Katika maisha ya kimapenzi hakuna kitu kinachouma  kama kusalitiwa, tena kusalitiwa kunakouma zaidi ni pale unapobaini  mpenzi wako kampa penzi mtu unayemjua halafu ukijilinganisha wewe na  huyo aliyepewa unashindwa kuelewa kilichomshawishi mpenzi wako.
Lakini  licha ya kwamba usaliti si kitu kizuri, watu wamekuwa wakisalitiana,  tena sana tu. Inafika wakati unashindwa kuamini kama yupo mtu ambaye  hajawahi kumsaliti mpenzi wake.
Niseme tu kwamba wapo wachache  waliotulia ila asilimia kubwa ya walio kwenye uhusiano ni wasaliti hata  tafiti zimethibitisha hilo. Kama hali yenyewe iko hivyo, cha kujiuliza  ni kwamba unapobaini mpenzi wako kakusaliti ni kipi unachotakiwa  kufanya? Je, ni kuamua kunywa sumu kama ambavyo wamekuwa wakifanya  wengine? Sidhani kama huo ni uamuzi sahihi. 
Mtaalam wa masuala ya  mapenzi James Johnson kutoka Marekani amependekeza mambo 10 unayoweza  kufanya baada ya kubaini kuwa mpenzi wako amekusaliti.
1. Kubaliana na kilichotokea
Kama  kishakusaliti ni tukio ambao limeshatokea na haliwezi kufutika. Kubali  kuwa umetendwa, huzunika lakini mwisho liache lipite ili uweze kujipanga  upya.
2. Usijilaumu
Wapo ambao wakishasalitiwa hujuta  kukubali kuingia kwenye uhusiano na watu waliowatenda. Utamsikia mtu  akisema ‘najuta kumkubalia awe mpenzi wangu’. Kujilaumu kwa namna hiyo  hukutakiwi kwani kutakufanya uzidi kunyong’onyea.
3. Jitoe
Jifanye  kama vile aliyesalitiwa siyo wewe bali ni rafiki yako kisha jiulize  ungemshaurije? Ushauri ambao ungempata basi uchukue kisha uufanyie kazi.
4. Pima ulivyoathirika
Je,  kitendo cha mpenzi wako kukusaliti kimekukosesha imani juu yake? Kama  ni hivyo, unadhani una sababu ya kuendelea kuwa naye au unahisi madhara  aliyokupatia huwezi kumvumilia?
5. Mpasulie ukweli
Kwa  vyovyote utakavyoamua ni lazima umweleze juu namna alivyokuumiza kwa  usaliti wake. Hata kama utampa nafasi nyingine lazima ajue jinsi  alivyokuumiza ili iwe changamoto kwake.
6. Chunguza kwa nini kakusaliti
Usiliache  likapita hivi hivi, unatakiwa kujua sababu ya yeye kukusaliti. Je, kuna  ambacho anakikosa kwako au ni tamaa zake tu? Jibu utakalolipata  litakusaidia katika maisha yako ya kimapenzi.  
7. Usikubali akulainishe
Huenda  huyo mpenzi wako ni ‘msanii’ na anaweza kukulainisha kwa maneno ambayo  yanaweza kukufanya ukalichukulia tukio hilo kiurahisi. Kuwa na msimamo  na eleza hisia zako kwa uwazi.
8. Amua kusuka au kunyoa
Likishatokea  hilo jaribu kuzungumza na moyo wako. Uamuzi wa kuendelea kuwa naye au  kumuacha uuchukue bila shinikizo. Hata kama kakuumiza, kama unadhani  unaweza kumpa nafasi nyingine mpe ili usije ukajuta baadaye kwa kumkosa  lakini kama unaona moyo wako unamkataa, muache.
9. Msamehe
Kwa  uamuzi wowote utakaochukua ni lazima uwe tayari kumsamehe ili kuliondoa  dukuduku lako rohoni. Kutokumsamehe kunaweza kukufanya ukawa unaumia  kila wakati na kukosa amani.
10. Iwe fundisho kwako
Chukulia  tukio hilo kama fundisho kwako. Huenda wewe ndiye uliyechangia  kusalitiwa, kama ni hivyo badilika ili yasije yakakukuta kama hayo  utakapokuwa na mwingine. Pia kama kusalitiwa kumetokana na kutoridhika  kwa mpenzi wako, kuwa makini wakati wa kuchagua mwingine wa kuwa naye.
Saturday, March 17, 2012
Mambo 10 ya kufanya baada ya kusalitiwa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment