KUNA baadhi ya watu kati yetu ambao wanaweza kufuga mawazo ya kuachwa na wapenzi wao kwa miaka mitano mfululizo, huku wengine wakitumia miezi mingi kuondokana na huzuni iliyotokana na kutukanwa na wazazi, kufokewa na bosi, kupata hasara katika biashara, kufeli mitihani na kadhalika.
Hii ina maana kuwa ni wachache kati yetu tunaofahamu namna ya kupambana na mawazo yanayotuhuzunisha na kuyashinda. Kwa kuzingatia umuhimu ule ule wa furaha niliokwishaueleza kwenye moja ya kati ya mada zangu, nimeona ni vyema nikawafundisha hatua za kuondokana na mawazo yanayoumiza yatokanayo na matukio ya kuhuzunisha.
Mtu anapojikuta katika mawazo ya kuhuzunisha, lazima aanze kwa kurekebisha kwanza mhemko wake kwa kushughulikia mfumo wa upumuaji. Unapoletewa taarifa mbaya, moyo hushtuka na kuufanya uende mbio, hivyo ili kuurudisha katika hali yake ya kawaida, unatakiwa kuvuta pumzi kwa wingi ndani na kuzitoa nje pole pole. Hatua hii itasaidia kurudisha mapigo ya moyo katika hali yake ya kawaida.
Baada ya zoezi hilo, mwenye mawazo ya kuumiza anatakiwa kujilazimisha kutabasamu mara kwa mara, hata kama hawezi kufanya hivyo kwa wakati huo kutokana na tukio lililomletea mawazo mabaya. Kutabasamu husaidia kuchangamsha akili, ingawa inaweza kuchukua muda kurudi katika hali ya kawaida, lakini wataalamu wanasema inasaidia kuamsha hisia za furaha zilizokuwa zimeshambuliwa na mawazo mabaya.
Katika hali ya kawaida, uvamizi wa mawazo mabaya unapotokea hukuta mawazo mengine akilini na kuyaondoa, kisha yenyewe kuchukua hatua za kutawala akili.
unashauriwa baada ya kutekwa na mawazo hayo, chukua hatua ya kujilazimisha kurudisha akilini mawazo yaliyokuwemo awali kabla hujavamiwa. Lengo ni kutafuta nafuu na kufufua mawazo yenye kufurahisha.
Ikiwa wewe mwenyewe huwezi kufurahi baada ya kuchukua hatua hizo, wasaidie wengine waliopo karibu yako kufurahi.
Kwa mfano, unapokuwa kwenye msiba unalia, chukua jukumu la kuwanyamazisha wenzako na kuwapa faraja. “Nyamazeni kazi ya Mungu haina makosa,” ukifanya hivyo utakuwa umejisaidia wewe pia kuondokana na mawazo ya msiba yaliyokufanya ulie sana.
Watu wengi wanapokuwa na mawazo ya kuumiza, huwa wanadhani kuwa jukumu la huruma liko mikononi mwa watu wengine. Endapo wasipopata wa kuwaambia pole, huzidi kudumu kwenye msongo wa mawazo huku wakilalamika: “Tangu nimepata msiba, kaka yangu hajafika hata kunipa pole.”
Mawazo ya aina hii yakiongezwa kwenye mawazo, huzuni huzidi kuumiza zaidi, hivyo ni jukumu la mhusika kujihurumia mwenyewe na kujiuliza mwisho wa huzuni isiyokoma ni nini kama si kifo chake?
Baada ya kupoteza furaha, jambo jingine muhimu ni kuujali mwili wako kwa kula chakula kizuri, kunywa maji na kujitibu kama mawazo yako yameacha maumivu ya kichwa au mwili! Lakini jambo la kushangaza watu wengi wanapokuwa na mawazo hususa hata kula, jambo ambalo hudhoofisha afya zao na kuwaongezea matatizo zaidi.
Namna nyingine ya kukabiliana na mawazo ya kuumiza ni kupunguza hasira juu ya watu wengine. Katika hali ya kawaida, matukio mengi husababishwa na watu.
Kumkasirikia mtu aliyekusaliti, aliyekufilisi au anayekuroga ni adhabu nyingine kubwa unayojipa mwenyewe, hivyo ili ufanikiwe kuondokana na msongo wa mawazo ni vyema ukawa mtu wa kusamehe na kutokuwa na hasira na watu wengine ambao unadhani ndiyo chanzo cha matatizo yako.
Unapokuwa na mawazo yanayoumiza na baadaye ukafanikiwa kuyaacha, usikubali kuyarudia. Lakini watu wengi wanaoumizwa na mambo fulani huwa hodari sana kuyatunza akilini mwao na kuyarejea kila mara, jambo ambalo huwafanya waumizwe na mawazo hayo kwa muda mrefu bila kupumzika.
Yaliyotokea yamepita, achana nayo na usikubali akili yako iyarejee tena.
Ikiwa umekuwa na mawazo ya kuumiza kwa muda mrefu kwa sababu umefeli mtihani, umeshindwa kufanya jambo fulani au mtu kakuudhi, hebu badili mawazo hayo ya kushindwa na ufikirie kushinda katika siku za usoni.
Kwa mfano, kama hujazaa mtoto na ungependa kuwa naye, onja furaha hiyo kwa kusema mwaka ujao utampata. Hatua hii itakusaidia kuitumikia furaha hata kama katika hali ya kawaida hujaipata na hivyo kusogeza mafanikio yako karibu zaidi.
Yapo baadhi ya mambo ya kuhuzunisha ambayo hutukumba bila kutarajia na hivyo kutuletea mawazo. Njia pekee ya kuyaepuka mawazo ya aina hii ni pamoja na kukubali tukio husika.
Wengi wetu tunapofiwa kwa mfano, huwa hatukubali kuamini kilichotokea, matokeo yake ni kuumia kwa muda mrefu. Unapokuwa na tatizo, kwanza likubali kuwa limekupata kisha chukua hatua za kufaa kulikabili.
Saturday, March 17, 2012
Msongo wa mawazo na jinsi ya kukabiliana nao
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment