Saturday, March 17, 2012

Jitambue Kesho inavyozuia mafanikio ya wanadamu

Ni mara ngapi unawaza kuhusu “KESHO” je umeshawahi kujiuliza jinsi inavyozuia mafanikio yako kimaisha? Uchunguzi unaonesha kwamba watu wengi ambao hawajafanikiwa mpaka sasa kwenye maisha yao ni wale wanaofikiria zaidi kesho na kupuuza leo.

Katika hali ya kawaida mafanikio ya kesho hayapo, yakiwepo ujue yametokana na leo. Kama utakuwa mtu wa kusema moyoni mwako nitakwenda kazini kesho, nitajituma zaidi kesho, nitafanya hiki na kile kesho utajikuta kesho haziishi na kila zikujiapo huja tupu.

Katika uchunguzi wangu nimebaini kwamba, watu wengi wanazitegemea zaidi nyakati zijazo kufikia malengo yao. Utakuta mwanafunzi anaingiwa na uvivu wa kusoma kwa kuusikiliza mfumo wa ndani wa nafasi yake unaotawaliwa na ulimwengu wa kesho au nyakati zijazo. “Leo nimechoka sana nitasoma kesho, mtihani bado uko mbali nitajiandaa zaidi wiki ijayo.”

Tafsiri ya kusogeza mbele matumaini ni uvivu na hali ya kushindwa kutekeleza majukumu. Wengi wetu tunadhani kesho itakuja na zawadi ya wasiofanya kazi,
wasiojituma, wasiwajibika jambo ambalo si kweli. Siku zote kesho ya mafanikio inatokana na matendo ya leo.

Hii ina maana kwamba, kulala kizembe na kusema ‘One day yes’, eti siku moja mambo yatakuwa mazuri, huko ni kujidanganya na kujijengea ukuta wa kutofanikiwa maishani.
Mara nyingi kinachowafanya watu wengi watumaini nafuu ya kesho ni woga wa kukabili changamoto za matatizo na misuguano ya kimaisha na hivyo kuamini kwamba watakapoamka kesho yake, kazi ya kubeba zege inaweza kuwa si nzito na hivyo kupata fedha kwa urahisi zaidi.

Katika hali ya kawaida ukweli unabaki kuwa anayejituma kulima kuvuja jasho kujitaabisha kwa kazi hizi na zile kujibana, kukabiliana na changamoto za kimaisha kwa siku ya leo ndiye atakayepata mafanikio kesho. Sina shaka na hili mtu havuni kesho asipopanda leo.

Kama wanadamu wenye matumani ya kufanikiwa hatuna budi kujifunza na kufahamu kwamba kesho ina madhara makubwa sana kwenye maisha yetu. Tumekuwa nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi kwa sababu tunaamini katika kesho na hivyo kupuuza leo kwenye mawazo yetu.

Utakuta mtu amepata mshahara leo, lakini moyoni mwake yanaibuka mawazo: “zitumie tu bwana kwani huu ni mshahara wa mwisho kama ni kodi ya nyumba utaanza kuweka mwezi ujao.” Matokeo yake muda wa kulipa kodi unafika hana hata akiba licha ya miezi mingi ya kujipa matumaini kupita.

Tunapoendelea na mada hii lazima tujiulize tunaposukuma matumaini ya kesho, leo tumeshindwa nini kuyapata. Je tumefanya nini cha kuifanya kesho ije na mafanikio? Jambo la kujiuliza tangu umeanza kazi zimepita kesho ngapi, iweje ijayo iwe na nafuu kwako kimaisha. Tuache kujidanganya lazima tujitume leo ili kesho tupate.

Kila siku uamkapo hakikisha kwamba majukumu yako ya kimaisha umeyafanya kwa kiwango kinachostahili. Siku inayofuata nayo jitume, tumia uwezo wako wote usikubali kujilegeza kwa kisingizio cha kufanya zaidi wakati ujao. Maisha yenye uhakika yapo leo ya kesho ni ya kubahatisha.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment