Nina imani  uliyemchagua kuwa mpenzi wako ni chaguo la moyo wako, hasa nikizingatia  kuna wanawake wengi au wanaume wengi lakini upo na huyo uliyenaye.
Inawezekana  uliyenaye si wewe wa kwanza kumpenda, huenda yeye alikupenda kabla  yako, ila akashindwa kukuanza kutokana na uzito wa mdomo wake au desturi  ya mila zetu kuwa mmoja ndiye mwenye uwezo wa kuongea lile linalomsibu  juu ya matamanio ya moyo na mwili.
Kwanza lazima tujue kukaa pamoja  au kuchagua mpenzi ni bahati nasibu, unaweza ukapenda kiasi cha kufa na  kuoza lakini mwenzako yupoyupo hajali mateso ya moyo wako, anachojali ni  kuufurahisha mwili wake na siyo kufurahisha nafsi ya mpenziwe ambayo  ndiyo inayotaabika.
Nina imani kila atafutaye mpenzi, hutafuta wa  kufa na kuzikana, wapo wanaoanza uchumba mpaka ndoa kamili, pia wapo  wanaowataka watu kwa ajili ya kuangalia mwanamke ana nini kutokana na  sura yake, umbile lake au sauti ambayo hujiuliza akiwa hivi sauti yake  ipo hivyo, je, kwenye shughuli inakuwaje?
Mwingine anavutiwa na  utanashati wako au pengine ‘u-handsome’ au hata umbile lako la kimazoezi  ndivyo vinavyomfanya ajisikie kufanya mapenzi na wewe lakini siyo  kwamba anakupenda.
Wapo wanaofuata fedha zako na pale zinapoisha na  mapenzi pia huisha. Wapo wanawake duniani wasiojua dunia inakwenda wapi  na nini hatima ya maisha yao, hawa wanakutana na wanaume baa na kulala  nyumba ya wageni na baada ya hapo hamjuani.
Lakini wapo ambao wana  mapenzi ya dhati waliojitoa kimwili na kiakili, siku zote huwa na  maswali magumu mioyoni mwao na kuwafanya waishi kwa mashaka kwa kuhofia  kukupoteza.
Kama nilivyosema kuchagua mpenzi ni bahati nasibu,  hakuna aliye mjuzi wa kuchagua mpenzi aliye safi, inategemea karata  uliyofunua. Kama utapata karata nzuri hapo mshukuru Mungu kwa kukupatia  mpenzi mzuri mwenye haruma na mapenzi ya kweli.
Nina imani ndani ya mapenzi umpendaye siku zote huumia moyoni na kujiuliza maswali haya ambayo ni wewe wa kuyajibu.
Kwa kupitia kona hii, unatakiwa kuyajibu kwa vitendo kwa kuwa wengi wamekuwa na mapenzi ya mdomoni.
Unajua wapenzi wametoka  wapi? Tabu ngapi wamevumilia mpaka kupata mafanikio halafu wewe utokee  kama kunguru wa Zanzibar unapitia vilivyo anikwa!
Haah! Wananiudhi  sana, siyo siri siwapendi wanaodhurumu haki ya mtu, kwani wanaume  wamekwisha au wanawake wamekwisha mpaka umchukue wa mwenzio? Haipendezi.
Wacha tuendelee najua wamesikia, siku zote dawa chungu ndiyo inayotibu.
Eeh!  Nilishia wapi wiki iliyopita? Ooh nimekumbuka, niliishia kwa kujiuliza  ni maswali gani mpenzio hujiuliza ndani ya mapenzi ambayo unatakiwa  kuyajibu kwa vitendo hasa akiwa ana mapenzi ya dhati kutoka chini ya  uvungu wa moyo wake?
Akupendaye kwa dhati hujiuliza maswali haya:
Mosi: Je, unaujua upendo wake wa dhati kwako?
Pili: Je, unampenda kama yeye anavyokupenda?
Tatu: Je, mapenzi anayokupa unaridhika nayo?
Nne: Ni kweli yupo peke yake?
Tano: Ni kweli penzi lenu litadumu?
Sita: Je, unampenda kwa sababu gani?
Haya  maswali huwa moyoni mwa mtu, mara nyingi mtu hawezi kuzungumza mapema  na hubaki kuwa siri yake. siku zote vitendo unavyomfanyia kwa bahati  mbaya, humpa maswali mengi juu ya yale anayoyawaza.
Kwa mfano  ukichelewa kurudi nyumbani, lazima atakuwa na wasiwasi kwamba una  mwanamke au mwanamume mwingine. Mawazo hayo yataleta maumivu moyoni  mwake, japo hawezi kuzunguza.
Pia ukimkaripia mwenzi wako, atazidi  kujiuliza sana kwani ataona kama humpendi na pengine upo naye kwa  shinikizo fulani na si mapenzi ya dhati. Lakini pia suala la kutompa  nafasi ya kumsikiliza anachokisema au kushauri, humuumiza sana mpenzio  na kuona kwamba karata aliyofunua si dume la mchezo kama alivyofikiria,  bali ni galasha.
Kitu kingine ni kutoambatana naye katika safari zako  zisizo za kikazi au kwenye sherehe. Katika hilo lazima atajua una mtu  mwingine aliye muhimu kwako kuliko yeye.
Kingine ni kutomsifia kwa  lolote alilolifanya ambalo alitegemea umsifie lakini wewe ukaona ni  jambo la kawaida. Hili nalo humuumiza mpenzi wako na kumfanya ajiulize  maswali mengi.
Kwa wanaume, ikiwa mwanamke haonyeshi furaha yoyote  akimuona mwenzake amerudi kutoka kazini, yaani haonyeshi kama amemmisi,  basi ni lazima aanze kujiuliza kulikoni.
Kutokufurahia zawadi yake  anayokuletea na kuonyesha mbele yake kuwa hukuipenda na kuonyesha haupo  makini naye hata anapokuaga wakati akielekea kazini, pia humfanya abaki  na maswali.
Huna tabia ya kushukuru kwa chochote hata ukipewa busu,  kwako sawa. Inawezekana ulikuwa hujui maswali ajiulizayo mpenzio kwa  tabia zako. Sasa kama ulikuwa hujui, unatakiwa kufanya yafuatayo bila  kuulizwa ili kuifanya nyumba yako ijae furaha siku zote.
Maswali gani ambayo unatakiwa kumjibu mwenzako ambayo huwa vigumu  kuyasema kwa mdomo.
Baada ya kutambua maswali, nini cha kufanya?
Unapoanzisha  uhusiano unatakiwa kumsoma mwenzako anapenda nini na kipi ambacho  hakipendi. Vichukue vyote kisha kaeni chini na kuchambua kimoja baada ya  kingine. Angalia mifano ifuatayo:
Mosi
Mpenzi wako anapenda baada  ya kazi muwe pamoja, je, kwa upande wako nini kinakufanya usiwe pamoja  na mwenzako? Kama kina sababu ya msingi basi kaeni chini na kujadiliana  bila kutumia mabavu.
Pili
Mpenzi wako huenda anapenda muoge na  kula chakula cha usiku pamoja, kuna sababu ya kukuchelewesha? Kama  hakuna ni nafasi nyingine ya kuongeza upendo ndani ya nyumba.
Mara  nyingi wafanyakazi huwa mbali na wapenzi wao kwa muda mwingi, lakini  inapotokea unaoga na kula pamoja na wenzako, hali hiyo usababisha  kuondoa upweke na kumfanya mwenzio ajione upendo wako kwake bado upo  juu.
Kumekuwa na matatizo mengi katika uhusiano kwa wanaume wengi  kuamini fedha ni kila kitu. Unaweza kumpa kila kitu mkeo kwa kumnunulia  nguo, vyakula na kuhakikisha hana shida, lakini huna muda wa kukaa naye  badala yake mawazo na akili vyote vipo kwenye kutafuta fedha na kusahau  mwenzako naye anakuhitaji.
Hivyo basi pamoja na ugumu wa kazi  unatakiwa kutenga muda angalau saa mbili ili kuzungumza na kubadilishana  mawazo ikiwemo kula na kuoga pamoja. Siyo kumkuta kitandani na kumuacha  kitandani.
Tatu
Mpenzi wako anahitaji umuonyeshe unakijali  chochote anachokupatia, kumekuwa na tabia za baadhi ya wanawake  kutoshukuru zawadi zisizowafurahisha. Hii inapunguza upendo na kumfanya  mwenza wako asiwe na hamu ya kukuletea kitu kwa kuhofia hutakipenda.
Siku  zote onyesha kujali kile unachopewa hata kikiwa kidogo, kufanya hivyo  ni kuonyesha unajali na kumfanya mwenzako akuletee kikubwa zaidi.
Mwisho
Jiepushe  kuwa chanzo cha maumivu ya wenzetu, jaribu kuyafanya yote ambayo  hayahitaji nguvu wala fedha kumfurahisha wenzako. Mpende mwenzako kwa  vitendo kwa kuyafanya zaidi anayoyapenda na kuyaacha asiyoyapenda.
Muonyeshe  unamjali kwa kuwa naye karibu hata kumshirikisha katika mambo  yanayowahusu, kwani mwenzako ni sehemu yako, hivyo, ushauri wake ni  muhimu. Kama utakuwa umefuatilia tangu mwanzo wa mada hii, nina imani  nimeeleweka, kilichobakia ni utekelezaji.
Saturday, March 17, 2012
Mjibu mpenzi wako maswali haya kwa vitendo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment