KATIKA maisha yetu bila shaka tuna watu wengi au wachache ambao toka  moyoni mwetu tunawachukia na pengine tamaa yetu ni kuona wanapatwa na  mabaya kila siku. Miongoni mwao ni watoto, wazazi,waume, wake na  ndugu  zetu.
Pamoja na kuwepo kwa chuki ya asili ambayo nayo hufanya  kazi kwenye maisha ya mwanadamu, lakini wengi wetu tuna chuki  zinazotokana na orodha ya mabaya tuliyowahesabia wenzetu.
Mume  anaweza kuwa na orodha ndefu ya matendo machafu ya mkewe tangu  walipooana miaka saba iliyopita, ambapo kila siku anapomtazama tu huwa  kama anatazama CD ya matukio yaliyopita na kuifanya chuki yake kukuwa  kila siku.
Kwa bahati mbaya, wanadamu wengi wako hai kwenye  mabaya, uwezo wao wa kukumbuka makosa ni mkubwa zaidi kuliko wema  wanaofanyiwa.  Tabia hii inatokana na ukweli kwamba, akili zina tabia ya  kukosoa muonekano na taarifa ya vitu, lengo ni kuweka ulinganifu wa  jinsi mtu anavyojitambua.
Kwa mfano msichana akijitambua mwenyewe  kwamba yeye ni mzuri, mtazamo wake kuhusu wanaume utakuwa ni wa  kuwalinganisha na jinsi alivyo na wakati wote atapenda kuona anaokutana  nao mtaani wawe kama yeye, vinginevyo atawachukia.
Bila shaka  uchunguzi umebaini kuwa msingi wa chuki zetu ni ubinafsi wetu. Wanadamu  ni wabinafsi kwenye mali zao, mafanikio yao, uwezo, matakwa na muonekana  wao.
Kwa kutambua hilo, kinachotujengea chuki juu ya wenzetu ni  ‘USISI’ ambao kila mtu anao. Wako wenye usisi wa udini, ukabila, rangi,  jinsia, uwezo, elimu na tabia. Hali hii ndiyo inayowafanya wawaone  wenzao kama wakosaji.
Unamchukia mumeo kwa sababu unataka awe  kama unavyopenda, hupendani na mfanyakazi mwenzako, jirani yako, mke  mwenzako kwa vile unajenga msukumo wa usisi kwenye mtazamo wako juu  yake.
Ifahamike kwamba msingi huu wa maisha ni hatari kwa vile  umekuwa mzigo mzito kwenye maisha ya wanadamu wengi. Watu wengi wamepata  matatizo makubwa kwenye maisha yao kwa sababu walishindwa kujigundua  kuwa wana usisi na hivyo kulazimisha ulimwengu ufanye watakavyo, jambo  ambalo ni gumu.
Ni ukweli ulio wazi kwamba, hatuwezi kuishi  kwenye mtazamo wa kutaka mapenzi yetu yatimizwe na kuwa na msukomo wa  lazima wa kuifanya jamii inayotuzunguka itumikie mtazamo wetu. Kamwe  hatuwezi kuwafanya wenzetu, watembee, waongee, wawe na tabia kama zetu.
Hii  ina maana kwamba kama tulikwenda kwa mtu kutaka mkopo tukanyimwa,  tulitaka msaada tukakosa, tuliomba heshima, tulitarajia chochote kwa  wenzetu hatukupewa sawa na mahitaji, jawabu letu lisiwe chuki kwa vile  haitusaidii kujengea usisi wetu.
Wajibu wetu mkuu kwenye maisha  ni kujitambua na kuacha wengine nao watumikie kujitambua kwao kama  binadamu. Tusiingie kwenye uhasama wa bure kushindania mtazamo.  Tukumbuke mpaka tunaondoka duniani hali ya kila mmoja kujitambua  mwenyewe haitafutika.
Mama Theresa aliacha neno la msingi kwenye  maisha yetu lisemalo: “If you judge people, you have no time to love  them.” Kama utakuwa mwenye kuhukumu wengine hutakuwa na muda wa  kuwapenda Ni vema tusiwe wepesi wa kuhukumu badala yake tukubali  ubinadamu wa wenzetu katika maisha.
Saturday, March 17, 2012
Kwa Nini Wanadamu Huchukiana?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment