Katika  ulimwengu wa mapenzi, kila siku watu wanaingia kwenye uhusiano lakini  elewa kwamba siku ambayo wewe unamzimikia mtu flani siku hiyo hiyo wapo  wanaozinguana na kuachana.
Si kwa wapenzi tu, hata kwenye ndoa wapo  ambao leo hii ndiyo wanaoana lakini leo hii hii kuna wanaopeana talaka.  Iko hivyo na kwa maana hiyo suala la kupendana lipo lakini la kuachana  nalo halikwepeki.
Ndiyo maana ukijaribu kufuatilia hata wewe  unayesoma makala haya yawezekana mpaka umefikia hatua uliyonayo  umeshaacha au kuachwa. 
Hilo ndilo limenifanya niandike mada hii. Je,  unajua mbinu sahihi za kumuacha mtu ambaye mlikuwa mkiambiana I love  you, I love you too? Kama jibu ni hapana, leo nitakupa shule inayoweza  kukuongoza katika hilo.
Lakini kabla ya kulizungumzia hilo niseme tu  kwamba miongoni mwa vitu nisivyovipenda katika maisha yangu ni kusikia  flani na flani waliokuwa wanapendana sana hadi kuwa gumzo mtaani  wameachana.
Inaniuma kwa sababu najua ivavyouma. Mara nyingi  anayeachwa anaumia zaidi hasa akiwa hajajiandaa na ndiyo maana wataalamu  wa masuala ya mapenzi wamejaribu kuanisha mbinu ambazo unaweza  kuzitumia katika zoezi zima la kumuacha mpenzi au mume/mke wako hasa  pale zinapokuwepo sababu za msingi zinazoweza kukubalika.
1. Hakikisha umedhamiria
Unatakiwa  uwe umejiandaa kumkosa katika maisha yako. Jadiliana na akili pamoja na  moyo wako kama kweli vimeridhika na uamuzi unaotaka kuchukua. Jiulize  ni kweli amekukosea kiasi kwamba huwezi kuendelea kuwa naye?
2. Usiwe mwenye hasira
Unapotaka  kumuacha mpenzi, mume au mke wako kwa sababu maalum, hakikisha huna  hasira.Tulia ili hata pale utakapokuwa hauko naye usije ukajuta na  kudhani hukuchukua uamuzi sahihi.
3. Muda na siku sahihi
Wataalamu  wa mapenzi wanasema kuwa, muda wa asubuhi siyo mzuri kumuacha mpenzi  wako kwani utampa wakati mgumu siku nzima lakini pia kwa wapenzi  wanaofanya kazi siku za katikati ya wiki siyo siku nzuri.
Siku ya  Ijumaa jioni inapendekezwa kuwa siku nzuri ya kumuacha mpenzi wako kwa  maelezo kwamba ataitumia wikiendi kujiliwaza na hata inapofika Jumatatu,  anakuwa amepoa tayari kwa kuendelea na majukumu yake.
Kama nilivyosema awali, kila siku watu  wanaingia kwenye uhusiano mpya lakini pia wengine wanaachana. Sababu za  kuachana kwa wapenzi zinatofautiana ila kikubwa ni kwamba unapoachana na  mtu ambaye mlikuwa ‘mwili mmoja’ hutakiwi kumgeuza adui yako kwa  asilimia zote, hata kama kakukosea vipi.
Kwa mfano, yawezekana  ulitokea kumpenda na kuhisi angeweza kuwa wako wa maisha lakini kadiri  siku zinavyokwenda unabaini si mtu sahihi kwako. Katika mazingira hayo  suala la kumuacha haliepukiki ila cha kujiuliza ni kwamba utamuachaje?
Je,  itakuwa ni sahihi kumuambia laivu kwamba mimi na wewe basi? Inawezekana  ukafanya hivyo ila wataalam wa mapenzi hawashauri kwani wanajua madhara  ya kutumia mbinu kama hiyo na ndiyo maana wakashauri kutumia njia  ambazo zinaweza kusaidia ukamuacha lakini bila kumuumiza na maisha  yakaendelea kuwepo.
Jitoe taratibu
Chukulia kwamba umekuwa  naye kwa muda mrefu kidogo ukiwa na malengo ya kuingia naye kwenye ndoa  lakini katika utafiti wako ukabaini hakufai, unashauriwa kujitoa kwake  kimyakimya. Unachotakiwa katika mbinu hii ni kupunguza kumtendea mambo  ya kiupendo.
Kwa mfano, unaweza kupunguza kuonana naye, kumpigia  simu, kumtumia sms na hata kumsaidia kifedha kama ulikuwa ukifanya  hivyo. Kwa kufanya hayo ni lazima ataanza kuona tofauti na kuhisi penzi  linaelekea ukingoni.
Aidha, kwa kumfanyia hivyo ni lazima atahoji juu  ya mabadiliko hayo. Wewe hutakiwi kutoa maelezo yoyote zaidi ya  kuendelea kuyeyusha bila kumwambia wazi kwamba umemtoa moyoni mwako.
Kama  huyo mpenzi wako ni mwelewa atagundua kuwa, ndiyo unamuacha kimtindo na  yeye ataanza kujiandaa kukukosa, hata pale utakapokata mawasiliano moja  kwa moja atakuwa ameshajua kuwa umemuacha hata bila kumueleza.
Ukigundua  ameshafahamu kuwa umemuacha, hapo unaweza kumwambia kwa kifupi kwamba  umeamua bora kila mmoja aendelee na maisha yake. Kisaikolojia utakuwa  hujamuumiza sana lakini tayari utakuwa umemuacha.
Maneno ya busara
Unaweza  kumuacha mpenzi wako kwa kutumia lugha ambayo yeye mwenyewe atahisi  hukuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima umuache. Mfano: ‘Ashura, kusema  ukweli nilikupenda sana na mpaka sasa naamini wewe ni mwanamke wa maisha  yangu, sikuamini kama yupo mwanamke mwingine wa kunipa furaha kama wewe  lakini kwa hili lililotokea sina jinsi, inabidi nikuache. Utaendelea  kuwa rafiki yangu na kama ni kukusaidia nitakusaidia kama rafiki na si  mpenzi.”
Hayo ni maneno ambayo mwanaume anamwambia mpenzi wake  akimaanisha anamuacha lakini ukiyachunguza utabaini hayachomi sana kwa  kuwa anayeachwa bado anapewa nafasi nyingine ya urafiki wa karibu na si  mapenzi tena.
Mimi nikushauri tu kwamba, hakikisha unapotaka kuachana  na mtu ambaye mmekuwa pamoja kwa muda mrefu unakuwa makini. Hata kama  amekukosea vipi lakini busara itumike hasa kwa kuzingatia yale mazuri  ambayo aliwahi kukufanyia huko nyuma.
Saturday, March 17, 2012
Mbinu za kumwacha mpenzi wako bila ya kumuumiza
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment