TUNAPENDA kuongozwa na fikra zetu. Kila mmoja anataka muongozo wa maisha yake uendane na halmashauri ya ubongo wake. Hufanya hivyo, bila kujua kuwa kuna kikomo fulani ndani yake. Akili na matakwa ya moyo, wakati mwingine vinaweza kukupoteza.
Moyo unaweza kumpenda mchawi na ukawa huelewi kitu kwa chochote utakachoambiwa. Penzi la jambazi likikuingia, serikali ndiyo utaiona ni katili kwa sababu inamsaka mwenzi wako usiku na mchana. Hii ina maana kuwa mapenzi ni zaidi ya fikra za kila mtu.
Hutokea watu kuachana wakati bado wanapendana. Migogoro midogo inawafanya watengane, matokeo yake kila mmoja anabaki akiumia kivyake. Huo ni mfano mmoja kati ya mingi inayoonesha kwamba mapenzi yapo juu ya fikra za kawaida. Inahitaji utulivu wenye mashiko ya sayansi ya saikolojia.
Kuna ambao waliishi kwa mategemeo ya kuachana. Wakiamini wamechokana, matokeo yake kwenye ubongo wao wakatengeneza maneno: “Ipo siku.” Hata hivyo, miezi na miaka ikakatika mpaka wakazikana. Kumbe Mungu aliwaandikia wawe pamoja mpaka kifo ila wao hawakujua.
Dosari ya aina hiyo inatokana na wawili wanaopendana lakini upendo wao ukapofushwa na migogoro ya hapa na pale. Nasisitiza kuwa watu ni lazima wagundue mapema matatizo yao kabla ya kuhisi kwamba kati yao hakuna mapenzi. Vilevile, kila mmoja amuelewe mwenzi wake ni binadamu na siyo malaika.
Ana mapenzi naye, tena mapenzi makubwa. Hata hivyo, hiyo haimfanyi awe malaika. Ni binadamu, kwa hiyo wakati anadumisha mapenzi yake, anaweza kufanya makosa mengi. Jaribu kumvumilia kwa sababu ameumbwa na udhaifu, hajakamilika.
Baada ya utangulizi huo, ni vizuri kujua kuwa yapo makosa ambayo wengi huyafanya, tena mara nyingi ni bila kujua. Tunaishi nayo, matokeo yanakuwa ni mazoea. Hata hivyo, mara nyingi hutokea yanaharibu uhusiano ndiyo maana nimechagua tuyajadili. Yafuatayo ndiyo makosa yenyewe:
KULICHEZEA KAMARI PENZI LAKO NA MAISHA YAKO
Hapo ulipo hujawahi kuona mtu anapambana kuhakikisha mwenzi wake anabadilika tabia? Bila shaka tayari ulishajionea. Je, umejifunza nini kutoka kwao? Ni kweli kabisa kwamba mwenzi wako si malaika, kwa hiyo mnapokutana lazima mtatofautiana. Je, ikitokea hamuendani kabisa?
Umejitahidi kumuweka kwenye mstari unaotaka lakini mwenzako haendi. Unasubiri nini? Kung’ang’ania penzi la mtu ambaye huendani naye, ni sawa na kuuchezea kamari moyo wako, vilevile ni sawa na kuyachezea karata tatu maisha yako.
Upo na mwenzi wako ambaye hakutoshelezi. Mnakutana mara nyingi lakini hakufikishi pale unapotaka upelekwe na mwandani wako. Unanyamaza tu kwa imani kuwa ipo siku ataweza, siku zinakwenda na mabadiliko hayaonekani. Unajipa matumaini kedekede kwamba kuna siku nyoka ataota miguu na jongoo atakuwa na macho.
Unakuwa na mpenzi ambaye kila siku anakupa visingizio ili msikutane faragha. Je, kwa nini usijiongeze kwamba mtu huyo hana hisia na wewe? Au, kwa nini usijiulize kama pengine mtu wako yupo kwenye uhusiano wa pembeni ambako anatoshelezewa mahitaji yake?
Tatizo kubwa ambalo linatakiwa lijulikane ni kwamba wengi wanapoingia kwenye uhusiano, hawapimi watu wao ni wazuri kwao kiasi gani. Wanavutwa na matamanio ya juu. Mvuto wa juu, huipumbaza akili na kudhani moyo unapenda kumbe ni uongo mtupu.
Mtu anaweza kudumu na mwenzi wake ambaye hamtoshelezi kwa miaka mingi. Anapumbazwa na mvuto wa juu, kwa hiyo anashindwa kuelewa mantiki ya muungano wa nyoyo. Zingatia kwamba mwenzi wako ambaye nyoyo zenu zimeungana, lazima atakuridhisha, naye ataridhika kwa huduma unayompa.
MFANO: Jayden Brown anatoa ushuhuda: “Nikifikiria uhusiano wangu uliopita nabaki najishangaa. Nilikuwa mbinafsi, nilikuwa naoneshwa upendo na wapenzi wangu lakini nilikuwa sitoi ukilinganisha na wao. Nilishangazwa na wanawake waliojitoa kwangu, wao waliamini kuna siku ningebadilika.
“Wanawake niliokuwa nao, walijipa matumaini kuwa ni muda tu, kipo kipindi ambacho kingefika na maisha yetu yangekuwa salama. Kumbe walichowaza wao, hakikuwa ndani ya akili yangu.
“Wao waliamini kwamba upo muda wa mabadiliko ya mimi kuwa mtu bora, ningebadilika kuwa mwema kwenye mapenzi, ningekuwa mpenzi bora. Kitu mapenzi juu yao hakikuwa ndani yangu kabisa.”
KUZIDIWA NA HISIA MAPEMA
Jambo lingine ambalo ni hatari kubwa ni kuzidiwa na hisia mapema. Hakuna anayeweza kupinga ukweli kuwa mapenzi ni mchezo wa hisia, kwa hiyo siyo kosa kuzionesha kwa mtu ambaye umempenda. Tatizo ni wakati wa kuzionesha. Haifai kuzidiwa mwanzoni mwa uhusiano.
Ikae akilini kwako kuwa maisha ya sasa, mpaka unakuja kukutana na mwenzi wako, utakuwa umeshapita kwa wengine, naye ni hivyohivyo, kwa hiyo kila mmoja anajua matarajio ya mapenzi. Kitendo cha kuzidiwa na hisia huamsha hali fulani ya usumbufu kwa mwingine.
Nitoe msisitizo kuwa watu wazuri kwenye mapenzi ni wachache lakini wanatolewa macho na wengi. Kwa kulitambua hilo, unapaswa kuishi kwa akili ili usigeuke kero. Endapo atakuona msumbufu, hatasita kumkaribisha yule ambaye anamuona atampa furaha badala ya karaha.
Lazima atakuwa na uzoefu wa kimapenzi, bila shaka anaujua utulivu katika uhusiano. Kama ndivyo, unadhani atakubali kupoteza muda kwako, wakati kila siku unachemsha kichwa chake kwa maswali au vitendo ambavyo chanzo chake ni kuzidiwa na hisia za mapenzi juu yake.
Ieleweke kuwa hisia hutokana na ukweli wa mapenzi. Yaani, unapozidiwa na hisia, maana yake moyo wako haudanganyi. Unapenda kupitiliza, kwa hiyo unakuwa unahitaji na mwenzako naye akutendee haki. Ni hapo ndipo usumbufu huibuka. Upendo kugeuka kero kwa anayependwa.
Mapenzi siyo maneno, vitendo ndiyo hutafsiri upendo. Vema ukatia akilini kuwa kama kweli unampenda, utamsaidia pia kupata utulivu. Wewe ndiye utamfanya awe na utulivu, endapo hutampa usumbufu wa hapa na pale. Inahitaji busara kidogo kulitambua hilo, kwani wengi wamefeli.
Mara nyingi mtu anayezidiwa na hisia, hushindwa kujidhibiti. Mwenzi wake akichelewa kujibu SMS, hugeuka tatizo kubwa linalohitaji suluhu ya mtu wa tatu. Akimpigia simu, ikaita mara saba bila kupokelewa, akipokea tu shari. Kabla ya salamu ni swali: “Mbona hupokei simu?”
Katikati ya mazungumzo, kama upande wa pili utaonekana kuna utulivu, shari inaanza: “Mbona upo sehemu iliyotulia hivyo? Upo wapi?” Kwa akili ya haraka, inamtuma mwenzi wake yupo nyumba ya kulala wageni, hoteli au sehemu yoyote akishiriki tendo la faragha na mtu mwingine.
Hisia mara nyingi hudanganya, kwani huzalisha mawazo mabaya na matokeo yake ni karaha ndani ya uhusiano. Hakuna anayeweza kuvumilia tuhuma za kila mara. Mapenzi maana yake ni amani na furaha, wewe hiyo amani humpi, furaha ndiyo hana kabisa. Lazima atakukimbia au atakuumiza zaidi kwa sababu anaweza kutafuta mlango wa kutokea wakati hujajiandaa kuachwa.
KUSHINDWA KUSOMA ALAMA
Zipo alama muhimu ambazo ni vema kuzijua na uzibaini kwa mwenzi wako kabla hujazama kwenye dimbwi la mapenzi. Bahati mbaya wengi hutawaliwa na papara, matokeo yake hushindwa kubaini vitu ambavyo vinaweza kumfanya apate uelekeo wa uhusiano wake.
Katika pointi hii, nashauri watu kwenda kwa mwendo wa kinyonga badala ya kupiga mbizi bila kujua kina cha maji. Kusoma alama muhimu kwa mwenzi wako mapema ni sawa na kutegua kitendawili. Itakusaidia kujua kama kweli uliyenaye ana mapenzi ya kweli au anaweza kuwa laghai.
Wengi wanapoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi hueleza kuwa wanapenda, tena huweka wazi kuwa hisia zimeanguka kwa wale wanaowapenda. Hata hivyo, huacha mambo mengi ndani ya uvungu wa nyoyo zao. Wewe utakuwa mshindi, endapo utaweza kumsoma mwenzi wako na kumuelewa kinagaubaga.
Pointi hapa ni kuwa mwanzo kabisa wa uhusiano, yapo mambo mengi ambayo kila mmoja hujitahidi kuyazungumza. Hiyo huita kujiweka wazi lakini imethibitika kitaalam kwamba maelezo ambayo hutolewa ni asilimia 40 tu, zilizobaki hufichwa. Asilimia 60 zilizobaki utazifichua kwa kusoma alama muhimu.
Nyongeza ni kwamba mara nyingi wengi hujitahidi kusema uongo mwanzoni mwa uhusiano. Hata kama mtu anapenda lakini hudanganya hili na lile pengine kwa hofu, tahadhari au kama pointi ya kushinda penzi. Mantiki hapa ni kukutaka uwe makini na umsome mwenzako kwa undani kabisa
Katika kipengele cha kusoma alama muhimu, kuna vitu vya msingi vya kuzingatia ambavyo ni hivi vifuatavyo;
1) Jamii: Mwenzi wako anasimama vipi na jamii yake? Usiingie kichwakichwa kwenye mapenzi na mtu ambaye hata jamii yake inamuona ni tatizo. Vilevile, yule ambaye ni muoga inabidi uanze kumtilia wasiwasi mapema. Ni kwa ajili ya maisha yako, hivyo ni vema kuchangamka.
Hutakiwi kugundua muda umeshapita kuwa mwenzi ana tabia usizopenda. Mapema msome na umuelewe. Chunguza msimamo wake kwenye jamii, anavyojiamini, je, anaonesha kuwa na dira ya maisha? Kama hana uelekeo, unatakiwa kuachana naye haraka.
2) Hisia: Zisome hisia zake, je ni mtu anayejali? Unatakiwa kujua kama hisia zake zipo karibu kwa kiasi gani. Atakapotakiwa kukutimizia haki yako ya faragha, atakuwa tayari kwa wakati? Ni aibu mmeshakuwa na uhusiano kwa muda mrefu ndiyo unaanza kulalamika kwamba mwenzi wako hakutimizii huduma ya uwanja wa wawili.
Lingine kwenye hisia, unatakiwa ujifunze kujua kama mwenzi wako ni mtu wa kulipuka au kinyume chake. Inawezekana ni kweli mwenzi wako anakupenda lakini akawa ni mtu wa jazba, tatizo dogo ‘anapaniki’ utadhani nyoka aina swila, kakanyagwa mkia. Mjue halafu umpime, je, unaweza kumvumilia? Jiridhishe mara mbili, vinginevyo bwaga manyanga.
3) Muonekano: Ni kipengele kidogo muhimu ndani ya kifungu cha kushindwa kusoma alama kama sehemu mojawapo inayowafanya wengi kufanya makosa kwenye uhusiano. Muonekano si suala la baadaye, inatakiwa mapema sana umtathmini halafu ujiridhishe kama anakufaa au kinyume chake.
Ni aibu umeshaingia kwenye uhusiano, halafu baadaye unamsaliti mwenzi wako na kuanza kuwatolea macho wale ambao unaona ni wazuri zaidi. Hakikisha kwamba mwanzo kabisa kwenye uhusiano wako, unajiridhisha kuwa anao mvuto unaokutosha. Kama hakuvutii achana naye mapema, usimpotezee muda wake.
Muda wako pia ni mali, kwa hiyo hilo pia litazame kwa umakini kwa sababu inawezekana ukachukulia ni jambo dogo leo, ukaanza naye uhusiano kwa kujifurahisha lakini mbele ya safari utakapotaka kuamua, ikakugharimu kwa maana pengine wakati wewe unawaza kutoka, mwenzako ndiyo kwanza anaongeza gia.
4) Kipimo cha mapenzi: Hiki ni kipengele nyeti. Kina maana kubwa, kwa hiyo hupaswi kudanganyika kwa namna yoyote ile. Hakikisha upendo wake kwako upo wazi. Wengi hushindwa kulifanyia kazi mapema, matokeo yake hubaki wakijuta baadaye. Chukua angalizo hili, kwa hiyo kama haoneshi upendo wa kweli, vema umuache aende.
Je, anaonesha yupo tayari kwa ujenzi wa uhusiano imara? Yupo wazi kwako na anapenda kila mtu ajue kwamba yeye ni wako? Alama hizo ndizo ambazo zinaweza kukupa muongozo unaojitosheleza. Kama upendo wake ni wa wasiwasi, nawe mkatae haraka. Wekeza upendo kwenye upendo, vinginevyo wewe utampenda lakini mwenzako atakudharau.
KUAMUA UHUSIKA WAKE KWENYE UHUSIANO
Ni rahisi kuamua jinsi ambavyo wewe unavyoweza kuhusika kwenye uhusiano wako lakini si yeye. Kufanya hivyo ni sawa na kuingia kwenye moyo wa mwingine, kitu ambacho hakiwezekani hata kiduchu. Kaa ukijua kwamba nafsi ya kwanza itabaki kuwa ya kwanza na ya pili itaendelea kusimama katika uhalisia wake.
Maisha ni kama picha ambayo unaijenga kwenye fikra zako. Endapo utawaza mema na kutamani kumfanyia mwenzi wako vitu vizuri, ni rahisi kutekeleza. Utakosea mno, kama utakuwa unasumbuliwa na mawazo kwamba unachokitenda, mpenzi wako naye atakaa na kufikiria kisha akutendee kama unavyomfanyia.
Kwa miaka kadhaa, nimejifunza kujua tabia za watu kwenye mapenzi na kubwa ambalo nimebaini ni kwamba saikolojia ya ndani ndiyo ambayo inaleta utata. Uhusiano wa wengi unashindwa kudumu kwa sababu hiyo. Ukweli ni kwamba ndani ya mtu, kunakuwa na matarajio ambayo hayafikiriwi upande wa pili.
Hili ni tatizo lakini linaweza kuwa kinyume chake kama mhusika ataligundua hilo na kulitafutia ufumbuzi. Kwa nini uwaze peke yako? Iweje kichwa kiume kwa tamaa ya kutekelezewa jambo ambalo linaweza kuingizwa kwenye majadiliano? Mapenzi ni kitu kinachokutanisha nafsi mbili zenye hisia tofauti, kwa hiyo inabidi kuelewana ili muende sawa.
Acha kuwaza peke yako. Mshirikishe mwenzako jinsi ambavyo wewe ungefurahi kwa namna atakavyohusika kwenye mapenzi yenu. Muelekeze cha kufanya. Mshauri muonekano ambao wewe utakupa nguvu ya kujiamini kwamba upo kwenye uhusiano salama. Usipojadiliana naye, unadhani utasaidiwa na nani?
Kosa kubwa ambalo watu wengi huwa wanafanya ni kuwaacha wapenzi wao na kwenda kujadiliana na marafiki. Mtu anaweza kuketi na rafiki yake na kumwagia lawama chungu nzima jinsi asivyofurahishwa na mwenzi wake, wakati angezungumza na mhusika mafanikio yangeonekana kwa urahisi zaidi.
Achana na tabia ya kumsengenya mwenzi wako kwa marafiki zako. Unamponda kwa yale anayofanya kwa kuona hayapo sawa lakini mapenzi hayapo hivyo. Tambua kwamba wewe pekee ndiye mwenye nafasi ya kumfanya mpenzi wako abadilike kulingana na jinsi unavyotaka. Jijengee mawazo chanya kuanzia leo.
Binadamu walivyo katika jinsi mbili tofauti, ndivyo wanavyotofautishwa na namna ya kupenda pia jinsi ya kuhusika kwenye mapenzi. Wengi huishi na maumivu kwa kuona kwamba anachowaza, hakipo kwa mwenzi wake.
KUKOSEA TAFSIRI
Binadamu kila mmoja kwa namna yake, anayo njia ya kuonesha ishara za mapenzi. Hata hivyo, ipo wazi kuwa wengi hufanana pale wanapochachawa kutokana na kuzidiwa na hisia za kupenda. Kila mmoja anaruhusiwa kupenda lakini pupa zikikuzidi, ni rahisi kuonekana mapepe. Haipendezi kuonekana hivyo.
Ieleweke kuwa ipo jamii ya watu ambao wanaweza kupenda lakini wasioonesha waziwazi hisia zao. Wakakomaa kisabuni, wewe ukadhani hawapendi kumbe wanaumia ndani ya nyoyo zao. Hili likae kichwani kwako, usije ukafanya kosa kubwa la kukosea tafsiri, matokeo yake uhusiano wako ukakaa tenge.
Tambua pia kuwa ipo jamii ambayo inaweza kuonesha waziwazi kwamba wanapenda kumbe hakuna lolote. Ni uchangamfu tu uliopo ndani yao. Anaweza akawa anakujali, ukiwa mbali anakupigia simu. Ukiwa na tatizo anajitoa kukusaidia lakini hiyo haina ishara kuwa anakuhitaji kimapenzi. Ni mambo ya urafiki tu hayo.
Hivyo basi, kabla hujaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, hakikisha huchanganyi mambo. Usimtafsiri mtu kwa alama za juujuu. Fanyia kazi kile unachohisi. Usije ukachukia kwamba mtu unayempenda anakuchukia, wakati kumbe mwenzako ndiyo swaga zake. Lazima aweke madoido kidogo kwa kuhofia kuonekana mwepesi.
Wala usije ukadandia mti ambao siyo kwa kudhani unapendwa, wakati mwenzako ni geresha tu! Chukua hatua sahihi, kabidhi moyo wako kwa yule anayekupenda, si kwa sababu akikuona anakuchekea na kujishaua, la hasha! Kaa kwa yule ambaye amedhihirisha mapenzi ya kweli kwako. Ukikosea tafsiri, utaumia mbele ya safari.
Saturday, March 17, 2012
Makosa makubwa ambayo wengi huyafanya katika mapenzi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment