Sunday, March 18, 2012

Kwa Nini Kila siku unakimbiwa na wanawake

Wewe mwanaume unayesoma hapa, jiulize; huwa unadumu na mwenzi wako? Unaachwa au kukimbiwa baada ya muda mfupi? Kama jibu ni ndiyo, hapa utapata tiba. Sikia nikuambie, wapo wengi ambao kila wakianzisha uhusiano, siku mbili tatu, mwanamke anamkimbia.
Anampenda sana, anamfanyia kila kitu ambacho yeye anaamini kinakidhi kwa mwanamke wake, lakini baada ya muda mfupi sana, anaachwa! Anabaki kujiuliza maswali yasiyo na majibu. Rafiki yangu, lazima ujue kwamba pamoja na kuwa mapenzi hayana kanuni za moja kwa moja, zipo ndogo ndogo ambazo zikifuatwa, mateso kwako yatakuwa ni kitendawili.
Huwezi kukimbiwa na wanawake bila sababu za msingi, lazima kuna kitu kinachosababisha uachwe. Hapo sasa hakuna sababu moja, wewe ukiachwa kwa sababu hii, mwingine atakimbiwa kwa sababu ile. Katika darasa hili, ukijifunza kwa umakini utaweza kujua kasoro yako ilipokuwa na kufanya mabadiliko ili ‘usiachike’ tena!
Wanaume huwa wanawalaumu zaidi wanawake kutokana na sababu za hapa na pale zinazosababisha kuachana kwao. Lakini wengine hutoswa bila kuelezwa sababu za msingi, akibaki na maswali mengi lakini mwisho hupata msichana mwingine kabla ya kuachana naye tena bila kujua sababu halisi.
Wakati mwingine sababu zenyewe huwa za maana lakini zingine mh! Ni aibu kuzitaja hadharani. Hata hivyo, kuna wengine huamua kuachana na wapenzi wao kwa makosa ambayo wao hudhani ni makosa kumbe wao ndiyo wanaokosea! Hebu tuone…

UKOJE?
Kama una tatizo la kuachana na wapenzi kila wakati, kipegele hiki kinakuhusu! Anza kuangalia tabia zako upya. Unaishije na mpenzi wako, jirani zako na watu wanaokuzunguka? Unatumiaje ulimi wako? Wasichana wengi wanapenda wanaume wachangamfu na wacheshi wakiamini kwa namna moja ama nyingine, ni burudani kwao lakini huwa hawapendi kabisa uwachangamkie wengine kupita kiasi.
Wanaume wengi hupingana na hili lakini utafiti unaonyesha kwamba, asilimia 70 ya wanaume wanaowachangamkia sana wanawake, mwisho wake hufanya nao mapenzi kama siyo kuingia katika uhusiano moja kwa moja. Usibishe, tafiti uone!
Kama una tabia hii, hata kama unaamini kwamba uchangamfu wako siyo wa nia mbaya kwa wanawake, achana nao maana unamkwaza mpenzi wako bila kujua. Wakati mwingine anaweza kuonyesha wivu lakini mwingine hawezi kusema, hivyo hubaki akiumia moyoni mwake lakini akichoka huamua kuachana na wewe hata kama anakupenda akihofia kuwa katika penzi la kuchangia. Angalia vizuri tabia zako katika kipengele hiki.



MWANAMKE MATUNZO!

Hapa jamani inabidi tuambiane ukweli, tena bila kufichana! Kuna baadhi ya wanaume ni wabahili sana, yaani kutoa fedha kwa wapenzi wao wanaona shida sana. Visingizio vya kwamba wao siyo mabuzi ndiyo vimewajaa akilini mwao.
Utawasikia wakisema; “Mimi siyo buzi bwana, demu wangu halafu nimlipie? Haiwezekani!” Achana na hizo fikra ndugu yangu. Unatakiwa utoe matunzo kwa mpenzi wako. Siyo lazima mpaka akuambie! Ni jukumu lako kufahamu aina za vipodozi anavyotumia.
Mnunulie bila kukuambia, mpelekee, kuwa mbunifu, ukiona nywele zake zinaanza kufumuka, mpe fedha ya saluni, tena ikiwezekana mchagulie mtindo uupendao. Leo asuke rasta za kimasai, baada ya wiki kadhaa unambadilishia mtindo mwingine.
Jiulize kama wewe ndiye mpenzi wake halafu unakataa kumpa matunzo, unataka nani amhudumie? Hivi ulivyokutana naye akiwa mzuri, anapendeza unadhani ni nani aliyekuwa anamhudumia?
Nakuhakikishia ndugu yangu, kama huna utamaduni wa kutoa matunzo kwa mpenzi wako tarajia kukimbiwa! Kwa maneno mengine ni kwamba, kama hutoi matunzo kwa mpenzi wako ni kama umemruhusu awe katika uhusiano na mwanaume mwingine ambaye atatoa matunzo.
Ni wajibu wako kumnunulia mavazi, manukato na hata fedha za matumizi yake binafsi. Tatizo hili huwakumba hata wanandoa, hawataki kuwahudumia wake zao, wakidai kwamba wameshaoa! Usimpompendezesha atapendeza? Na asipovutia unadhani nini kitafuata kama siyo kutafuta mwanaume mwingine nje? Upo tayari kusalitiwa?


Inawezekana unashangaa kwa nini wanawake wanakukimbia kila siku, kumbe kuna sehemu fulani huwa unakosea bila kujua. Hapa ndipo kwenye dawa. Ndiyo sehemu pekee utakayoujua ukweli na kuchukua hatua.
Katika sehemu ya kwanza, wiki iliyopita nilianza kwa kuelezea tabia mbili; moja ikiwa kujiangalia upya tabia zako na pili ni kumpa matunzo mwenzi wako.
Lazima wanaume mfahamu kwamba hata gari linapoharibika huhitajika kupelekwa gereji kwa kufanyiwa ukarabati. Vivyo hivyo hata mwanamke anahitajika kupewa matunzo ili aendelee kuwa bora na anayekuvutia.
Ukweli ni kwamba, wanaume wengi hukwepa kutoa matunzo ya karibu kwa wapenzi wao wakidai wanachunwa! Nani amekudanganya ndugu yangu? Kumtunza mpenzi wako siyo kuchunwa!
Mpendezeshe apendeze, usipofanya hivyo wewe unataka nani akutunzie? Kama una tabia hii badilika haraka, maana wanawake wa sasa wapo makini kuangalia wanaume ambao wanatambua wajibu wao.
Kuna mwingine huwa hatoi fedha mpaka siku atakayolala na mpenzi wake, hiyo ni mbaya zaidi maana hisia za kwamba umemnunua huanzia hapo.
Najaribu kuwaweka sawa na kuwakumbusha kwamba mwanamke anahitaji matunzo na kama ukishindwa kumtunza utakuwa unampa mwanya wa kutafuta mwanaume mwingine. Hapo ndiyo mwanzo wa usaliti.

UKOROFI, UKALI SI DAWA!

Watu wanatambua kwamba mwanaume ndiye kichwa cha nyumba, lakini hilo lisiwe kigezo cha wewe kuwa mkorofi na mjeuri hata kwa mambo mengine yasiyo ya msingi.
Mwanamke anahitaji mwanaume mwenye msimamo, asiyeyumbishwa, lakini pia anatamani sana kusikilizwa mawazo yake. Mwanamke anahitaji kuliwazwa na mpenzi wake.
Ukali kupindukia hupunguza mapenzi na hujenga woga na hofu. Wakati mwingine hushindwa kukushirikisha katika mawazo yake mazuri ambayo yangeweza kujenga kwa kuhofia ukali wako.
Ni vizuri kuwa makini katika hili, huna sababu ya kuwa mkali kwa mpenzi wako. Mwanamke ni mtu wa kuelewa, kama kuna mahali amekosea, zungumza naye taratibu huku upendo wa kweli, utii na utu ukionekana usoni mwako na hata kinywani mwako.

UMAPEPE

Kuna baadhi ya wanaume wana tabia ya umapepe, nikisema hivyo naamini naeleweka. Hili ni tatizo lingine wasilopenda wanawake. Siyo wanawake pekee bali hakuna mtu atakayejisikia vizuri mpenzi wake kuwa na tabia ya umalaya. Kila mmoja anapenda kuwa na penzi la peke yake na siyo la kuchangia!
Ikiwa una tabia za kupenda kubadilisha wanawake kila wakati, tarajia kuachana nao kila siku. Lazima mwanaume uwe na staha, mapenzi ya kweli na mtulivu kwa mwenzio.
Naomba nieleweke kitu kimoja hapa, wakati mwingine hata tabia zako za ajabu ajabu, zinamkosesha raha mpenzi wako na fikra za kuachana na wewe zikizidi kuusumbua ubongo wake.
Epuka tabia ya kusifia wanawake wengine vijiweni au ukiwa na mpenzi wako katika matembezi. Unapaswa kujiheshimu. Heshima unayoionesha kwa mpenzi wako ni kithibitisho tosha kwamba unampenda na kuheshimu uwepo wake.

MPE KIPAUMBELE

Mwanamke mwenye mapenzi ya kweli kwako, lazima atatamani kujua mambo mengi kuhusu wewe, lakini kubwa zaidi ni uwazi kuhusu maisha yake pamoja na kutoa ushauri kwako pale utakapohitajika.
Anapenda kuona ukimpa nafasi ya kwanza katika maisha yako, uwe wazi kwa kila kitu kinachoendelea katika maisha yako. Nafasi ya kwanza ninayoizungumzia hapa ni pamoja na kuwa naye karibu na kumpa taarifa za mipango yako ijayo, lakini katika hilo, pia, mwanamke anapenda kuona unaitambua thamani yake na kuyashika maisha yake ipasavyo.
Mwanamke akiona hapewi kipaumbele na mpenzi wake, hupoteza imani ya kuwa na mwanaume huyo. Kama una tabia hizi, ndugu yangu achana nazo, vinginevyo kila siku utaishia kubadilisha wanawake kama nguo.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment