Saturday, March 17, 2012

Migogoro na utatuzi wake katika mahusiano yetu

Mahusiano mengi sana yamefikia katika hali mbaya na mengine kufa kabisa huku wapenzi wakiachana katika maumivu na majeraha makali ya moyo kisa kikubwa kikiwa kutojua kwao kuishughulikia migogoro inayojitokeza katika mahusiano yao.

Mara nyingi katika ushauri tunasema shida sio kujikuta ndani ya migogoro bali shida ni namna mnavyoishughulikia migogoro hiyo. Unapoona mahusiano ya wengine ni mazuri na ya kutamanisha, haimaanishi nao hawana migogoro, bali wanayo lakini tofauti ni ujuzi wao wa kushughulika na migogoro hiyo.

Kiu yangu ni kwamba, mwisho wa kusoma andiko hili ufahamu namna ya kuboresha mahusiano yako kupitia kujua jinsi bora za kushughulikia migogoro baina yako na mpenzi wako pamoja na wote wanaokuzunguka.

Tunaziona ndoa na mahusiano mengine mengi yakiwa na maumivu, machungu na mapigano kuliko nyakati za amani na maelewano.

wale walioweza kuimarisha amani na maelewano katika mahusiano yao sio kwamba ni mapacha na wanafanana katika kufikiri na kutenda kwao, sio kwamba wameumbwa wenye tabia za kufanana na mtazamo sawa bali ni wale waliojifunza kuchukuliana na tofauti zao, wakizikubali na kuzielewa vema na kila mmoja akijaribu kuujazia udhaifu wa mwenzake, wamejifunza kuzungumza kila mmoja kwa lugha ya mwenzake wakizielewa haiba zao na kubadilika kutokana na hali halisi.

Kwakuwa wote hatufanani, na tofauti hizi tunaingia nazo katika mahusiano yetu, daima lazima tofauti ziibuke baina yetu, na sio kwamba mgogoro huwa mmoja bali huwa mingi, midogo na mikubwa, na wala hili sio jambo baya na lakushangaza bali ni kitu cha kawaida.

Nini maana ya “mgogoro” Ni kutofautiana, baina ya watu, kupingana, kutoafikiana katika jambo fulani au mawazo fulani.

Kati ya njia za kizamani ambazo zinatumika na wapenzi wengine katika kushughulikia migogoro ni kuinyamazisha, kuifukia na kujitahidi kuisahau migogoro hiyo, njia hii imetumika sana hasa kwa wale wanaoshika dini zao. Kwa kuzika na kufunika migogoro hatutatui bali tunajenga na kukomaza maumivu ya ndani na chuki ambayo taratibu inabadilisha mitazamo yetu kuwa mibaya kwa wale tunaowapenda.

Kumbuka, tofauti hizi zinapozikwa, huzikwa zikiwa hai, na hivyo lazima zitafufuka na kuleta shida.

Wapendanao wengine hushughulikia migogoro yao kwa kuamua kupakua kila kilichopo moyoni na kukimwaga kwa aliyewaudhi, tumesikia wengi wakisema “mpe vidonge vyake”, “mpakulie” kwa wengine njia hii imezaa vita na magomvi tele. Neno baada ya neno, jibizano baada ya jibizano na hatimaye kofi na ngumi navyo vikaingia kazini.

Kutokana na tafiti tulizozifanya kwa wanandoa wengi na wale wengine walio katika mahusiano, wengi wameelezea kuumizwa sana na viugomvi vya mara kwa mara vinavyosababishwa na mgogoro fulani baina yao. Kumbuka kuwa mgigogoro inaweza kushughulikiwa pasipo magomvi.

Ugomvi maana yake ni vita ya maneno ambayo inaruhusu hisia za hasira kuchukua nafasi, na hapa wapenzi hawaangalii tena sababu za mgogoro wao bali wanaanza kulengana wenyewe binafsi na kushushiana maneno, matusi na lawama.

Kwa wale wanoamini vitabu vitakatifu vinasema “Wapumbavu hugombana wakati wote bali wanaoepusha magomvi huleta heshima”.


Katika kushughulikia migogoro inakupasa uyafahamu haya:

1. Migogoro ni jambo asilia na kwahiyo haliepukiki
Kama nilivyokwisha kusema awali kwamba wote sisi tumetokea katika tofauti, mitazamo yetu na matakwa yetu ni tofauti na kwahiyo tutegemee kabisa kutofautiana katika chaguzi zetu, mapendeleo yetu, mitazamo yetu nk. Migogoro pia haiepukiki hususan kwa watu wanaopendana na wenye kiu ya kudumisha pendo lao zaidi.

Migogoro ya mara kwa mara baina ya wanandoa ni ile ya maneno, hii kwa jinsi ilivyo peke yake haidhuru kitu, kwa kutegemeana na kupevuka kwa wale waliotofautiana. Wako wanaoweza kutofautiana, wakalumbana kwa maneno na wakaishia mwisho mwema, wako wanaolumbana na kuishia katika kutwangana.

2. Migogoro huonyesha kunyimwa au kudhulumiwa kwa hadhi au hitaji la mmoja baina ya wapendanao
Kila mtu ana mahitaji binafsi na ya msingi katika uhusiano, mtafiti William Glaser anasema kati ya mahitaji ya msingi ya mwanadamu ni hitaji la kupenda na kupendwa na hitaji la kujiona au kuonwa wathamani na unayefaa na unayestahili.

Mara unapoingia katika mgogoro na mpenzi wako, hembu jiulize, ni hitaji gani ambalo halijatimizwa? Maana kwa kutokutimizwa kwa hitaji lolote lako lazima itapelekea mgogoro kunyanyuka.

3. Migogoro wakati wowote ni dalili ya hitaji lililofichika au lililojificha
Wakati wowote unapojikuta katika mgogoro kunakuwa na hitaji ambalo halijatatuliwa au kupatiwa ufumbuzi. Kwa kutatua mgogoro yamkini isiwe njia ya kulisuluhisha tatizo. Ni bora waangalie kwa undani dalili hizo ili ugundue hitaji ambalo mwenzako amekazana kulitimiza na baada ya kuligundua basi litatue tatizo hilo na siyo kutatua dalili zake tu.

4. Migogoro mingi haishughulikiwi kwa uwazi kwa sababu wengi wetu hatujajifunza njia bora za kutatua migogoro hiyo
Wapendanao wengi hudharau vimigogoro vidogo vidogo, wakiviepusha visisumbue uhusiano wao, na mara migogoro mikubwa ijapo, watu hawa huiepuka pia maana hawajui namna ya kukabiliana na hata ile midogo.

Kama hujui kushughulikia migogoro midogo, je hiyo mikubwa utaiwezea wapi? Hakuna vijimigogoro katika uhusiano, yote huitwa migogoro na inastahili kupatiwa uzito sawa katika kushughulikiwa na siyo kudharauliwa maana athari zake ni kubwa.

5. Migogoro inatoa fursa ya uhusiano wetu kukua
Migogoro inafananishwa na baruti, baruti yaweza kuleta uharibifu mkubwa ikitumiwa vibaya na pia yaweza kuleta mabadiliko mazuri ikitumiwa vizuri. Ni baruti hiyohiyo iwezayo kuvunja nyumba na kuua lakini ni baruti hiyohiyo iwezayo kuondoa mlima au kichuguu ili kutengeneza barabara au nyumba nzuri.

Kupitia migogoro mtu anaweza akazishirikisha tofauti zake kwa mwingine, kukutana na migogoro kunakupa fursa pia ya kuonja nguvu ya mwenzako. Kila mmoja akiwa katika mgogoro hujaribu kuleta njia mbadala ya kulijadili suluhisho, njia hizi zaweza kuangaliwa na wote na baadaye kufikia maamuzi mema pale mgogoro unaposuluhishwa, wote hujengwa na kukua. Itaendelea wiki ijayo... 6. Migororo hufanya wapendanao kutokujihisi kutosheka na penzi lao.
Migororo isipotafutiwa ufumbuzi vikwazo kuinuka mara kwa mara na wapendanao hujikuta wanakuwa wenye kukwepa na kujihami katika kila kitu kwa sababu ya kuogopa kuumizwa, tabia hii ni kitanzi katika uhusiano, kamwe msitegemee penzi lenu kukua kwa staili hii.

NINI CHA KUFANYA UNAPOKUWA KWENYE MGOGORO NDANI YA UHUSIANO?
Mara nyingine tunafikiri kuwa wapenzi wetu nao wataichukulia migogoro kwa namna sawa na sisi, lakini unakuja kukuta njia zao ni tofauti kabisa na za kwetu.

Watafiti wengi wamesema kuwa mchakato wa mgogoro katika uhusiano huanzia katika tofauti zetu tulizo nazo, zinazosababisha sisi kutofautiana kimtazamo, tofauti hizi za kimtazamo husababisha kugombana (migogoro kuibuka) na hapo njia ya utatuzi huhitajika.

1. Je, wewe hujitoa (Withdraw) kukwepa kuhusika katika mgogoro?
Watu wa namna hii huwa na tabia ya kuiona migogoro kama si kitu, huiona migogoro ni ya kupoteza muda tu, haina haja ya kuchukua fikra zao nyingi, hawana haja ya kujiingiza katika kutatua.

Hapa wanajitoa kimwili tu lakini kifikra na kihisia bado wapo ndani ya migogoro. Hujiweka katika hali ambayo itamfanya kila kinachoongelewa hakimwingii moyoni hata kama anakuangalia usoni, wengi wetu hutumia staili hii, ingawa siyo tabia nzuri hata kidogo.

2. Je, wewe hulazimisha ushindi katika mgogoro (winning)?
Kama nafsi yako imetishwa na mgogoro huo, na unaona ni lazima ushinde wewe, basi kila wakati utalazimisha ushindi tu. Watu hufanya mbinu mbalimbali ili tu kuwa washindi, kwa sababu katika uhusiano tunajuana sana udhaifu wetu basi kila mmoja atajaribu kuingiza mkuki kwenye maeneo dhaifu ya mwenzake ili tu kumfanya awe mpole na kuuruhusu ushindi uende kwa yule muumizaji.

3. Je wewe hujishusha wakati wa migogoro?
Hapa mmoja huangalia eneo gani atafaidika kwa kujishusha na kukubali mawazo yake yashindwe, sio kila kitu atakuwa mpole, la! bali katika maneo fulani. Mtu wa hivi atakubali ajinyime kidogo ili basi afaidike kidogo na wewe ufaidike kidogo pia, sio kwamba ushinde kabisa, au ashinde yeye kabisa, staili hii huusisha wale wenye kuzifikiria pande zote mbili za mgogoro.

4. Je, wewe ni kati ya wale wenye kutafuta suluhisho? (Resolvers)
Katika staili hii, wapendanao huruhusu mawasiliano ya wazi na ya moja kwa moja, katika kubadili hali, mtazamo au tabia zao, wapenzi wanakuwa tayari kutumia muda wowote kuziangalia tofauti zao, ili hata kama baadhi ya matakwa yao yametimizwa basi waridhike na suluhisho wanalolifikia pamoja.

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment