Saturday, March 17, 2012

Namna 11 za Kutibu Wivu

11. JIFUNZE KWA WATU WENGINE
Mara nyingine ni rahisi kugundua kuwa unafanya makosa baada ya kuwaona wengine na kujifunza kutoka kwao. Hivyo basi, jaribu kuwaangalia watu wengine walio kwenye uhusiano. Fuatilia mtindo wao wa maisha, mafanikio yao kisha ujitazame wewe.
Bila shaka hapo ulipo, utakuwa umeshawahi kujionea wanaume na wanawake wenye wivu, jinsi wanavyotenda mambo yao, wanavyoudhi na kuchukiza kwenye uhusiano. Kama ndivyo, basi hilo ni somo kwako kwa kuepuka yale yaliyowafanya wachukize.
Inawezekana ukawa umeona kupitia kwa macho yako au umesimuliwa. Muhimu kutambua ni kwamba hulka za wivu, hususan unapozionesha mbele za watu wa pembeni ni mbaya. Kwa mantiki hiyo, kama utaweza kutambua na kuelewa alama za wivu, sina shaka kuwa utakuwa unaweza kujua jinsi ya kuishi katika mazingira salama.

10. MPE NAFASI
Kumbana mwenzi wako haina maana ndiyo utamfanya adumishe uaminifu kati yenu. Jifanye kama mtu usiyejali, muache atoke na marafiki zake. Inaweza kuwa tatizo endapo ataona unamnyima uhuru anaoutaka. Anahitaji nafasi ya kufurahi na marafiki zake, unambana kwa nini?
Akilini kwako lazima ukubali kwamba mwenzi wako ni mtu mzima na anajitambua, kwa hiyo uhuru utakaompa, utawezesha yeye kujiamini zaidi na kuheshimu uaminifu wako kwake. Kisaikolojia, mwenzi wako akigundua unamuamini, naye huzidisha upendo.
Vizuri pia kutambua kuwa wivu hukua zaidi pale mmoja anapokuwa na hisia kwamba mwenzi wake anasaliti. Kama upo kwenye uhusiano wenye afya, huhitaji kusumbuliwa na mawazo mabaya. Endapo utashindwa kuondoa wingu la shaka ndani yako, kaa ukijua kuwa unajiharibia.

9. ONGEZA UAMINIFU
Mojawapo ya dawa nzuri ya kukabiliana na wivu ni kuongeza kiwango cha uaminifu. Muamini mwenzi wako na utaona jinsi mambo yatakavyokwenda. Tunza akilini kwamba kutengeneza uhusiano imara na wenye mafanikio, huhitaji kiwango kikubwa cha uaminifu.
Amini kuwa mwenzi wako atafanya mambo sahihi hata kama wewe hutakuwepo. Muamini kuwa anajitambua, kwa hiyo hatakuwa na muda mchafu wa kutenda maovu kwa kigezo kwamba haupo. Ana akili timamu, akiamua kutenda ‘uwaluwalu’, hashindwi hata kama utakuwepo.


8. MWONESHE MWENZI WAKO
Ukiwa na mwenzi wako, muoneshe kwa mifano halisi jinsi unavyojisikia au unavyoweza kumtendea katika nyakati ambazo unamuonea wivu. Kufanya hivyo, ni rahisi kwako kutambua maumivu yako, vilevile na yeye atajua mahali ambako anakosa mengi matamu.
Mtu anapoona wivu wa ndani, husumbuliwa na maumivu ya moyo. Aghalabu, akili yake hushindwa kufanya kazi inavyotakiwa. Mantiki ya hoja hiyo ni kwamba mwenzi wako hawezi kukutendea mambo matamu, ikiwa kichwa chake hakitakuwa katika hali ya kawaida.
Unaweza pia kuvuta picha na kujadili muonekano wako pindi unapokuwa na wivu. Hakikisha mwenzi wako anakuelewa kinaga ubaga kile unachomaanisha. Je, umegundua umepoteza raha kiasi gani? Umefahamu namna ambavyo huwa unaboa? Mpe uhuru mpenzi wako akwambie ukweli.
Inawezekana akawa anasita kukwambia bayana kutokana na hofu. Unapaswa kulijua hilo mapema. Unaweza kumpa nafasi aseme, akakujibu hakuna kitu. Ukishagundua kuwa anakohofia, jaribu kumshawishi ili afunguke. Akikubali kueleza la moyoni, ni tiba kubwa kwako.
Bila shaka utagundua ni kiasi gani anakerwa na tabia yako ya wivu. Je, ni nani anapenda kumuudhi mwenzi wake kila siku? Hakuna na kwa hakika hata wewe mwenyewe hupendi. Hivyo basi, amani yake itatokana na tabia yako ya kumuonea wivu.
Fikiria kuwa anashindwa kuwa mtulivu kufanya jambo lolote kwa sababu anahofu unaweza kulipokea tofauti. Kwa nini unamnyima uhuru kwa sababu ya wivu wako? Fungua moyo leo, muoneshe kuwa unamuamini. Imani yako itamfanya aongeze upendo kwako. Siku zote, mapenzi husafiri kwa mtindo wa nipe nikupe.
Hata hivyo, njia hii kwa watu wengine hushindwa kufanya kazi. Inapasa mtu mwenyewe awe amedhamiria kurejesha amani na furaha kwake na kwa mwenzi wake. Vema uzingatie kwamba wivu ukizidi ni ushamba. Jamii itakudharau, hata mwenzi wako akikuchoka, anaweza kukugeuza zuzu.

7. JIAMINI
Wivu mara nyingi huanza kutokana na kukosa kujiamini. Jiulize, unajisikia salama wewe mwenyewe? Je, unaogopa kwamba mpenzi wako anaweza kukuacha kwa sababu umepungukiwa sifa kadhaa? Mambo mengi kati ya hayo yanapogota kichwani, huyafanya maisha yako yatawaliwe na wivu.
Inawezekana mwenzi wako anakupenda kuliko wewe unavyompenda. Si ajabu, akawa anawaza kufanya maisha bora zaidi akiwa na wewe. Amekukubali kwa namna ulivyo kiasi kwamba hawazi kukupoteza. Tofauti na mawazo yake, tabia yako ya kutojiamini, hufikiria kwamba hakupendi.

6. WASILIANA MARA KWA MARA
Una wasiwasi na mahali ambako mwenzi wako yupo? Huna amani na unahisi anakusaliti. Moyo wako umefunikwa na jakamoyo na kila hatua mapigo yanaongezeka kasi au yanashuka. Kimsingi huna sababu ya kuwa hivyo. Usiishi kwa dhana, ila simamia vitu vinavyoonekana.
Mawasiliano ni njia bora kabisa ya kudhibiti wivu. Mnapozungumza mara kwa mara au ‘kuchati’ kwa SMS, Facebook au mitandao mingine ya kijamii, huwaweka karibu. Kama una hali ya wasiwasi, itakwisha au kupungua kwa sababu muda wote utajiona kama mpo pamoja.
Je, mkiwa wawili chumbani au sehemu yoyote ya faragha, bila simu wala mtu wa tatu anayeweza kuingilia ukaribu wenu, mnaweza kuanza kulumbana kwa sababu ya kuoneana wivu? Jibu ni hapana. Hivyo basi, mawasiliano ya mara kwa mara huwaweka karibu na ni salama zaidi kuliko hata mngekuwa wawili chumbani.
Mawasiliano yasiwe yenye kuishia katika simu au mitandao, kama hamjafunga ndoa au tayari ni wanandoa lakini hamuishi pamoja, jitahidini kukutana mara kwa mara. Ikiwa mnaishi eneo moja, wekeni utaratibu wa kuonana kila inapobidi, hiyo itasaidia kukuza upendo na amani ambayo itayeyusha hulka za wivu.
Wakati ukitekeleza hili la kuonana mara kwa mara na mwenzi wako, si vibaya ukamwambia jinsi unavyoumizwa na tabia ya yeye kufanya mawasiliano ya karibu na watu wenye jinsia tofauti na yeye. Ukizungumza naye kwa upole, hali itakuwa nzuri kuliko kulaumu au kulalamika.
Hoja ya wivu iwekwe mezani halafu muijadili kwa upana. Kitendo cha kujadili na mwenzi wako jinsi wivu unavyokutesa, kitasaidia kuweka mwanga na kupata ufumbuzi wa tatizo husika. Kama atajua mambo ambayo akiyafanya utaumia halafu akatekeleza bila woga, maana yake atakuwa amedhamiria kukuumiza, hivyo hakufai kwa maisha yako.


5. ACHA KUFANANISHA
Kuna tabia ambayo huwatesa watu. Ni kujifananisha na watu wengine. Mfano; Mwenzi wako ana ukaribu na mtu fulani, wewe badala ya kushughulikia tatizo ili amani ichukue mkondo wake, unaanza kumtazama huyo mtu halafu unajifananisha.
Pengine ukampima na kujifananisha kutokana na muonekano wako ukilinganisha na yeye. Unaweza pia kuweka kigezo cha fedha, ukajiuliza kama anakuzidi au unamzidi. Zaidi ya hapo, sura, mavazi na kadhalika, vinaweza kukutesa akili. Acha tabia hiyo, wekeza upendo na mambo yatakaa sawa.
Huwezi kujifananisha na mtu mwingine, vilevile kwa mwenzi wako, haipendezi pia haitakiwi kumlinganisha na yeyote yule. Kila mmoja yupo tofauti kwa sababu kadhaa. Pamoja na ukweli ni kwamba suala la kumtazama mtu na kumuona anakuzidi linaweza kukupa unyonge lakini ujinga wa kupindukia.
Watu wengi husumbuliwa na mawazo kuwa wenzi wao wanaweza kuwaacha na kwenda kuanzisha uhusiano na wengine wenye ubora kuliko wao. Kama mpenzi wako aliwahi kuvutiwa na mtu mwingine kabla yako, huwezi kujua, muhimu ni kuzingatia kile ambacho amevutika kwako.
Zingatia kuwa endapo mwenzi wako angekuwa amedata kwa mtu mwingine tofauti na wewe, huwezi kujua lakini ukweli ni kwamba msingekuwa na uhusiano wa kimapenzi mlionao leo. Achana na mawazo yasiyojenga, amini kuwa mwenzako amedata kwako ndiyo maana leo mpo pamoja.
Jenga utaratibu mzuri wa kuheshimu jinsi mwenzako alivyo. Kadhalika jiamini kwamba duniani hakuna mtu bora kama wewe, kwa hiyo usiishi kwa kumuogopa mtu kutokana na fedha zake au sifa nyingine yoyote. Dunia imeumbwa na vitu tofauti, hivyo na watu wametofautiana, ingekuwa wote tunafanana, hakika ingekuwa ni ulimwengu ‘unaoboa’ kuishi.


4. BADILI WIVU KWA HISIA CHANYA
Jifunze kutafsiri matendo yake kwa upendo. Vuta picha na ujipe hamasa chanya badala ya kuumia kwa kila atendalo. Katika hili, ni vizuri ukaongozwa na subira, kwani asili ya watu wenye wivu wa kupindukia, hukimbilia kupandwa na jazba, badala ya kuuliza kwa utaratibu na kupokea jibu linalojitosheleza.
Hata siku moja usije ukadanganywa kwamba ukiwa mkali ndiyo kutamfanya mpenzi wako asikusaliti. La hasha! Wekeza upendo kisha muishi kwa maelewano, hapo utaweza kumpa sababu ya kuishi kwa uaminifu. Utafiti unaonesha kuwa kundi la wasaliti wa uhusiano wao, huundwa na idadi kubwa ya watu waliochoshwa na migogoro ya kimapenzi.
Mantiki hapa ni kuwa mtu yupo kwenye uhusiano wake lakini anaamua kutoka nje baada ya kuona hana maelewano na mwenzi wake. Hivyo basi, ni vizuri ukawa unafuata hatua zinazofaa katika kupata ufumbuzi wa kila jambo unaloona halipo sawa kwa mwenzi wako, badala ya kugombezana. Itakugharimu.
Kama wivu wako unakufanya ujione wewe ni dhaifu, huna jambo la kufanya zaidi ya kuhakikisha unaishinda hali hiyo. Ukiwa na tabia ya kujiamini, itakusaidia kuufunika wivu, japo bado utaendelea kuwepo ndani yako lakini jinsi utakavyokuwa unashughulikia mambo yako na mwenzi wako, itakupa heshima zaidi.
Wivu ukizidi ni hatari kwa sababu unaweza kukuweka roho juu muda wote, ukaonekana mapepe na jamii ikakucheka kutokana na jinsi kichwa chako kilivyo rahisi kushika moto. Hii ina maana kuwa kudhibiti wivu ni kujiongezea heshima. Tafakari mwenyewe, unataka uheshimiwe au udharauliwe?
Unajidharau? Unakosea sana, muonekano wa juu hubadilika kutokana na wewe mwenyewe unavyoamua na kujipanga. Tatizo ni nguo? Mbona hivyo ni vitu vya kununuliwa? Unayo nafasi ya kutafuta na kupata, kwa hiyo punguza kuchachawa, wekeza upendo kwa sababu ndiyo dawa ya kila kitu.
Jambo lingine ni kuwa hutakiwi kumlazimisha mwenzi wako kuwa kama unavyotaka wewe lakini si vibaya kumshauri akawa na muonekano ambao unakuvutia. Labda anavaa akiwa anaacha wazi maungo yake, haitakiwi upandwe na jazba kisha kumtolea maneno makali, kaa naye mjadili mavazi sahihi.
Mapenzi ni diplomasia, hivyo wewe zungumza halafu muachie nafasi na yeye aseme linalompendeza. Hakikisha hutumii maneno ya kuudhi katika mazungumzo yenu. Vilevile na yeye anapaswa kudhibiti hasira zake. Mwisho mnakubaliana kwa upendo. Vuta picha inavyokuwa, mapenzi yanataka hivyo.


3. UNARUHUSIWA KUULIZA
Kuna jambo linakutatiza au umeona mwenzi wako anawasiliana na watu ambao huwaelewi, inawezekana pia akawa karibu na mtu wa jinsi yako, kwa hiyo unahisi kwamba unaweza kuibiwa. Suluhu hapo siyo kukaa na msongamano wa vitu kichwani, keti naye ukiwa na hali ya utulivu kisha muombe akupe ufafanuzi.
Kama una hasira usizungumze naye kwa sababu inaweza kuharibu maana. Siku zote, mazungumzo ya uhusiano wa kimapenzi, huendeshwa kwa njia ya upendo. Kama unahisi mbele utapandwa na jazba endapo hutapokea majibu mazuri, vema ungoje siku utakayokuwa na utulivu wa kutosha.
Usiyafanye mazungumzo yenu kuwa mahojiano. Jiweke kwenye kipengele cha mapenzi, kwa hiyo wewe siyo polisi. Pengine majibu yake yakawa siyo ya kunyooka, unachotakiwa kufanya ni kumuelewa au pale anapokuwa anasitasita, jaribu kumuongoza kuelekea kwenye jibu ambalo litasaidia ujenzi wa uhusiano wenu.
Hasira, jazba, ukali na mikunjo ya sura yako, vinaweza kumfanya ashindwe kukupa majibu sahihi.

SIKU zote naomba uzingatie ushauri niliokupa wiki iliyopita kuwa tabia ya kukusanya mambo mengi na kutaka majibu kwa wakati mmoja ni mbaya, kwani hutoa picha kuwa umemkamia kwa maswali, kwa hiyo mwisho wake atakuona una gubu.
Ishi kwa upendo, tatua mambo yako kidiplomasia. Usikubali uonekane una gubu, kwani hiyo ikipita itakufanya mapenzi yakushinde. Hata kama kuna mambo yanakuumiza kichwa, jitahidi uelekeze majadiliano yako kwa jambo lililopo mezani tu.
Ni mbaya sana suala la kwanza limekwisha, wewe uibue jambo la miaka mitatu iliyopita, eti nalo unalitakia majibu. Au unamkumbusha: “Unakumbuka mwaka jana, uliwahi kufanya hivihivi.” Kufanya hivyo ni makosa.


2. USIISHI KWA DHANA
Hutokea mtu ameketi, ghafla anaanza kusumbuliwa na mawazo kuwa mwenzi wake yupo sehemu ya hatari akifanya mambo yasiyokubalika. Hili ni tatizo la wivu ambalo huwatesa wengi, hivyo kuelekea kukamilisha mada hii, nakutaka uachane na maishi ya dhana. Tafsiri matukio.
Dhana ikitawala maisha yako, utakuwa unapenda kutuhumu bila hoja. Mbele ya safari ya maisha yako ya kutuhumu, utajikuta ni mwingi wa mawazo na kujiumiza moyo pasipo maelezo yoyote. Hujawahi kumfumania mwenzi wako lakini humuamini tu. Hii inamaanisha wewe mwenyewe hujikubali.
Tambua kuwa kama unafikiria mabaya kwa mwenzi wako bila sababu, hiyo ni dalili ya kukosa uaminifu. Mantiki hapa ipo kwenye hoja kuwa kuwaza kwamba mwenzi wako anafanya madudu, inamvunjia heshima, vilevile nawe unakuwa kwenye kapu baya, kwani si muaminifu. Jihadhari na tatizo hilo.
Unaweza kupona kwenye kipengele kuwa si muamifu kama kuna jambo aliwahi kukufanyia, hivyo ukamtoa imani. Hata hivyo, muongozo kwako uwe kwenye ukweli kuwa kama mlishaketi, mkazungumza na kukubaliana kusameheana, hutakiwi kutomuamini, kufanya hivyo ni kujiumiza. Usiishi kwa wasiwasi.
Kuna msemo: Aliwazalo mjinga ndilo linalomtokea. Maana yake ni kuwa matukio ambayo unaweza kuyaunga kwenye ubongo wako, ni rahisi kukutokea. Hutakiwi kuwaza mabaya, hebu tafakari mambo katika sura chanya. Mheshimu mwenzi wako naye akupe heshima yako unayostahili.
Ikiwa utawaza mambo mabaya, inawezekana ukamgombeza. Ukamnyima raha. Maswali yakawa mengi, huku ukimjaza tuhuma lukuki. Mwisho wa kero zake, naye atakasirika, hivyo ikiwa ana akili chafu, anaweza kufanya kweli ili unayowaza yatimie.
Unaweza kumpigia simu mwenzi wako lakini akashindwa kupokea. Usikimbilie kufikiria yupo hotelini anafanya uchafu, fikiria kazi zake kuwa ni nyingi. Baadaye akikupigia, usipande jazba kuwa hakukupokelea simu yako, zungumza naye kwa upole, kama ni maswali muulize kwa lugha iliyo laini.
Anza leo kufanyia kazi hili: Umempigia simu mwenzi wako, hajapokea. Baadaye ukimpata hewani au akikupigia, kabla ya kuzungumza lolote, unaanza kumpa pole kwa kutingwa na mambo mengi mpaka akashindwa kupokea simu ulipompigia. Hiyo ina maana kubwa, inaepusha migogoro.
Ipo wazi kuwa ubongo wa mtu mwenye wivu, hufikiria kwamba anasalitiwa kila anapopiga simu ya mwenzi wake na kutopokelewa au kuchelewa kupokelewa. Hawezi kufikiria kama mpenzi wake anaweza akawa amepata ajali. Kama simu haipatikani, hatafikiria kuwa betri imekufa. Atawaza mambo mabaya tu.

1.TAFAKARI NI KWA NINI UNA WIVU
Je, kuna kitu kilitokea nyuma kwenye uhusiano wenu ndiyo maana umeondoa imani juu yake? Unaogopa kwamba kuna jambo litatokea? Kwamba mpenzi wako ataanzisha uhusiano na mtu mwingine au atakuacha jumla? Wivu hautakiwi lakini ni ukweli usio na shaka kuwa matukio ya nyuma hukaribisha wivu.
Inawezekana mtindo wa maisha ya mwenzi wako yakawa kichocheo cha wewe kumuonea wivu. Ikiwa umetafakari na kugundua hivyo, muweke chini mzungumze. Muweke bayana kwamba anatakiwa kubadilika ili nafsi yako iwe na amani kamili.
Pengine kwenye uhusiano uliopita ulitendwa. Ukafanyiwa mambo mabaya mpaka ukajihisi huna thamani. Sasa unahisi hata huyo uliyenaye anaweza kufanya yaleyale yaliyokuumiza. Katika hilo, una haki ya kuona wivu kwa maana wanasema mtu akigongwa na nyoka, siku akiguswa na jani hushtuka.
Hata hivyo, katika hali kama hiyo wivu wako utakuwa unaongozwa na wasiwasi, hivyo unaweza kutulia kwa njia ya mazungumzo. Usikae na sononeko la moyo, zungumza na mpenzi wako kwenye kila jambo ambalo unahisi lina kukwaza. Inawezekana kwako ni kubwa lakini mbele ya mwenzi wako ni dogo na ufumbuzi wake ni rahisi.
HITIMISHO
Kujua jinsi ya kuikabili hali yako ya wivu itakusaidia kwenye maisha yako. Na unapaswa kulitilia mkazo kabla wivu haujaharibu uhusiano wako. Ni watu wachache mno wanaoweza kuwa hawajijui kama wana wivu au la, kwa hiyo ni rahisi kuukabili kwa sababu ni rahisi mhusika kujijua.
Je, umewahi kuona alama za wivu ndani yako? Umefanya nini sasa? Rejea matoleo ya makala haya kuanzia mwanzo, utakuwa

Related Posts by Categories



No comments:

Post a Comment