HII ni nafasi ya kuongeza ufahamu katika uhusiano, kona hii ipo kwa ajili ya kuwaelekeza wale wasiofahamu na kuwakumbusha waliosahau kwa vile sisi wanadamu tuna upungufu mkubwa, hivyo kukumbushana ni wajibu wetu. Kutokana na muda wangu mfupi wa kukaa chini ya jua, nimegundua mambo mengi kwenye uhusiano wa kimapenzi huwa yanafanyika kwa pupa bila kujua upande wa pili upo vipi.
Unapoanzisha uhusiano na mtu ni kosa kuzama mzimamzima bila kujua kama unayemkabidhi moyo wako yupo tayari kuupokea na kuutunza. Wengi huwa hawaliangalii hili, kwani ni sawa na kukuta gari kituoni bila kuangalia linakwenda wapi, wewe unapanda kwa vile tu umelikuta kituoni.
Unapokutana na mtu siku ya kwanza bila kujua yupo vipi na ana historia gani, wewe unaingia kichwakichwa, hilo huwa ni kosa kubwa. Penzi la aina hii mara nyingi huwa na mateso kwa vile hujui kabla yako alikuwa na wangapi.
Katika dunia ya leo, kuna wachache wanaosema kweli kuwa wapo katika uhusiano lakini wengine huficha ili kukidhi haja zao za mwili na mwisho wa siku mateso yanawapata.
Watu wengi hushangaa kwa nini mwanzo wa mapenzi huwa motomoto lakini siku zinavyokwenda penzi linapoteza mwelekeo.
Kwa nini?
Kama nilivyosema, ni makosa kumkabidhi mtu moyo wako bila kujua kama yupo tayari kuupokea na kuutunza. Uhusiano mwingi wa sasa huwa ndani ya uhusiano mwingine.
Uhusiano ndani ya uhusiano
Asilimia kubwa ya watu wanaoanzisha uhusiano, huwa tayari wamo ndani ya uhusiano mwingine lakini wanakuwa wasiri sana kuwaeleza wenzi wao kuhusu suala hilo.
Kwa vile penzi haligawanyiki, lazima mwenye mali akigundua au kushtuka na kumdhibiti, hapo ndipo mateso yanapoanza, ukipiga simu haipokelewi au inakatwa na akipokea anakuwa na sababu kibao.
Kwa vile umezama bila kujua kiini chake, unakuwa ukiteseka kwa vile uliingiza kichwa na miguu bila kujua kwamba uliyemkabidhi moyo wako siyo.
Kila kiumbe kina haki ya kupenda lakini kiumbe hichohicho pia kinahitaji upendo wa upande wa pili.
Unapompenda mtu, usikurupuke, tumia muda wako kufanya uchunguzi kujua historia, pia chunguza upendo wake ni wa tamaa ya mwili wako au fedha zako.
Pia hata ukianzisha uhusiano, bado hutakiwi kumuamini mpenzi wako kwa asilimia mia, mpaka upate uhakika kama ni wewe peke yako ambaye upo moyoni mwake.
Siku zote aliye tayari kuupokea moyo wako huwa makini wakati wote kuhakikisha hauumizi. Yote haya yanataka utulivu wa hali ya juu wa kuzuia hisia zako zinapopenda kwa kasi.
Usitafute mateso ya kujitakia kwa kupanda gari la mapenzi usilojua linakoelekea, maumivu ya mateso ya moyo hayana msaidizi zaidi ya kuumia wewe mwenyewe, hivyo kuwa makini kabla ya kuanzisha uhusiano ambapo utamkabidhi mtu moyo wako akutunzie.
Saturday, March 17, 2012
Usipande basi la mapenzi usilojua mwelekeo wake
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment