Kuna mtu aliulizia  juu ya tabia ya mpenzi wake kuonyesha hamuamini kwa kila analofanya,  akichelewa kupokea simu, akirudi asimkute, akienda dukani akachelewa  kidogo, vyote kwake huonekana ni matatizo.
Tabia hizi ni kero pale  mpenzi wako anapoonyesha hakuamini kwa kila unalolifanya. Unajiuliza ni  kwa nini akuone si muaminifu na bado yupo na wewe?
Hapa kuna kitu cha  kuangalia. Pengine huyo mpenzi wako ana wivu wa kupindukia na kuona  kila ukiwa peke yako basi akili yako inawaza kusaliti.
Si kweli, si  kila mwanamke akiwa peke yake anawaza ngono, kufikiri hivyo ni kosa  kubwa na inaonyesha jinsi wanaume wa mfumo huo walivyo na ufinyu wa  kufikiria.
Mwanamke anatakiwa kupewa uhuru wa kufanya mambo ya kimaendeleo ambayo wewe mwenyewe unatakiwa kuwa msimamizi.
Wapo  wanaokaa nyumbani kwa vile hawana shughuli lakini hawawazi kufanya  ngono tu, tabia ya umalaya ni ya mtu wala si kwa sababu ya kubaki peke  yake.
Lakini kuna kitu ambacho napenda kukizungumza kwa wapendanao  wote hasa wewe mwenye mpenzi mwenye wivu sana. Unapoona huaminiwi basi  jenga mazingira ya kuaminiwa ili uwe huru.
Nina maana gani? 
Kuna  baadhi wa wanawake huwa hawajui wakiwa peke yao waishi vipi na wakiwa  ndani ya uhusiano iweje pia. Wengi hujiwekea mazingira hatarishi ambayo  kwa mwanaume yeyote rijali, hawezi kuyakalia kimya.
Mfano: Simu  unazopigiwa hazieleweki na wakati mwingine ukakwenda kuzungumzia  pembeni, kwa nini mwenzako asihoji? Unatoka nyumbani bila ruhusa hata  ukiulizwa huna majibu ya kujitosheleza, kwa nini asihoji?
Unakwenda  dukani kwa muda mrefu au unasimama na mwanaume na kuzungumza naye  vichochoroni, hata kama hamzungumzii mapenzi lakini mpenzio lazima  ahoji.
Mazingira ya kuaminiwa
Kwanza, jiheshimu mwenyewe kwa  mavazi na muonekano wako, jiepushe na mazoea na wanaume yaliyopitiliza,  jiepushe kugeuza simu kama kichaka cha kuficha maovu yako. Mlindie  heshima mwenzio hata akiwa mbali nawe.
Punguza vikao na mashoga  wasiokuwa wa lazima. Fanya kile anachokitaka mwenzio na kukiacha  asichokitaka, kuwa sehemu ya maendeleo yake, onyesha umeolewa kwa  kulisema wazi na siyo kuwa msiri ili kujiweka mbali na wanaume wakware.
Ukivifanya vyote hivi vitamfanya mumeo au mpenzio, akuamini hata akiwa mbali na nyumbani.
Saturday, March 17, 2012
Jenga mazingira ya kuaminiwa ili uwe huru
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment