KATI ya vitu muhimu katika maisha ya binadamu ni pamoja na ndoa. Ni  tendo la muunganiko ambalo linaongeza thamani, heshima na utu mbele ya  jamii inayokuzunguka. Wengi wanatamani sana kupata wenzi.
Pamoja na ukweli huo, zipo changamoto ambazo husababisha kuchelewa kupata au kumpata mbabaishaji ambaye hana lengo la dhati. 
Wapo  wasichana warembo, wanaume watanashati sana, lakini kila wanapokuwa  kwenye uhusiano, wanagundua kwamba wapo na watu ambao ‘bado wanazuga’.  Hawana mpango wa kuingia kwenye muunganiko wa ndoa.
Hapo ndipo  panapotokea kuachana. Rafiki yangu, kuacha, kuacha au kuachana mara kwa  mara, kunasababisha sononeko la moyo. Kunakaribisha simanzi na mwisho  wake, mhusika hukata tamaa ya kupata mwenzi wa maisha.
Inawezekana  kabisa, hata wewe uko kwenye kundi hili. Aaaah! Usihuzunike, anza sasa  kutabasamu, maana unakwenda kukutana na dawa baada ya kumaliza kusoma  mada hii.
ANZA KUJIJALI
Maumivu  ya kuachwa kila wakati, yanaweza kusababisha kutokujiweka ‘sopsop’,  kitu ambacho ni tatizo kubwa sana. Sahau maumivu yote, angalia maisha  yako yajayo. Rafiki yangu, hivi unadhani kama hujipendi, hujithamini  nani atakupenda?
Ninaposema ujipende namaanisha ujipe upendo ule wa  kawaida wewe mwenyewe kabla ya kuhitaji upendo wa mtu mwingine. Mwingine  inawezekana hajitunzi, anavaa nguo chafu, hapigi pasi, nywele zipo  timtim n.k
Nani atakupenda kwa misingi hiyo? Hakuna anayependa kuwa  na mtu ambaye hana desturi ya usafi, kwanza hata kama ni mzuri kiasi  gani unapokuwa upo rafu, hakuna mtu ambaye atausumbua moyo wake kuanza  kukufikiria wewe usiyejipenda.
Siyo lazima wakati wote uwe ‘smati’,  kwa kuwa inawezekana wengine wanafanya kazi ambazo zinawalazimu kuvaa  nguo chafu, lakini baada ya hapo, unatakiwa kuwa katika hali ya usafi.
Upande  wa wasichana siyo lazima uweke nywele zako dawa au usuke rasta wakati  vitu hivyo huna uwezo navyo, unaweza ukasuka nywele zako vizuri au  wakati mwingine ukanyoa mtindo mzuri unaokubalika ambao hautakuweka  katika mtazamo mbaya kwa jamii.
Anza kujipenda kabla ya kuhitaji  upendo kutoka kwa mtu mwingine, hiyo itakusaidia kuwa na mvuto na  mwonekano mzuri kiasi cha kuweza kumpagawisha mtu mwingine kuanza kuhisi  cheche za moto wa mapenzi katika moyo wake.
Safiri na neno hili, huhitaji tena mateso katika maisha yako. Sawa jamani? Haya, tuendelee.
KUJIAMINI NI MUHIMU
Hili  ni tatizo la kisaikolojia zaidi kwa sababu kuna baadhi ya watu wanakosa  kujiamini. Kuna mwingine anaweza akakaa kwenye kioo kwa saa kadhaa na  kuanza kujitoa kasoro katika mwili wake.
Hujiona mbaya asiyevutia na  ambaye hana thamani kabisa katika ulimwengu wa mapenzi, hujiona hawezi  kupata mpenzi katika maisha yake yote baada ya kujitoa kasoro hizo.  Mwingine hujiona ana matiti mabaya, mfupi sana, mrefu sana ana matege,  ana makengeza na kasoro nyingine zozote ambazo huhisi ni kosa kuwa nazo. 
Nani amekuambia kuwa una kasoro? Mshukuru Mungu kwa kukuumba jinsi  ulivyo, amini kuwa Mungu ana makusudi yake kukuumba kama ulivyo.
Kuna watu wengine wanaweza kukupenda kutokana na hizo kasoro unazoziona katika mwili wako!
Kujitoa  kasoro na kutojiamini ni kosa kwa kuwa unakuwa unajiathiri kisaikolojia  na kujiona hufai kupendwa mwisho wa yote unakuja kumparamia mtu yeyote  kwa nia ya kujiondolea mkosi na akishakutumia anakuacha solemba unabaki  na machungu moyoni na kujiongezea matatizo zaidi.
Naamini baada ya  kujipenda wewe na kujiamini kuwa unavutia, utakuwa katika hali ya  kawaida kisaikolojia na wakati mwingine anaweza akajitokeza akupendaye  na kukuomba hifadhi ya moyo wake kwako.
Sababu ya kukaa muda mrefu  bila mpenzi au kutamkiwa kuwa unapendwa isiwe chanzo cha kupata maumivu  mapya ya moyo. Kuachwa kwako, kusiwe chanzo cha kuingia kwa mwingine  ambaye anaweza kuwa mwiba zaidi.
Acha papara, tulia, pata wasaa wa  kumchunguza huyo anayedai anakupenda kwa muda wa kutosha kwa kuwa  inawezekana naye akawa ni mmoja kati ya wale wanaotaka kukufanya chombo  cha starehe!
Akikuhitaji kuwa na wewe (huyo mwanaume)lazima  umchunguze kwanza na usiruhusu aujue mwili wako kabla ya kuelewa nia  yake hasa kwako ni ipi; starehe ya muda mfupi au anakuhitaji kimaisha.
Usifanye mambo kwa papara, unahitaji utulivu wa kutosha ili uweze kumpata yule ambaye ni muhimu kwa ajili yako.
 Ukijiamini na kuwa makini ni wazi kuwa utampata yule anayekupenda kwa dhati.
Saturday, March 17, 2012
Je.Umekata tamaa ya kupata mwenzi wa maisha
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment