Uamuzi  wa ndoa si wa kujaribu. Unatakiwa kujihakikishia kwamba ni kweli  umevutiwa na kila kitu cha mwenzako, kwamba utakuwa naye katika shida na  raha. Hayo ndiyo mambo ya kuzingatia.
Nimeshaandika mengi kuhusu  sifa za anayetakiwa kuoa au kuolewa, lakini nasogea mbele zaidi na  kuangalia sababu za kumpenda mtarajiwa wako katika ndoa. 
Zipo  sababu za msingi sana ambazo unatakiwa kuwa nazo kabla ya kuingia kwenye  ndoa
KWA NINI UJIULIZE
Lazima nifafanue hili kwanza kabla ya kuendelea. Hivi unafikiri ni kwa nini ni lazima kujiuliza sababu za kumpenda mwenzi wako?
Yes!  Ni kwa lengo la kujiwekea usalama katika ndoa yako ijayo. Kujiandalia  amani na pumziko la kweli. Kwenye mapenzi ya dhati pekee ndipo  vinapopatikana vitu nilivyotaja hapo juu.
Kwa maneno mengine kuwa  na majibu ya swali linalosomeka kwenye kichwa cha mada hii ni  kujihakikishia ndoa bora. Tuendelee kujifunza.
NI MWENZI WA NDOTO ZAKO?
Jambo  kubwa kuliko yote ambalo unatakiwa kuliangalia kwa jicho la tatu ni  kama mwenzi huyo ni wa ndoto zako. Je, yukoje? Rafiki, siku zote kabla  ya kuamua kufanya chochote lazima ujiulize kama ndicho ulichokuwa  ukikifikiria.
Hata kwa upande wa mwenzi wako, lazima ujiridhishe, ni  kweli ni yule uliyekuwa unamtarajia? Ana sifa unazohitaji? Acha tabia ya  kujifariji kwamba utampenda taratibu ndani ya ndoa, hicho kitu hakipo.
Hakuna  kujifunza kupenda katika ndoa, lazima ujihakikishie mwenyewe kuwa  mwenzi wako ni yule mwenye sifa ulizokuwa ukizitarajia. Hili ni la  msingi, maana unaweza kuwa naye siku mbili, ukatamani mwingine nje, kwa   nini? Kwa sababu si yule mwenye sifa ulizotarajia.
NI SURA, UMBILE?
Kuna  baadhi ya watu utawasikia wakisema: “Mpenzi wangu ananivutia sana,  yaani ni mzuri sana. Najua hata nikitoka naye, marafiki zangu  watanisifia kwa kuchagua vizuri...”
Hizi ni fikra potofu ndugu zangu.  Mapenzi ya kweli hayapo kwenye sura wala umbile la mtu. Vipo vigezo vya  muhimu kabisa vya kuzingatia tofauti na uzuri wa sura.
Sura  hubadilika ndugu zangu, binadamu wanazeeka, kuna kuugua na matatizo  mengine ambayo yanaweza kubadilisha mwonekano ambao ulikuvutia. Je,  yakitokea ndiyo utakuwa mwisho wa kumpenda?
Kama leo hii unamuoa kwa  sababu umevutiwa na matiti yake madogo, akishazaa na kunyonyesha kisha  yakaanguka, ndiyo mwisho wa kumpenda? Umempendea ngozi yake nyororo,  akipata ‘aleji’ ya mafuta, ngozi ikaharibika na kuwa na mabakamabaka  utakuwa mwisho wenu?
Wewe mwenye mpango wa kuolewa na mwanaume  mwenye kigezo cha kifua cha kimapenzi, kesho akifutuka na kuwa na  kitambi utamuacha? Rafiki yangu, kiukweli ni kwamba kigezo cha uzuri wa  sura na umbile si sahihi kabisa katika kuchagua mwenzi. Vipo vitu  vingine muhimu zaidi vya kuangalia.
Kama ulikuwa unaishi katika  dunia ya fikra hizo, hama ndugu yangu.
Saturday, March 17, 2012
Kabla ya ndoa jiulize, kwa nini umempenda
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment