Kugombana ni sehemu ya maisha ya binadamu. Yawezekana kabisa ulikuwa na  mwenzi wako ambaye ulimpenda kwa moyo wako wote na sasa mmeachana.  Kutengana kuna mambo mengi, wakati mwingine ilikuwa hasira tu.
Siku  zote baada ya hasira kuisha, moyo hubaki peke yake katika nafasi yake  halisi ya kufanya maamuzi. Hapo ndipo kwenye lengo la mada yetu ya leo.  Kwamba kwa msingi huo umegundua kwamba kumbe mpenzi wako uliyeachana  naye, bado unampenda.
Kwamba hata makosa aliyokuwa akiyafanya,  ulimsababishia au si makubwa kiasi cha kuachana na badala yake mnaweza  kukaaa na kuzungumza kiutu uzima na kuyamaliza. Yes! Hilo ndilo  ninalotaka kulizungumzia.
Upo tayari rafiki? Je, uko katika kundi  hilo? Unataka kumrudisha mpenzi wako wa zamani? Kama majibu ni ndiyo,  mada hii inakuhusu sana.
JE, NI SAHIHI?
Baadhi  ya watu huamini kwamba kurudi kwa mara nyingine kwa mpenzi wa zamani ni  kujidhalilisha, kujishusha na kujisalimisha. Kwamba hakuna mwanaume wala  mwanamke mwingine yeyote atakayeweza kuwa naye tofauti na huyo  anayemrudia.
Jambo hilo si la kweli hata kidogo, kikubwa cha  kuzingatia hapa ni moyo; je, unahisi bado unampenda? Ni kweli naye  anakupenda? Kama sifa hizi zipo, hayo mambo madogo ambayo mmetofautiana  ni ya kawaida kabisa ambayo mnaweza kurekebishana taratibu.
Kwa  msingi huo basi, hakuna tatizo lolote katika kurudiana na mpenzi wako wa  zamani, maana tayari unakuwa umeshamjua vya kutosha, hivyo kukupa  urahisi wa kufanya yale anayoyapenda na kuepuka asiyopenda jambo  litakalozidisha umri wa uhusiano wenu, si ajabu mkaingia kwenye ndoa.
UTAFAIDIKA NA NINI?
Utafiti  usio rasmi nilioufanya, unaonesha kwamba zipo faida za kurudiana na  mpenzi mliyeachana, lakini kikubwa ni awe moyoni mwako.
Hebu msikie  Julius Kihesupe wa Uwanja wa Ndege, jijini Dar es Salaam, ambaye alipata  kuzungumza nami hivi karibuni akitoa maoni yake kuhusu suala hili: “Si  vibaya kurudiana, maana kwanza mnakomaza uhusiano.
“Kumrudia mtu wako  wa zamani maana yake ni kwamba umekubaliana na udhaifu wake wote.  Unajua anachopenda na anachochukia, hapo lazima mtadumu. Bila  kudanganya, mke wangu wakati wa urafiki wetu, tukiwa na miaka miwili  kwenye uhusiano tulitibuana tukaachana.
“Kila mmoja alikaa kivyake  kwa miezi kama sita hivi, nikakutana naye Dar, nikiwa nimeachana naye  Mbeya, nikamwita tukakaa na kuzungumza, miezi minne mbele yake tukafunga  ndoa.”
CHUNGUZA ALIPO
Kitu cha kwanza kabisa ambacho  unatakiwa kuchunguza ni mahali anapopatikana kwa wakati huo, nasema  hivyo kwa sababu yawezekana alihama makazi, kikazi n.k. Kujua  anapopatikana ni mwanzo wa kuelekea kwenye mafanikio ya kumkamata katika  himaya yako.
ANA HISTORIA GANI?
Lazima ujue kuhusu historia  yake kiuhusiano baada ya kuachana na wewe. Hapo unatakiwa kufanya  ‘ushushushu’ wako kimyakimya bila yeye kujua. Ikiwa ameshafanya ‘vurugu’  sana, maana yake ni mtu asiye na msimamo na huenda anaongozwa zaidi na  tamaa za kimwili na si mapenzi.
Katika kipengele hiki, ni muhimu sana  kujua kama muda huo ambao wewe unahitaji kurudi tena mikononi mwake  kama ana uhusiano mwingine. Kimsingi kama atakuwa ndani ya uhusiano,  itakubidi uhairishe zoezi lako.
Unatakiwa kufanya hivyo kwa sababu  kwanza, anaweza kukubali kuwa na wewe wakati akiwa bado hajaachana na  mpenzi aliyenaye kwa muda huo, hivyo kuwa kama mwizi tu kwa mwenzako.
Kubwa zaidi ni kwamba, utakuwa katika mapenzi ya kushea, jambo ambalo si zuri kisaikolojia na hata kiafya.
Kumbuka kwamba, unaweza kuwa na mwenzi wako, mkapendana kwa  dhati na mkadumu kwa muda mrefu, lakini kwa bahati mbaya mkaachana kwa  sababu ambazo mnazifahamu wenyewe.
Katika muda mfupi ambao utakuwa  umeachana naye, anaweza kufanya mambo ya ajabu sana. Pamoja na kwamba  moyo wako unamhitaji, lakini anaweza kuwa tayari ameshapoteza sifa za  kuwa na wewe. Katika hali hiyo, ni sahihi kurudiana naye? Bila shaka  jibu hapa ni siyo sahihi.
Wiki iliyopita tulianza kuangalia kama ni  sahihi kurudi kwa mwenzi huyo, faida utakazopata kwa kurudiana naye,  kuchunguza sehemu anayopatikana na kufuatilia historia yake baada ya  kutengana kwenu.
Enheee! Sasa twende kwenye vipengele vingine.
 
MAWASILIANO
Ukishachunguza mahali alipo na kuridhika na historia yake  ya kimapenzi baada ya kuachana na wewe, sasa unatakiwa kutafuta  mawasiliano yake. 
Kupata mawasiliano yake ni hatua ya kwanza,  kitakachofuata baada ya hapo ni kujenga mawasiliano. Hapo sasa  inategemea na namna mlivyoachana, lakini kama hamkuwa na ugomvi mkubwa  sana, basi unaweza kumtumia meseji za kichokozi mara nyingi uwezavyo kwa  siku.
Majibu yake ndiyo yatakayokupa mwanga wa kuendelea na kipengele  kingine. Kikubwa hapa ni kutozungumzia kabisa mambo ya mapenzi, badala  yake iwe ni kumjulia hali na utani wa hapa na pale.
MPE MWALIKO
Baada  ya kutengeneza mawasiliano naye, sasa unatakiwa kumwalika katika  shughuli mbalimbali za kifamilia na binafsi. Mathalani umepata mwaliko  wa kwenda kwenye sherehe au hafla fupi ya usiku, omba kampani yake.
Kama  mtu mzima atagundua kitu kilichopo moyoni mwako. Hata kama atakuwa  mwenye moyo wenye kutu, kutoka naye mbele za watu, kutamfanya akumbuke  enzi zenu mlipokuwa mkitoka pamoja, hivyo kufikiria kurudi tena  kwako.
Ikiwa ataamua kukuambia kwamba anaona mrudiane litakuwa jambo  zuri zaidi, maana atakuwa amekurahisishia, lakini akinyamaza, basi njia  inayofuata hapa chini ni muafaka kwake.
MVUTE KARIBU YAKO
Sasa  unatakiwa kumsogeza karibu zaidi na wewe. Lazima afahamu kwamba, kuna  kitu fulani kipo ndani ya moyo wako. Meseji zako zibadilike, kama  ulikuwa unamwandikia, “Vp uko poa?” au “Mambo yanaendaje?”,  sasa  unatakiwa kubadilisha hadi “Niambie sweetie, uko poa?”
Meseji za aina  hiyo zitamfanya aone tofauti na inawezekana kabisa akagundua kwamba upo  kwenye mawindo ya kumrudisha tena kwako. Katika hatua hii katu hutakiwi  kufungua mdomo wako kumwambia kuwa unataka kurudiana naye na badala yake  unatakiwa kuacha vitendo vizungumze vyenyewe. 
 
OUTING
Kutokana na ukaribu wenu, kumwalika katika mtoko wa chakula cha mchana au usiku, haitakuwa vigumu kwake. Hiyo itakuwa njia nyingine ya kumfanya awe karibu yako zaidi. Mkiwa katika mtoko huna haja ya kuzungumza chochote kuhusu uhusiano wenu, labda kama yeye ataanzisha mjadala huo. Ongelea mambo mengine ambayo ni maarufu zaidi labda katika duru za siasa, sanaa n.k lakini si mambo yanayohusu mapenzi kabisa. Kama kichwani mwake alikuwa amekufanya kama rafiki yake wa kawaida, mtazamo utaanza kubadilika taratibu na kuanza kutamani kurudi tena mikononi mwako. Jaribu kufikiria, kama umetoka naye, akiamini labda unataka kumuomba msamaha na kurudiana naye, wewe unaanza stori za soka! Bila shaka atajiona kama mpumbavu kichwani, si ajabu akaamua kujifunga mwenyewe kwa kuomba urudi tena kwake.
JADILI PENZI LENU
Hatua hii ndiyo muhimu zaidi hapa; sasa unatakiwa kuanza kuzungumzia juu ya uhusiano wenu. Mwambie jinsi ulivyokuwa ukifurahishwa na mapenzi yenu. Msifie alivyokuwa anajua majukumu yake na kukuonesha mapenzi ya dhati. Si vibaya kama utamweleza pia sababu ambazo unahisi zilisababisha wewe na yeye kuachana. Kwa kauli hizo utampa nafasi ya kuchambua/kumjua mwenye makosa na mahali pa kurekebisha.
KIRI MAKOSA YAKO
kiwa kuna mahali unaamini ulikwenda kinyume na yamkini ndiyo sababu kuu iliyosababisha muachane, kiri makosa yako mbele yake. Mweleze kwamba wewe ndiyo chanzo cha matatizo na huenda kama si kukosea, msingeachana. Kujutia hasa kama uso wako utawakilisha vyema kilicho moyoni mwako, kutamfanya akuone muungwana ambaye unatambua ulipojikwaa na sasa unataka kurekebisha makosa yako. Hapo utakuwa na nafasi kubwa ya kumnasa kwa mara nyingine.
MWELEZE YAKO YA MOYONI
Sasa huna sababu ya kuendelea kujitesa, toa dukuduku lako. Mwambie moja kwa moja kilichopo moyoni mwako. Kwamba unahitaji nafasi nyingine kwake, maana umeshajua makosa yako.Hii ni nafasi ambayo si rahisi kabisa kuchomoka. Itumie vilivyo. Sauti yako pekee itoshe kumaanisha kile kilichopo moyoni mwako. Lazima atakuelewa. Kama utakuwa umefuata kwa makini vipengele vyote hapo juu, lazima urudi tena mikononi mwake. Kuna nini tena? Ameshakuwa wako huyo, ila kuwa makini usimpoteze tena.
AKIKATAA JE?
Pamoja na kufuata vipengele vyote hivyo, inawezekana akakataa. Kukataa kwake lazima kuna sababu nyingi. Mwingine anaweza kukuambia moja kwa moja sababu za kukataa kurudiana na wewe wakati mwingine anaweza asiseme chochote.
Huenda akakumbia kwamba tayari ana mtu wake, au hafikirii kurudi mikononi mwako; usihuzunike.
Ni bora sana huyu anayekuambia ukweli, kuliko kurudi halafu ukutane na mateso yale yale.Inawezekana labda hana mapenzi na wewe. Kama ndivyo, kuna sababu gani ya kujikomba? Kubaliana na ukweli, halafu subiri mwingine!
Sikia, subiri mwingine na siyo utafute, maana mwenzi wa kweli huja mwenyewe, hatafutwi!
No comments:
Post a Comment