Kama bado hujaingia kwenye ndoa, huu  ni wakati wako sahihi wa kufanya uchaguzi bora ambao hautakuwa na majuto  hapo baadaye. Hapa nazungumzia juu ya kutizama maisha yako yajayo.
Acha  kuangalia leo, wakati kesho yako inaonekana wazi kuwa mbaya yenye  majuto ya kila aina. Hapa nitachambua kwa mapana mambo mawili makubwa;  Hisia na maisha!
Wapo rafiki zangu ambao wanakubali kuongozwa zaidi  na hisia huku wakiacha maisha yao ya baadaye yawe mabaya. Ieleweke  kwamba, maisha utakayoishi kesho ni matokeo ya jinsi unavyoishi leo.
Wakati  mwingine mtu anakuwa na mpenzi wake, ana kasoro kibao, kila siku  ugomvi, hakuna maelewano, lakini kila anapotaka kuachana naye, hisia  kali za mapenzi dhidi yake zinamzidi na kujikuta akiendelea kuwepo  kwenye penzi la mateso.
Huu si wakati wa kunyanyasika katika mapenzi,  ni muda ambao unatakiwa kuangalia vyema tabia na mienendo ya mpenzi  wako. Kama hairidhishi, usijiumize; Chukua hatua ya moja kwa moja huku  ukizingatia kwamba, maisha yako yanayofuata yatakuwa bora ukijivunia  ujana wako.
Hata kama unampenda sana, anajua mapenzi sana, ana  faida gani kama kila siku ameendelea kukuumiza? Kukunyanyasa?  Kukusimanga? Haoni faida yako, anakudharau waziwazi! Kwa nini uendelee  kukaa kifungoni wakati kuna njia?
Mwamuzi wa maisha yako ni wewe,  hatatokea mtu wa kukupangia maisha bora hapo baadaye, yote hayo unapaswa  kufanya mwenyewe. Chagua maisha unayoyapenda.
Nina maana gani  ninaposema maisha? Rafiki zangu, huu ni mustakabali wa maisha  yanayofuata. Kwamba maisha yako baada ya leo ni yapi? Unahitaji kuishi  maisha gani?
Maana kama ukiwa hujui unataka kuishi vipi, utakuwa  unakwenda bora siku zisogee na mwishowe utajikuta ukiingia kwenye  majuto. Kwa nini uingie kwenye majuto wakati unaweza kujipanga na  kufanya kesho yako iwe bora zaidi?
Ndugu zangu, ninapozungumzia  kuhusu hisia nina maana kubwa sana. Kwanza, fahamu kuwa hisia na mapenzi  ni vitu viwili tofauti kabisa, ingawa ili uwe na hisia lazima pia uwe  na mapenzi.
Kwa maneno mengine, mtu mwenye mapenzi ya dhati ni  rahisi zaidi kuongozwa na hisia kuliko mwenye hisia kupanda mbegu ya  mapenzi ndani ya moyo wake. Hisia katika mapenzi, tunaitafsiri kama ile  hali ya kuingiwa na mapenzi ndani ya moyo kupitiliza, pia kuzama katika  penzi kiasi cha kuwa mpofu wa kutoweza kuona mbadala wake.
Mtu  mwenye hisia kali za mapenzi kwa mwenzi wake, huwa haamini kama kuna  mwingine ambaye anaweza kuwa kama mpenzi wake, hali hii inasababisha  kufunika makosa au matatizo yatakayotokea katika uhusiano wao hata kama  ni makubwa.
Akibahatika kugundua, basi uulizaji wake unakuwa si wa  kujiamini sana, lakini pia ni mwepesi wa kuyumbishwa au hata kuomba  msamaha kwa kosa ambalo ni la mpenzi wake. Huyu tunamwita anayeongozwa  na hisia.
Mtu mwenye hisia zaidi kuliko mapenzi, yupo tayari  kuishi maisha ya kubahatisha bila kuwa na mipango ya mbele, lakini awe   na mpenzi wake. Huu ni ulimbukeni wa hali ya hali juu. Rafiki zangu,  kifungo si lazima upelekwe gerezani, hata wewe unaweza kujiingiza katika  kifungo cha mapenzi.
Usikubali kuendelea kuwa katika mapenzi na  mtu ambaye unajua wazi ana kasoro kibao, kwa sababu eti unampenda! Hata  kama unampenda kwa kiwango gani, lakini ndiyo hivyo si mwaminifu,  mkorofi, hana heshima; Utaendeleaje na mpenzi wa aina hii?
Lakini  katika yote hayo, tatizo kubwa zaidi ambalo ni la hatari, ni ile hali  ya kuwa na mwenzi ambaye si mwaminifu. Kutokana na kigezo chako cha  kuangalia jinsi hisia zako zinavyokuongoza, wakati mwingine unaweza  kusalitiwa lakini usijue au unajua lakini unaamua kuacha kwa kuhofia  kumpoteza. Huu ni ulimbukeni rafiki zangu.
Katika suala la  usaliti ni vizuri kuwa makini katika kufanya uchunguzi kwanza kabla ya  kufanya maamuzi. Mathalani mpenzi wako amekuja, anaonekana  amechoka-choka, hana furaha na uso  mng’avu kabisa!
Tabasamu lake  halipo na kwa kumwangalia tu usoni unagundua kwamba ana alama ya busu  kwenye shavu lake! Wakati mwingine ananukia manukato ambayo siyo  aliyoyatumia asubuhi.
Au anaweza kuja na furaha kupitiliza,  uchangamfu kupitiliza, kukukumbatia kwa muda mrefu zaidi kuliko kawaida  ambavyo mmezoeana n.k.
Hizi ni dalili za wazi kabisa, katika hali  kama hiyo lazima uwe na mashaka na inawezekana akawa ametoka kwa mtu  mwingine. Alama ya busu shavuni mwake, haina haja ya kuwa na maswali  mengi maana tayari jibu utakuwa nalo.
Saturday, March 17, 2012
Unajua Kwamba unaweza kuwa chanzo cha maumivu yako
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment