au kucheza soka, kusikiliza muziki laini, kuangalia filamu, kutembea kwenye bustani za maua au vinginevyo, fanya kwa lengo la kutuliza mawazo na hisia zako, utaona mabadiliko.

2. Jenga picha nzuri akilini
Yawezekana umeboreka kwa sababu umejaza fikra nyingi chungu mawazoni mwako. Futa yote uliyokuwa unayafikiria na vuta taswira ya mandhari tulivu.

3. Imba kwa sauti
Bila shaka kuna wimbo unaoweza kuuimba vizuri. Bila kujali kama umesahau baadhi ya mashairi au la, imba kwa sauti huku ukijisikiliza kwa makini, jilazimishe kufurahia jinsi unavyoimba. Wataalam wa ubongo na akili wanaeleza kuwa kusikiliza ‘tune’ yako mwenyewe husaidia sana kutuliza mawazo.

4. Jichanganye na marafiki
Yawezekana huna mazoea ya kujichanganya sana na marafiki au watu wanaokuzunguka. Unapohisi umeboreka, jilazimishe kuchangamana na wenzako, shiriki kwenye mazungumzo au shughuli wanayoifanya na utahisi ahueni kubwa.

5. Tafakari kuhusu kilichokukwaza
Kama umeboreka kutokana na kazi nyingi, mazingira uliyopo au kwa sababu ya watu waliokuzunguka, jiulize kwa makini na ukishabaini sababu iliyokufanya uwe hivyo, tafuta njia ya kujitoa. Unaweza kuondoka mahali ulipo na kwenda sehemu nyingine tulivu kwa muda, akili ikitulia rudi na endelea na utaratibu wako.

6. Zitawale pumzi zako
Miongoni mwa mbinu inayoaminika kutuliza akili pale unapoboreka ni kuzitawala pumzi zako. Unapohisi kuna jambo haliko sawa, unashauriwa kuanza kuvuta hewa taratibu kwa kutumia pua na kuitoa kupitia mdomo. Vuta pumzi ndefu na ibane kwa sekunde kadhaa, kisha anza kuiachia taratibu.

7. Washirikishe wenzako
Kama jambo lililokufanya uboreke unahisi liko nje ya uwezo wako, washirikishe watu unaowaamini na usione aibu kuomba msaada. Wataalam wa saikolojia wanaeleza kuwa, jambo unaloliona ni zito na halitatuliki, ukianza kulijadili na wenzako utagundua kuwa kumbe linawezekana.

8. Kunywa maji mengi
Maji yanaelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa kutuliza mifumo mbalimbali ya mwili, ukiwemo mfumo wa kufikiri. Unapoona umeelemewa na hisia chungu, kunywa maji mengi taratibu na yaache yasambae kwenye mishipa yako ya damu. Unashauriwa kuwa na mazoea ya kunywa angalau glasi nane kwa siku.

9. Jipe muda wa kupumzika
Kupata muda wa kutosha wa kupumzika ni miongoni mwa vitu vinavyopunguza kwa kiwango kikubwa kuboreka. Mapumziko ya kitandani (siyo kulala usingizi) husaidia kutuliza mwili na akili. Jijengee ratiba ya kupumzika kitandani kabla ya kulala. Pata muda wa kutosha wa kulala angalau saa 8 kila siku. Lala muda muafaka na amka mapema.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment