Saturday, March 17, 2012

Khanga moja nyumba ya kupanga? Unaitaka ndoa yako?

NI wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii nikiamini muwazima na mlikuwa na wakati mzuri sasa katika kusherehekea Siku ya Wapendanao.
Sitaki kufikiria jinsi ‘mlivyoinjoi’ siku hiyo lakini naamini mlipata fursa ya kudhihirishiana kuwa kweli mnapendana na mapenzi yenu yanatoka mioyoni mwenu.
Baada ya kusema hayo sasa nirudi katika kile nilichodhamiria kukiandika wiki hii. Nazungumzia tabia ya baadhi ya wake za watu hasa wale wanaoishi nyumba za kupanga kujiweka katika mazingira ya kuzibughudhi ndoa zao.
Matukio ya flani kutembea na mke wa mpangaji mwenzake yamekuwa yakisikika mara kwa mara na ukijaribu kufuatilia utabaini kuwa, wapo wanaume ambao wamekuwa wakijikuta wanawatokea wake za watu kutokana na vishawishi wanavyopata.
Siyo kwamba nafagilia wanaume wanaowatokea wake wa wenzao kwa kuwa tu wamepata vichocheo, hapana! Nazungumzia hizi tabia mbaya wanazokuwa nazo baadhi ya wanawake za kuwatega wenzao kwa mavazi, kwa makusudi au bila kujua.
Kuna hili vazi la khanga moja ambalo baadhi ya wanawake hupendelea kulivaa hasa wanapokuwa chumbani na wapenzi wao. Kulivaa huko ni sahihi kabisa kwani unapokuwa na mtu wako faragha huchaguliwi cha kuvaa, hata usipovaa chochote sawa tu lakini ishu ni pale unapokuwa nje ya chumba au nyumba unayoishi.
Wapo wake za watu ambao ni wa ajabu sana na hili nitalizungumza kwa kurejea tukio moja lilitokea juzikati maeneo ya Sinza, Dar. Kuna mama mmoja anaitwa mama Frank, yeye amejaaliwa kuwa na makalio makubwa.
Mama huyo ameolewa na mume wake anajiheshimu sana lakini kitu ambacho wamekuwa wakikorofishana mara kwa mara ni tabia ya mwanamke huyu kupenda kuvaa nguo za kihasara.
Mara kavaa taiti na kitopu kisha anatulia kibarazani, mara kavaa khanga moja kisha anakatiza kwenye korido kwa staili ya ‘hamsini… hamsini… mia…’ yaani kwa raha zake.
Juzikati saa tatu usiku mama huyo alitoka akiwa na khanga moja kwenda kuoga bafu la nje ambalo liko mbali kidogo.
Wakati anatoka mlangoni, mwanamke huyo akakutana na kijana wa kiume mlevi, naye alikuwa anaelekea chooni. Yule kijana kutokana na jinsi yule mama alivyokuwa akitingisha, uvumilivu ukamshinda, akamvaa na kutaka kumbaka. Majirani ndiyo waliozuia tukio hilo la ubakaji lakini baadhi ya wapangaji walimsema mtu mzima huyo kutokana na staili yake ya uvaaji.
Ninachotaka kukisema kupitia tukio hilo ni kwamba, mke wa mtu hasa wewe unayeishi nyumba ya kupanga huna sababu ya kuvaa khanga moja unapokuwa nje ya chumba chako unacholala. Hata ‘sitting room’ siyo sahihi kabisa labda kama umekaa na mumeo na mlango umefungwa.
Nasema hivyo kwa kuwa, kuvaa hivyo kunakufanya utafsiriwe tofauti. Hebu jiulize kuna sababu gani ya kuwaonesha wanaume wengine jinsi ulivyoumbika? Ili iweje sasa? Wakutongoze halafu iweje?
Jamani kujiheshimu ni pamoja na kuchagua unavaa nini ukiwa wapi. Kitendo cha wewe kwenda kuoga bafu la nje ukiwa umevaa kanga moja na kukatiza mbele za wanaume kwanza unaonesha kutokujijali lakini pia unajiweka katika mazingira mazuri ya kubakwa.
Ndugu zangu leo nilitaka kulizungumzia hilo, ni kwa kifupi lakini naamini utakuwa umenielewa na kulifanyia kazi ili uweze kuishi maisha yasiyo na migogoro.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment