Mapenzi ni suala  linalotakiwa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa ili yasije yakaleta madhara.
 Yawezekana mwaka uliopita ulifanya makosa na ukampa nafasi mtu ambaye mwishoni alikutibulia furaha yako. Usifanye tena makosa! 
 Chagua mtu sahihi kisha hakikisha unampatia mapenzi ya kweli ili naye aweze kukupatia kile ulichotarajia kutoka kwake.
 Baada ya kusema hayo sasa nirudi kwenye mada yangu. Nazungumzia mapenzi  ya muda au wazungu wanaita ‘temporary love’. Inaweza ikatokea uko  kwenye uhusiano na mtu ambaye ulimuahidi kumpenda daima na kwamba  hutamsaliti.
Mpenzi wako huyo mnaishi pamoja lakini sasa inatokea  mnatengana kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wenu. Wewe  unabaki Tanzania mwenzako anakwenda masomoni Uingereza.
Katika  mazingira hayo ni wachache sana wanaoweza kuvumiliana, wengi huwasaliti  wapenzi wao kwa kuanzisha uhusiano wa muda na wa siri na mtu mwingine.
Inakuwaje?
 Ilishawahi kutokea kwa rafiki yangu, mpenzi wake alipata nafasi ya  kwenda kusoma Marekani. Baada ya muda mfupi akaniambia hawezi kukaa bila  demu hivyo kuna kasichana kanajua kila kitu kuhusu uhusiano wao lakini  kapo tayari kuwa naye kwa muda lakini kwa siri.
Nilijaribu kumsihi  asimsaliti shemeji yangu lakini hakunielewa hivyo jamaa akaendelea na  yule demu mpaka siku chache kabla ya yule mpenzi wake kurudi, ndiyo  wakaachana.
Sasa hivi jamaa anaendelea na mpenzi wake kama kawaida na yule demu aliyekuwa naye kwa muda wanaheshimiana kama dada na kaka.
Nini madhara yake?
 Kwanza katika mazingira haya inaonekana huyu mwanaume hana mapenzi ya  dhati kwa mpenzi wake na endapo itagundulika kuwa alikuwa na mtu kwa  muda, uhusiano wao hauwezi kudumu.
Lakini pia kuna uwezekano mkubwa  wa mtu kunogewa. Mwanaume anaweza kunogewa na penzi la yule demu na  huenda akabaini kuna vitu alikuwa akivipata kutoka kwake lakini mpenzi  wake hana.
Hali hii inaweza kusababisha akamsaliti tena na kama  waswahili wasemavyo kuwa muonja asali haonji mara moja, mwisho atachonga  mzinga.
Pia watu wanapoanzisha uhusiano kwa muda ni vigumu kuachana  moja kwa moja. Kwa maana hiyo mwanaume huyu anaweza kuutibua uhusiano  wake kwa penzi la nje aliloonja.
Uhusiano wa muda ni sahihi?
 Hauwezi kuwa sahihi hata siku moja na wanaofanya hivyo ni wasaliti  ambao wanaweza kujikuta wanajiingiza kwenye matatizo makubwa.
 Uvumilivu unatakiwa kuchukua nafasi yake. Kama mpenzi wako yuko mbali na  wewe, mtunzie penzi lake. Ukiwa kiruka njia hata kama ni kwa siri Mungu  anaweza kukuadhibu na ukajikuta unajuta.
Neno langu
Tuache  ulimbukeni kwa kuwa na tamaa za kijinga. Kila unalomfanyia mwenzako  kama ni baya jiulize na wewe ukifanyiwa na ukajua utajisikiaje?
Leo  hii ukisikia mpenzi wako aliye mbali na wewe kaanzisha uhusiano na mtu  mwingine eti kwa kuwa kashindwa kuzizuia hisia zake za mapenzi  utajisikiaje?
Huwezi kujisikia vizuri na kama utachukulia poa basi utakuwa huna mapenzi ya dhati kwake.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo.
Saturday, March 17, 2012
Je,Ni sahihi kujiingiza kwenye penzi la muda ‘temporary love’?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment